Waumini wa dini ya Kiislam wa manispaa ya Mtwara, wakikusanyika katika viwanja vya Mashujaa jana kwa ajili ya kufanya dua ya kuombea gesi isisafirishwe kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam. Waumini hao wameitaka serikali kubadilisha msimamo wake wa sasa na badala yake kupeleka vinu vya kufua umeme wa gesi mjini Mtwara ili wakazi wake wanufaike kwa kupata ajira.
Maelfu ya shura ya maimamu yameunga na wananchi wa mikoa ya Kusini, kuitaka Serikali isitishe mpango wa kusafirisha gesi asilia kwenda Dar es Salaam.
Aidha, wametaka uwekwe mtambo wa kufua umeme uliokusudiwa hapo awali mkoani hapo.
Akisoma tamko kwenye hadhara ya waumini wa Kiislam mjini hapa, Ustadhi Mohamed Salim, alisema kwa kuwa wanaamini serikali yao ni sikivu basi isitishe zoezi zima la ujenzi wa bomba mpaka pale suluhisho la tatizo hilo litakapopatikana baina ya wananchi na viongozi.
Tamko hilo lilotolewa lilitolewa jana na Shura ya Maimam katika kongamano la dini ya waumi wa Kiislamu lililofanyika katika uwanja wa Mashujaa mjini hapa.
Aidha Ustadhi Salim amesema kuwa kumekuwepo na majibu ya kutoridhisha na ya kuwakashifu wananchi wa Mtwara kutoka kwa Mkuu wa Mkoa, Waziri wa Madini na Rais mwenyewe, ambayo yanajaribu kueleza vitu vingine na si hoja yenyewe ya wananchi wa Mtwara.
“Majibu yanayotolewa na viongozi hao yanaonyesha na yanajikita katika kuelekea upingaji wa kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar lakini sababu ya kukataa gesi isitoke si hivyo…,” alisema.
Alisema serikali haina budi kubadilika kimawazo na kuona kuwa mikoa ya kusini ina haki ya kuendelezwa kiuchumi na kuachana na kasumba ya kila kitu kupelekwa Dar es Salaam.
“Ifike wakati sasa wa kuendeleza mikoani … mikoa mingine ili mrundikano wa watu uliopo Dar upungue…na usawa wa maendeleo kati ya mikoa mbalimbali iliyopo hapa Tanzania.
Alisema katika historia mkoa wa Mtwara umetengwa kwa muda mrefu tangu enzi ukoloni.
Akitoa mfano Imamu huyo alisema Mtwara ilikuwa na reli ikaondolewa, bandari kwa sasa haitumiki, taa kubwa za uwanja wa ndege zilizoondolewa na kupelekwa Arusha.
Alisema leo gesi imegundulika wanataka kuiondoa na kuifanya Mtwara ibaki kuwa maskini.
Katika tamko lao hilo walisema wamechoshwa na hali hiyo na wako tayari kufa kwa ajili ya gesi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment