BAADHI
ya masuala ambayo nimekuwa nikiyajadili yanajitokeza hivi sasa kwa mshindo
mkuu.
Nimekuwa
nikisema kwamba tunajitahidi mno kujenga taifa dogo ndani ya nchi kubwa. Hili
linadhihirika sasa. Nimekuwa nikisema pia kwamba tunaonekana kuwa na haraka ya
kufanya mambo kama vile tunakwenda kwingine, hapa si kwetu na wala hatujafika.
Hili nalo linajionyesha.
Hivi
sasa tumetekwa na kelele zinazopigwa kuhusu gesi asilia inayochimbwa kusini mwa
Tanzania, na tayari tumeanza kuona dalili za nchi kuparaganyika kutokana na
‘utajiri’ huo.
Tunachokishuhudia
si mjadala wa jinsi gani tunaweza kunufaika kama taifa kutokana na gesi
inayochimbwa nchini ( na pia utajiri mwingine unaotokana na rasilimali za nchi)
bali ni ghadhabu za makundi hasimu yanayokinzana kuhusu namna ya kugawana
kidogo tulicho nacho.
Kwa
muda sasa, wataalamu duniani wamekuwa wakijadili kile kinachoitwa ‘resource
curse’, au laana ya rasilimali. Hii ni laana ya nchi kama yetu ambazo
zinajikuta zikiwa na rasilimali kubwa, lakini badala ya rasilimali hizo kuzinufaisha
nchi hizo inageuka kuwa ni balaa, laaana. Hili ndilo linaelekea kutokea hapa
nchini.
Bado
hatujui kwa uhakika ni kiasi gani cha gesi asilia tulicho nacho. Nimesoma
mahali kadhaa kwamba gesi hii ni nyingi mno na inaweza ikaifanya Tanzania kuwa
mojawapo ya nchi zenye machimbo ya gesi makubwa duniani. Bila shaka hilo
lingekuwa jambo jema kwa nchi inayoendeshwa kwa utaratibu unaoeleweka na
inayojadili masuala muhimu kwa uwazi wa kutosha.
Kwa
bahati mbaya, hii si kweli. Tumekuwa tukishuhudia usiri unaogubika mikataba juu
ya rasilimali nyingine kwa muda mrefu sasa, na hakuna dalili kwamba tutaanza
kesho au keshokutwa kuwa wawazi zaidi.
Hadi
leo serikali inakataa kuanika hadharani maudhui ya mikataba inayoingia kwa
niaba ya Watanzania, na serikali ikiulizwa inajibu kwamba mikataba hiyo
ni siri baina ya serikali na ‘ wawekezaji.’
Hii ni
mantiki iliyopinda, kwa sababu rasilimali za nchi si mali ya serikali, ni mali
ya wananchi na serikali inatakiwa ifanye kazi ya kuzisimamia kwa niaba ya
wananchi wake, waliopo na watakaokuja baadaye. Serikali kujifanya inaweza
kutoa, kugawa, kuuza au kuhaulisha mali hizo bila wenye mali kujua nini
kimefanyika kwa sababu ni siri kati ya serikali na ‘mwekezaji’ ni sawa na
msimamizi wa shamba kumwambia tajiri wake kwamba ameuza ng’ombe wake lakini bei
ya mauzo hayo ni siri kati ya bwana-shamba na mnunuzi. Uliona wapi jambo kama
hilo ?
Jazba
zimepanda, ghadhabu zinazidi kuumuka, kimsingi kwa sababu tunakabiliwa na
nakisi ya imani. Wananchi wengi hawaiamini serikali yao kwa sababu wamezoea
kuiona ikiwatendea kinyume cha haki, na mara kadhaa imedhihirisha udhaifu wake
katika kusimamia rasilimali za nchi.
Iliwahi
kutokea waziri mhusika wa sekta ya madini alitembelea machimbo ya dhahabu,
akapitishwa sehemu kadhaa, lakini alipotaka kuingia chumba cha kuhifadhia
dhahabu akazuiwa kwa sababu za ‘kiusalama.’ Ungedhani waziri angefoka,
angelazimisha chumba hicho kifunguliwe au angejiuzulu. Mawe ! Alifyata
mkia, akarudi Dar es Salaam kimya kimya, na akaendelea na kazi yake ya uwaziri
bandia.
Wananchi
wa kusini wameiona serikali yao inavyofyata mkia kwa ‘wawekezaji’ katika
maeneoe mengine, na hawana imani kwamba itawatendea haki. Na wala matamshi ya
wakuu wa serikali hayasaidii kutuliza hisia. Waziri anapowaambia wananchi
wanompinga kwamba hawana elimu ya kuelewa nini kinaendelea, ni nani hasa
anakuwa hana elimu, wananchi au waziri mwenyewe ?
Mkuu
mwingine anaposema kwamba wapo watu wanaotaka kuingiza siasa katika masuala ya
maendeleo, hajui kwamba masuala yote ya maendeleo ni masuala ya kisiasa?
Binafsi huwa najiuliza mara kwa mara, hivi hawa watu wamejifunza nini na
wapi kuhusu siasa na uendeshaji wa nchi na uchumi wake ?
Zipo
shutuma kwamba mradi wa kujenga bomba ni ‘dili’ ya watu fulani, na kwamba
umebambikizwa gharama maradufu ili wajanja wapate mgawo wao. Sina uhakika
kuhusu hilo, lakini siwezi kushangaa kama ni kweli kwani hivyo ndivyo
tunavyoenenda. Wizi, ubadhirifu, utapeli, ulaghai, uchakachuaji, udhalimu na
udanganyifu vimekuwa ni sehemu ya utamaduni wa utawala wetu, hadi nimesoma mahali
ikipendekezwa kwamba mbinu hizi zingefundishwa shuleni.
Naangalia
mbele tunakokwenda, na ninachokiona ni giza kwa sababu sioni umakini wa
watawala wetu katika kuhimili vishindo vya wakubwa wa dunia hii mbele ya
utajiri mkubwa wa rasilimali kama gesi na mafuta ya peteroli. Wababe wa dunia
wanaodhibiti biashara hii hawana huruma wala uvumilivu kwa vijinchi vyetu
vinavyoendeshwa kama NGO.
Hata pale wanapopambana
na miamba wanaotetea maslahi ya mataifa yao, wababe hawa hawasiti kuchukua
hatua kali, ikiwa ni pamoja na kuondosha serikali inayowapinga na kuweka ya
kwao. Anayetaka kujua zaidi akasome kuhusu waziri mkuu wa Iran, Mohammad
Mosaddegh na mchezo aliofanyiwa na the Seven Sisterskatika miaka ya
1950.
Inaelekea
tunacheza mchezo wa hatari kwa kukabidhi masuala mazito kwa watu wepesi, lakini
iko siku tutakuja kujuta na kusaga meno. Madhara yake ni makubwa na yanaweza
yakazua zahma ambayo tuliamini kwamba sisi, kama Watanzania, tumejijengea kinga
dhidi yake.
Katika
miaka ya 1970 waziri wa mafuta wa Venezuela, Perez Alfonso, aliwahi
kusema kwamba mafuta ya pateroli ni « Kinyesi cha
Shetani » na ni ukweli ulio wazi tukiangalia nchi kama Nigeria,
Kongo-Brazza, Gabon, Angola na Guinea ya Ikweta, nchi zenye mafuta mengi lakini
watu wake ni masikini hohe hahe na migogoro haiishi.
Hapa
kwetu tumeanza kushikana mashati kabla hata Shetani hajaenda msalani. tumesikia
harufu kidogo ya ushuzi wake tunatafutana. Akisha kwenda haja kubwa
itakuwaje ?
Source: Jenerali
Ulimwengu
No comments:
Post a Comment