CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kisipoangalia kitajikuta kinaupoteza mwaka 2013 kama kilivyofanya mwaka 2012 kwa kundelea kukilalamikia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Imefika wakati sasa inabidi wanasiasa na viongozi wa chama hicho wakae chini na kujiuliza ni kitu gani hawakifanyi kwa usahihi na ni kwa namna gani maamuzi yao na uongozi wao umechangia katika kuvuruga chama. Imetosha sasa kuendelea kukilaumu CCM kuwa kinatumia mbinu mbalimbali kukivuruga.
Siku chache zilizopita tumeshuhudia – hasa kwenye mitandao – kile ambacho kinaitwa “minyukano” ndani ya chama ambapo viongozi mbalimbali wa Baraza la Vijana wa CHADEMA pamoja na wengine kutoka ndani ya Sekretariati ya chama wakirushiana lawama za kila aina, tuhuma na kutajana kuwa ni mapandikizi na kuwa wanatumiwa na chama tawala kukivuruga chama.
Tumeshuhudia kweye mitandao hii viongozi mbalimbali wakijitokeza ama kwa majina ya au kwa makuwadi wao kutuma tuhuma dhidi ya wengine. Hakuna ambaye ameachwa salama. Kuanzia Mwenyekiti Freeman Mbowe, Katibu Mkuu Dk. Wilbroad Slaa, Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe na uongozi karibu mzima wa umoja wa vijana na hadi wale wa mikoani.
Hata kauli za baadhi ya viongozi wa kitaifa ambazo zimejaribu kuonyesha kuwa hakuna “mgogoro” zinatolewa huku zikithibitisha tu kuwa kuna tatizo ndani. Na hakuna kitu ambacho kimepoza kidogo malumbano hayo kama ushindi wa Godbless Lema Arusha baada ya Mahakama ya Rufani kumrudishia Ubunge wake ambao kama nilivyowahi kuandika kwenye gazeti hili ulifutwa kwa makosa makubwa.
Lakini siku chache kabla na baada ya uamuzi wa mahakama CHADEMA wamekuwa wakilumbana huku akitafutwa mtu wa kujaribu kutoa uongozi wa jinsi ya kutoka kwenye matope haya ya kashfa.
Bahati mbaya sana karibu wote wanaozungumzia malumbano haya wanazungumzia kwa kuitazama CCM. Kwamba mkorogano unaotokea ndani ya BAVICHA ni kwa sababu ya CCM, na kuwa tuhuma zinazotolewa ndani ya mitandao nazo zinatokana na uratibu wa uongozi wa CCM.
Sasa imekuwa kwamba hakuna baya lolote linalotokea ndani ya chama isipokuwa liwe limesababishwa na CCM. CCM imekuwa ndiyo chanzo na mwisho wa matatizo yote. Hakuna anayetaka kuangalia uongozi wa kitaifa na mfumo wa CHADEMA unavyochangia matatizo ndani ya chama hiki kikuu cha upinzani nchini.
Kwa baadhi ya watu ambao tumekuwa tukikiunga mkono yanayoendelea sasa yanatia kinyaa, yana kera na kuudhi kwa wakati mmoja na kwa kufuatana. Inaudhi kwa sababu inatisha huko mbele itakuwaje. Hivi kweli kwa mtindo huu na hali hii CHADEMA kinaweza kuingia madarakani? Na kikiingia kitatawala vipi?
Tujiulize jinsi ya migongano hii ya watu inavyoendelea itakuwaje kama chama kitashika madaraka? Mawaziri wake si watakuwa hawa hawa wanaogombana au kitaenda kukopa mawaziri CCM? Hivi leo kama wanashindwa kuheshimiana na kuwasiliana vizuri itakuwaje wakiingia madarakani, si itakuwa kile kile tunachoshuhudia ndani ya CCM hivi sasa?
Si tumeyaona ya mawaziri wasiopatana na siasa za visasi ndani ya watawala wa sasa? Si kwamba tunaanza kushuhudia mgongano ambao utaendelea baada ya CHADEMA kushika madaraka?
Lakini kinachokera zaidi ni kuwa uongozi wa taifa wa CHADEMA ni kana kwamba unapuuzia kinachoendelea. Kwamba wanakiona lakini wanasema wanategea ili wakusanye ushahidi zaidi. Yaani haya madudu yametokea kwa karibu miaka miwili sasa na wao bado wanajaribu kutafutana na kunyemeleana.
Sasa wamekuwa na haraka ya kushughulikia matatizo kwenye ngazi za chini na hasa mikoani lakini kwenye ngazi ya taifa wameendelea kubeba na kubebana hasa sasa yamekuwa kama povu la mbege iliyotingishwa sasa imefurika. Na matokeo yake wanaanza kutuonyesha tatizo ndani ya chama hicho. Tatizo ambalo inshallah itabidi tuliweke bayana kwani kuendelea kulifumbia macho ni kuwapa kibali Chaddema waje kututawala wapendavyo.
Hatari ninayoiona ni kuwa kwa vile CHADEMA kinapendwa na kinaamini kinapendwa basi hakitaki kujiangalia. Wanafanya kosa lile lile ambalo CCM walilifanya mara baada ya kurudi kwa mfumo wa vyama vingi. CCM kilikuwa na nafasi nzuri sana ya kujirekebisha na kujitengeneza upya lakini kiliamini kinapendwa.
Nakumbuka mara kadhaa CCM kilikuwa kikitamba kuwa ilikuwa ni kwa hisani yake vyama vingi vilirudishwa kwani wananchi wengi walioulizwa na tume ya kukusanya maoni juu ya vyama vingi walitaka kuendelea na chama kimoja (yaani CCM).
Ni katika ukungu wa kupendwa CCM ndipo kilipojikuta kinaanguka na kuanza kukataliwa; sera zake kubezwa, uongozi wake kupuuzwa na maono yake kudharauliwa.
CHADEMA nacho sasa kinajiweka katika hali ile ile ya CCM au nitolee mfano wa chama kingine. Kule Zambia kina Frederick Chiluba walisimama kuongoza mabadiliko dhidi ya utawala wa Kenneth Kaunda.
Chiluba alikuwa maarufu sana katika harakati za vyama vya wafanyakazi na alipoweza kumuangusha Ken Kaunda ilileta wimbi la hofu. Wananchi wa Zambia waliamini wamepata mkombozi. Muda haukupita kabla ya utawala wa Chiluba nao kuanza kuonekana ni ‘wale wale’. Na kweli tumaini la wananchi likapotea baada ya karibu miaka 20 ya utawala wa MMD wananchi wa Zambia wakaamua kuwaondoa.
Hawakurudisha chama cha Kaunda moja kwa moja bali walimleta Michael Satta ambaye alikuwa ndani ya MMD na akatoka baada ya kuona kimepoteza mwelekeo.
CHADEMA kinafanya mchezo na mapenzi ambayo watu wanayo kwake kiasi kwamba hakitaki kujirekebisha mapema. Haitoshi kufukuzana na kusimamishana. CHADEMA kinahitaji kujiangalia muundo wake, kanuni za uongozi wake na mwelekeo wake na kuona ni jinsi gani hivi vinachangia kuleta matatizo.
Bila kufanya hivyo kitaendelea kukumbwa na misukosuko na kitazidi kupoteza muda wa kujiandaa na badala yake kutafuta visingizio vingine vingi vyenye kuhusisha CCM.
Wakati umefika kwa Mwenyekiti Mbowe na viongozi wake kukaa chini na kujiuliza wanafanya kitu gani vibaya hadi kuleta matatizo ndani ya chama. Waache kuuliza CCM inafanya nini kuwavuruga kwani CCM haina jinsi isipokuwa kuwavuruga kwani kwa kufanya hivyo ndivyo kitakavyoweza kuendelea kukaa madarakani.
Si jukumu la CCM kuimarisha upinzani, ni jukumu la upinzani kuimarisha upinzani na kuidhoofisha CCM. Cha kushangaza baadhi ya wapinzani wenyewe ndio wanaipa nguvu CCM. Na hapa ndipo tatizo la CHADEMA lilipo na tutakaa kushuhudia ukifka 2014 wakishindwa kupata hata viti nusu ya serikali za mitaa na watakuja na kujipongeza kwa kupata majimbo 50 kwenye uchaguzi mkuu! Na wapo watu watashangilia!
source: Raia Mwema: Lula wa Ndali Mwananzela
No comments:
Post a Comment