NA MUHIBU SAID
Nyota za utendaji kazi wenye ufanisi serikalini za mawaziri; Dk. Harrison Mwakyembe (Uchukuzi), John Magufuli (Ujenzi) na Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), zimetabiriwa kuwa zitazidi kung’ara na kuungwa mkono na wananchi, huku akisema kuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, atashinda kiti cha urais wa nchi hiyo Machi, mwaka huu.
Kadhalika, Rais Jakaya Kikwete, akitabiriwa pia kufanya maamuzi magumu yakayoishangaza dunia, katika mwaka huu.
Utabiri huo ulitangazwa na mrithi wa kazi za aliyekuwa Mnajimu Mkuu Afrika Mashariki na Kati, Marehemu Sheikh Yahya Hussein, Maalim Hassan Yahya Hussein, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.
Maalim Hassan, ambaye ni mtoto wa Sheikh Yahya Hussein, alisema utabiri huo unaohusisha matukio ya kisiasa, kibiashara na jamii, aliyosema yatatokea mwaka huu, umezingatia kwamba, mwaka huu ulianza siku ya Jumanne, ambayo alisema inatawaliwa na Sayari ya “Mars” au “Mariikh”.
Alisema nyota za sayari hiyo ni mbili; ambazo ni “Punda au “Aries” na “Nge” au “Scorpio” na kwamba, kinyota, nyota hiyo ni ya mwanzo, ambayo ndiyo kichwa na kama nyumba ya mwanzo na kwamba, maana yake ni mwanzo wa jambo, “Anza jambo”, “Tangaza jambo” au “kupata mafanikio”.
HAKUNA RAIS MWANAMKE 2015
Kutokana na nyota hizo, alisema haitawezekana kamwe kwa Tanzania kuongozwa na rais mwanamke baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Alisema mbali na kufanya maamuzi magumu, Rais Kikwete atafanya mambo ya ajabu na yasiyotabirika na kuungwa mkono kwa asilimia 100 na wananchi wote wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Maalim Hassan alisema Rais Kikwete pia ataendelea kupata wasaidizi sadifu, hasa kwa upande wa uwaziri.
“Vilevile, nyota za mawaziri Harrison Mwakyembe, John Pombe Magufuli na Khamis Kagasheki zitazidi kung’ara mwaka huu na kuungwa mkono na wananchi,” alisema Maalim Hassan.
Alisema nchini Kenya, Muungano wa Cord ukiongozwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Raila Odinga, katika Uchaguzi Mkuu ujao, utashinda na kuwabwaga Uhuru Kenyatta na William Ruto na Muungano wao wa “Jubilee” na ule wa Musalia Mudavadi wa Amani.
Alisema uchaguzi huo wa Kenya unaotarajiwa kufanyika nchini humo, Machi, mwaka huu, utafanyika kwa amani na utulivu.
Alisema pia Rais Kikwete ataunganisha nchi na kuwa moja yenye uimara wa utaifa kuliko watangulizi wake na atashirikiana zaidi na wanasiasa na viongozi wa dini kuondoa mtikisiko wa uvunjifu wa amani uliokuwapo nchini mwaka jana.
Pia alisema kuna chama cha siasa nchini kitachochea kujitenga na kuunda taifa lake, lakini kusudio hilo halifanikiwa kwani litapingwa na Watanzania wote kwa kauli na vitendo.
WABUNGE KUUNGANA
Vilevile, alisema wabunge wengi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wataungana katika masuala yatakayohusu utaifa bila kujali itikadi za kivyama au kimajimbo.
Hata hivyo, alisema nyota zinaonesha pia kuna baadhi ya wabunge wataanguka bungeni wakati wa majadiliano, lakini akasema kinyota haionekani kuwa kutakuwa na athari na kushauri juhudi za ziada kufanyika ili kuokoa maisha yao.
TANZANIA KUISHINDA MALAWI
Alisema pia Tanzania itashinda kwa kishindo kwenye mgogoro wake na Malawi kuhusu Ziwa Nyasa bila nchi hizo kupigana na sakata la gesi ya Mtwara litatulia kwa amani kwa wananchi wote kuungana na kuunga mkono matumizi yake kwa faida zaidi ya taifa badala ya jimbo au majimbo.
Pia alisema viongozi wengi, wakiwamo wabunge, wakuu wa mikoa, wilaya, wenyeviti wa vyama na makatibu wao, watatoa matamshi ya utatanishi na kusababisha hofu na mitafaruku mikubwa itakayowafanya watu kupigana.
Hata hivyo, alisema hali hiyo itadumu kwa muda mfupi, kwani baadhi ya viongozi watalazimika kukaa pamoja na kukubaliana mambo baina yao na kurejesha hali ya utulivu na amani.
Pia alisema mwaka huu, ambao una namba 2013, namba mbili za mwisho, ambazo ni 13 ukizijumlisha unapata 4, ambayo ni nyota ya “Kaa” au “Cancer” inayohusika na kilimo, mapenzi, unyonge, kufanya vitu kwa vishindo, siri na kuvumbuka kwake, kuvunjika biashara na kutimia kwa haja, mvua na mafuriko na majanga ya asili.
Hivyo, akasema katika mwaka huu, ndoa nyingi zitavunjika na watu wengi, wakiwamo mawaziri na viongozi wanaume na wanawake, watajikuta katika kashfa ya ngono, kufumaniwa au kufumania na kupigana kiasi cha baadhi yao kuuawa.
Hata hivyo, alisema maisha yatakuwa mazuri, lakini kwa Watanzania watakaojifunga mikanda kuelekea katikati ya mwaka huu, lakini maradhi ya watoto yataongezeka, hasa ya kifua na kichwa.
Alisema pia ajali zitakuwa nyingi, kuchafuka kwa bahari kutakuwako kwa wingi na kutakuwa na hofu ya watu wengi kuuawa.
Pia itatokea mioto mikubwa kwenye miji mikubwa, njaa kuongezeka, ukosefu wa maadili, wafanyakazi kuwapiga mabosi wao na uongo mwingi kwa maana ya propaganda.
Alisema pia umbeya utakuwa kwa kiwango kikubwa, masengenyo na vifo vya mashujaa au wale watakaojiona ni mashujaa.
Pia alisema kutakuwapo wingu zito la vifo vya ghafla kwa watunzi wa hadithi na vitabu, waandishi wa habari, wanasiasa na wasanii na kwamba, muda huu utakuwa mbaya zaidi ya mwaka jana.
Pia alisema mauzo ya bidhaa yataongezeka na kuongeza neema na watu kufaidika katika biashara. Pia mwisho wa mwaka huu mvua zitaongezeka, mazao yatakuwa mengi na wafanyabiashara wengi hasa wajasiriamali watafanikiwa katika kazi zao.
Alisema neema pia itawaangukia wajariamali wa aina zote nchini na wawekezaji wengi zaidi watajikita kwenye biashara ndogondogo kulikoilivyokuwa katika miaka iliyopita.
Vilevile, alisema mwezi utapatwa Aprili 25, ambayo itakuwa Alhamisi, Mei 25 (Jumapili) na Oktoba 18 (Ijumaa). Pia jua litapatwa Mei 10 (Ijumaa) na Novemba 3 (Jumapili).
Alisema siku hizo, zina athari ya moja kwa moja kwa maisha ya wanadamu, wakati Alhamisi inatawaliwa na Sayari ya Jupiter, ambayo inahusika na serikali, wizara, safari na magomvi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment