NA MUHIBU SAID
Ripoti ya uchunguzi dhidi ya maofisa watatu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeibua mapya baada ya kubaini kuwa wafanyakazi wengine zaidi ya 30 wa shirika hilo wanatakiwa kuhojiwa kutokana na kuisababishia Tanesco hasara ya mamilioni ya fedha.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco, Jenerali mstaafu Robert Mboma, akizungumza na NIPASHE jana, alisema kuwa CAG amekabidhi rasmi ripoti ya uchunguzi wa maofisa watatu wa shirika hilo waliosimamishwa kazi kutokana na tuhuma mbalimbali.
Maafisa ambao walikuwa wakichunguzwa ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji (Huduma), Robert Shemhilu; Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi (Manunuzi), Harun Mattambo.
Maafisa hao pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, William Mhando, walisimamishwa kazi Julai 14, mwaka jana na Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco.
Baada ya kuwasimamisha kazi kwa maafisa hao, Bodi ya Tanesco ilimpa CAG jukumu la kuchunguza tuhuma zilizokuwa zinawakabili.
Jenerali Mboma alisema kuwa ripoti waliyokabidhiwa na CAG, imebaini kuwa kuna wafanyakazi zaidi ya 30 wa Tanesco ambao wamelisababishia shirika hilo hasara hivyo wanatakiwa kuhojiwa ili watakaobainika hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Jenerali mboma alisema kuwa wafanyakazi hao wanatuhumiwa kuhusika kufanya malipo yaliyotakiwa kufanywa kwa dola za Marekani, lakini yakalipwa kwa Shilingi na kuongeza kuwa walibadilisha dola hizo katika benki ambazo Tanesco haizitumii.
Mwenyekiti huyo alifafanua kuwa kwa mujibu wa utaratibu uliopo, kubadilisha dola kuwa Shilingi kulitakiwa kufanyike katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) au katika benki yoyote ambayo Tanesco inaitumia, lakini wafanyakazi hao waliamua kutumia benki nyingine na kusababisha Tanesco kupata hasara ya mamilioni ya fedha.
Hata hivyo, Jenerali Mboma hakutaja kiasi cha fedha ambazo Tanesco imepata hasara kutokana na wafanyakazi hao kukiuka utaratibu huo.
Jenerali Mboma alisema katika ripoti hiyo ya CAG, kasoro nyingine zilizobainika ni kukiukwa kwa Sheria ya Manunuzi ya Umma na wizi wa umeme ambao baadhi ya wafanyakazi wa Tanesco wananufaika nao.
Alisema katika kukabiliana na tuhuma hizo, Bodi ya Tanesco inakusudia kuunda majopo mawili ya wataalam ambao watasikiliza kesi hizo ili wahusika waitwe kuhojiwa na wajitetee kutokana na tuhuma zinazowakabili.
Aliongeza kuwa jopo la kwanza litakaloundwa litawahusisha watu wa ngazi za juu ambao ni wateule wa bodi na la pili ni wale ambao wapo chini na hawateuliwi na Bodi.
Jenerali Mboma alisema majopo hayo yatawahoji maofisa waliosimamishwa tangu awali na wafanyakazi wengine 30 ambao wamebainika kuhusika katika kashfa hizo na baada ya hapo hatua zaidi za kisheria zitafuata.
Maafisa hao walisimamishwa kazi tangu Julai 14, mwaka jana na Bodi ya Tanesco sambamba na Mhando ambaye baada ya uchunguzi dhidi yake kukamilika, Bodi ilimfukuza kazi.
Baada ya kuwasimamishwa kazi maafisa hao, Bodi ya Tanesco ilimpa kazi CAG kuchunguza tuhuma zilizokuwa zinamkabili Mhando.
Baada ya CAG kukamilisha uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Mhando, Bodi ya Tanesco ilitangaza kumfukuza kazi rasmi Mhando Oktoba 29, mwaka jana baada ya kubainika kutenda kosa la kuingia kwenye mikataba yenye mgongano wa kimaslahi.
Hata hivyo, Bodi ilisema kwa kosa alilolifanya Mhando, hawezi kushtakiwa mahakamani kwa sababu makosa aliyoyafanya ya kuingia kwenye mikataba yenye mgongano wa kimaslahi ambalo ni kosa la kiuadilifu.
Hivi karibuni, Jenerali Mboma, alisema uchunguzi dhidi ya maafisa hao utakapokamilika na kukabidhiwa na CAG, Bodi itateua jopo la watu watatu kuipitia na kisha kutoa uamuzi wa hatua za mwisho za kuchukua dhidi ya maafisa hao.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment