WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, January 30, 2013

Kabange Twite atafuna bure mil. 56/- Yanga


NA MWANDISHI WETU

Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura

Baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza kukwama kwa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ya mchezaji Kabange Twite, imebainika kuwa Yanga wataingia gharama za bure za zaidi ya dola za Marekani 35,000 (Sh. milioni 56) katika kipindi cha kuanzia sasa hadi Juni wakati mchezaji huyo atakapokamilishiwa usajili wake, imeelezwa.

Aidha, imedaiwa kuwa mchezaji huyo ataikamua Yanga jumla ya dola za Marekani 80,000 (Sh. milioni 127) katika mkataba wake wa miaka miwili ulioanza mwezi uliopita na kwamba, gharama hizo ni mbali na nyumba, usafiri na matibabu katika kipindi chote ambacho Kabange atatumikia mkataba wake kwa ‘Wanajangwani’.  

Chanzo kutoka klabuni hapo kimedai kuwa fedha hizo ni sehemu ya gharama za uhamisho wake kutoka FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo Yanga walilipa dola za Marekani 20,000 (Sh. milioni 32) na mshahara wa kila mwezi wa dola za Marekani 2,500 ambao kwa miezi hiyo sita ya kukaa bure bila kucheza mechi rasmi za klabu hiyo (kuanzia Desemba 2012 hadi Mei mwaka huu), ni sawa na dola 15,000 (Sh. milioni 24).   
  
Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa Kabange, ambaye ni pacha wa Mbuyu Twite wa Yanga pia, hataichezea timu hiyo msimu huu baada ya klabu hiyo kuingiza taarifa zenye upungufu wakati ikimuombea ITC kwa njia ya mtandao (TMS). 

 “FIFA wamekataa kutoa ITC ya Kabange kwa sababu baadhi ya taarifa walizotuma Yanga zikiwamo za mkataba kati ya mchezaji (Kabange) na klabu hiyo na makubaliano ya mkataba wa Yanga na FC Lupopo ambayo ndiyo inayommiliki mchezaji huyo zilikuwa na kasoro,” alisema Wambura.

Akizungumza na NIPASHE kuhusiana na suala la Kabange, Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako, aliiambia NIPASHE kuwa wamestushwa na taarifa hizo na kwamba wataanza kukaa leo kujadili nini cha kufanya na kwamba, ni kweli wamekuwa wakiendelea kumlipa mchezaji huyo stahili zake zote kama walivyokubaliana. Hata hivyo, Mwalusako hakutaja kiasi wanachopmlipa Kabange. 

“Ni kweli tumepata taarifa za kukwama kwa ITC ya Kabange. Kamati zetu zitaanza kukaa kuanzia kesho (leo) tuangalie namna ya kufanya maana mchezaji tumeshamnunua na tunamlipa mshahara na mahitaji yake mengine,” alisema.

Juzi mchana, Mwalusako alishuhudiwa na mwandishi wa habari hii akikabidhi barua kwenye ofisi za TFF kuliomba shirikisho hilo liwasaidie kuomba ITC ya mchezaji wao.
Hata hivyo, Wambura aliliambia gazeti hili jana kuwa licha ya kupokea barua hiyo, hawana namna ya kuwasaidia kwa sababu dirisha la usajili limeshafungwa.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment