Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dr:Ali Mohd Shein
KATIBU Mkuu Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Dk Khalid Mohamed amependekeza nafasi ya
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika Muungano itazamwe upya na kuondoa
kero za Muungano.
Dk Mohamed alisema hayo
alipotoa maoni mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba jana, kwa niaba ya
Watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Huku akisisitiza kuwa
maoni hayo si msimamo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bali ni maoni ya
Watumishi wa ofisi hiyo, alisema Katiba Mpya itazame upya nafasi hiyo ili iwe
kama Hati za Muungano zinavyosema.
“Wakati Rais Nyerere
(Julius) na Rais Abeid Amani Karume wanakubaliana kuunda Muungano, kuna mambo
walikubaliana katika hati hiyo ya Muungano, kwamba Rais Nyerere awe Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar, Abeid Amani Karume kuwa
Makamu wa Rais katika Serikali ya Muungano,’’ alisema DK Mohamed.
Dk Mohamed alifafanua kuwa
Katiba ya sasa haionyeshi wala kumpa nafasi yoyote Rais wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika masuala ya Muungano, hivyo tumependekeza katika
Katiba ijayo nafasi yake itazamwe upya.
Mbali na hilo, Dk Mohamed
alisema pia wamependekeza mambo ya Muungano yatazamwe upya katika Katiba ijayo
ili kuondoa malalamiko yaliyopo baina ya pande mbili za Muungano.
Alisema kwa sasa mambo ya
Muungano yapo 22, lakini kiukweli ni zaidi ya hayo yaliyopo sasa kwa sababu
utakuta jambo moja lina mambo mawili au zaidi.
Alisema ili hilo
lifanikiwe ni lazima pande zote mbili za Muungano zikutane na kuainisha kwa
uwazi ni jambo lipi linalohusu Muungano na mipaka yake ijulikane ili kufanya
Muungano uwe imara.
“Kubainisha mambo ya
Muungano na mipaka yake ni jambo la muhimu wakati huu ambao tunataka kuandika
Katiba yetu, kwa kufanya hivyo tutaweza kupata mifumo ya kikatiba ambayo
itasaidia kutekeleza mambo ya Muungano,” alisema Dk Mohamed.
Alisisitiza kuwa ili
kufanya Muungano kuwa imara Katiba ijayo iweke vyombo vya kusimamia mambo ya
Muungano ambavyo vitakuwa na sura ya kimuungano.
“Sura ya Muungano itakuwepo pale ambapo viongozi na watumishi wa vyombo hivyo
vya Muungano watakuwa wanatoka katika pande zote mbili za Muungano na kwa
uwiano sawa,” alisema.
CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment