NA BEATRICE SHAYO
Hujuma zaidi zinaendelea kuigubika bandari ya Dar es Salaam, hali inayomfanya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe , kuipa siku mbili Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Bandari (TPA) kueleza sababu za kuondolewa kipengele muhimu kwenye mkataba wa ujenzi wa mtambo wa kupakua mafuta ya meli (SPM).
Alitoa amri hiyo jana alipozuri bandari hiyo akiongozana na Mawaziri Dk. William Mgimwa-Fedha , Dk Abdallah Kigoda- Viwanda na Biashara na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene.
Ilielezwa kuwa kuondolewa kipengele hicho kutailazimu TPA kugharamia Dola milioni 300 karibu sawa na Sh. bilioni 500 katika kipindi cha miaka miwili za kukarabati mtambo huo.
Wakati Dk. Mwakyembe akitoa agizo hilo, TPA ilieleza kuwa ili kuboresha huduma za bandari zote , Mamlaka hiyo inahitaji kupatiwa mkopo wa Dola bilioni nne.
Baada ya taarifa hiyo Waziri huyo alimbana Kaimu Mkurugenzi wa TPA, Madeni Kipande, akihoji kuwa wakati Mamlaka hiyo inakabidhiwa SPM, mzabuni aliyeujenga mtambo huo kampuni ya Leighton ya Singapore alionyesha kuwa kipengele muhimu kimeondolewa katika mkataba huo.
Waziri Mwakyembe alieleza zaidi kuwa awali mkabata huo ulimtaka mzabuni huyo anapokamilisha kazi yake alitakiwa kuacha vifaa vya ukarabati wa mtambo huo vyenye thamani ya Dola milioni 300 (bilioni 500).
“Nashangaa kampuni hii haikuacha vifaa hivyo kwanini na vifaa hivyo vingetumika kukarabati kwa muda wa miaka miwili na pia tusingeingia gharama zozote sasa tunataka kujua aliyekichomoa kipengele hiki ni nani ili na sisi tumchomoe.” Alisema Dk Mwakyembe.
Baada ya Dk Mwakyembe kuzungumza hayo, Simbachawene alihoji tena kwa Kaimu Mkurugenzi ni kwanini mkataba ubadilishwe wakati kipengele cha mkataba huo kilikuwa ni muhimu kwa mwekezaji huyo kupatiwa zabuni ya ujenzi wa mtambo huo? “Hivi hapa TPA si kuna wanasheria, iweje litokee hili jambo”. alihoji Simbachawene
Kipande akijibu hoja hiyo alisema baada ya zabuni kupita kipengele hicho kiliondolewa na kuifanya TPA kuingia gharama za kufanya matengenezo. Baada ya maelezo hayo , Dk. Mgimwa aliongeza kuwa serikali inahitaji kumfahamu aliyekiondoa kipengele hicho kwani jambo hilo linaonyesha TPA kuhujumiwa.
Aliitaka bodi ya TPA kueleza ilichukua hatua gani.
Baada ya malumbana hayo Dk. Mwakyembe aliitaka Bodi na Menejimenti ya TPA kufanya kikao cha Jumatatu ijayo na siku hiyo kumpekea maelezo ofisini kwake.
Alisema taarifa hiyo ataipeleka kwa mawaziri aliokuwa ameongoza nao ili kutoa kauli ya pamoja.
Mbali na hilo Dk Mwakyembe pia alisema kuanzia sasa kampuni za kigeni na za ndani hazitapewa vibali vya kujenga bandari kavu za kuhifadhi shehena karibu na eneo la bandari kwani hazipunguzi mrundikano wa mizigo bandarini.
Katika hatua nyingine Dk Kigoda aliliagiza Shirika la Viwango (TBS) kufanya kazi kwa saa 24 bandarini humo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment