Maoni ya Katuni
Jitihada kubwa za kuhimiza amani na usalama
kudumishwa nchini zimekuwa zikifanywa na viongozi wa ngazi mbalimbali
katika nyakati tofauti.
Makundi mbalimbali ya kijamii yamekuwa yakihamasishwa kila wakati
kuimarisha umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania wote bila
kujali tofauti za kidini, rangi, kabila, jinsia na maeneo ya uzawa.
Wakati huu ambapo Watanzania wamekuwa
katika sherehe za Eid El Fitr, viongozi wa kitaifa wameshiriki katika
ibada hizo kwa kuwakumbusha Watanzania kutokukubali umoja wetu
kusambaratishwa kwa vigezo vya mitafaruku ya udini.
Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal
wakati akizungumza katika Baraza la Eid El Fitr mjini Tabora juzi,
alisisitiza kuwa Watanzania wakatae kabisa kugawanywa kwa misingi ya
udini na kwamba ni busara kwa waumini wa dini na madhehebu kujenga
utamaduni wa kuvumiliana hasa zinapotokea hitilafu miongoni mwao.
Dk. Bilal alitumia fursa hiyo kuwaasa
Watanzania kumaliza tofauti za kidini kwa kukaa pamoja na kutafuta
muafaka kwa njia ya majadiliano ya amani na upendo pasipo kutawaliwa na
jazba wala chuki, huku akiwakumbushia waumini wote kauli na angalizo la
Rais Dk. Jakaya Kikwete kuwa vita vya dini havina mshindi.
Makamu wa Rais aliwakumbusha Watanzania
kuwa pamoja na Tanzania kuwa kisiwa cha amani, baadhi ya mataifa
hayatutakii mema, yanatuangalia kwa jicho la husuda na kutuombea mabaya.
Aidha, wanatuombea tufike mahali
tuharibikiwe ili wao wafurahi, suala ambalo endapo tutashikamana na
kuzitupilia mbali tofauti zetu, hilo halitatokea kwani katu "dua la kuku
halimpati mwewe".
Alisisitiza kuwa amani katika taifa au
jamii yoyote ni sharti la kwanza katika mchakato wa kuleta maendeleo,
hivyo ana imani kuwa viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kusaidia
kujenga maadili mema katika taifa hili na kwamba watu wakishiba imani
ndani ya nafsi zao na wakaelewa na kuzingatia mafundisho, maovu
yataondoka miongoni mwao.
Wito wake kwa viongozi wa dini na
madhehebu yote nchini ni wahakikishe kuwa wanatumia nafasi zao vyema
kuwajenga waumini wao kimaadili, ili wawe raia bora watakaosaidia
kudumisha na kuendeleza sifa na heshima ya taifa letu kuhusu kutunza na
kuilinda amani.
Tukio la kumwagiwa tindikali kwa wasichana
wawili raia wa Uingereza huko Zanzibar wiki hii ni moja ya matukio
yanayoliweka taifa katika sura mbaya duniani, na tayari baadhi ya vituo
vya runinga kama CNN vimelitangaza tukio hilo kwa uzito mkubwa.
CNN kupitia kipindi chake cha Out Front
imeonesha kuwa Tanzania siyo salama tena na kwamba watu wanaotaka
kutembelea nchini humu, lazima wachukue hatua za tahadhari. Hayo yote
yanatuhusu kama taifa kupambana nayo kwa gharama yoyote.
Binadamu wote humheshimu na kumwogopa
Mungu, viongozi wa dini wanamwakilisha Mungu katika kuwaongoza waumini
wao hapa duniani ili waishi kwa imani na matarajio kama inavyoagizwa
katika vitabu vya madhehebu yao. Na kwa uhakika, hakuna dhehebu
linalohamasisha waumini wake watende dhambi na kumuasi Mungu, kwao
amani, upendo na kuheshimiana ni kipaumbele kikuu kwa madhehebu yote.
Tunaamini kuwa viongozi wa dini ni mhimili
mkubwa katika kutatua tofauti za kidini, na ndiyo maana tunazo sababu
za kumpongeza Makamu wa Rais kwa wito alioutoa kwa viongozi wa dini
kumaliza tofauti zilizopo kwa kuzungumza bila jazba wala hasira.
Viongozi hao ndiyo dira kwa waumini wao, viongozi wa dini wanao uwezo
mkubwa wa kushawishi na kudumisha maelewano miongoni mwao.
Tunaamini pia kuwa nchi hii itabaki kuwa
nchi salama ya amani na utulivu na ambayo itaendelea kupigiwa mfano na
nchi nyingine. Uhuru wa kuabudu katika taifa hili umejengewa misingi
ndani ya Katiba na kutokana na ukweli huo, kila mmoja anapaswa kuheshimu
imani au dini ya mwenzake pasi na kujiona imani au dini yake ni bora
zaidi.
Yote hayo amewahi kuyasema pia mara nyingi
Rais wetu, Dk. Jakaya Kikwete kila anapopata nafasi ya kuzungumza na
viongozi wa madhehebu ya dini mbalimbali nchini kuhusu mustakabali wa
amani ya taifa letu. Amani hii ni tunu, tuilinde kwa nguvu zetu zote.
Mungu ibariki Tanzania na watu wake.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment