NA WAANDISHI WETU
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amepigilia msumari kwa nafasi ya urais kwa kupendekeza kuwa Katiba Mpya isiruhusu mtu yeyote mwenye historia ya kujilimbikizia mali kugombea urais kwa kuwa hana sifa.
Wakati Waziri Sitta akitoa pendekezo hilo na mengine, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (Zatuc) nalo limependekeza Katiba Mpya isimruhusu kugombea tena mgombea urais anayeshindwa katika Uchaguzi Mkuu.
Waziri Sitta alitoa pendekezo hilo, ikiwa ni sehemu ya maoni yake kuhusu uundwaji wa Katiba Mpya, aliyoyatoa alipokutana na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, jijini Dar es Salaam jana.
Alisema ibara ya 39 ya katiba ya sasa imeeleza sifa zinazomwezesha mtu kugombea urais wakati wa Uchaguzi Mkuu, lakini sifa kuu ya uadilifu haijawekwa kwa mgombea mhusika.
Kwa hali hiyo, alisema iwapo mgombea huyo atabainika ana historia ya kujilimbikizia mali, basi hatakuwa na sifa ya kugombea nafasi hiyo.
Alisema ili kuweza kumtambua mgombea huyo iwapo ana historia ya kujilimbikizia mali au la, anapaswa kuhojiwa hadharani kwa kutumia sheria ya ‘public enquires’ (mahojiano ya ana kwa ana) kuanzia kwa watoto.
“Katiba izungumzie kipengele cha uadilifu kama sifa kuu ya msingi kwa mtu anayetaka kugombea kiti cha urais. Ibara ya 39 ya katiba ya sasa inataja vigezo vya kuwa na elimu, uraia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano na umri, lakini kipengele kikuu cha muhimu cha uadilifu hakipo,” alisema na kuongeza:
“Viongozi wasio waadilifu huwachagua vibaraka wao. Katiba mpya ionyeshe kipengele cha weledi, uadilifu na utendaji kazi bora kama kigezo na sifa muhinu kwa mgombea wa nafasi ya urais. Ukitaka nchi isambaratike iongozwe na watu wanaojilimbikizia mali. Waafrika wengi wanaingiwa na ghadhabu ni kutokana na kutotendewa haki.”
Ibara ya 39 kuhusu sifa za msingi anazostahili kuwa nazo mgombea wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano, inasema: “Mtu hastahili kushika kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano isipokuwa tu kama-rais wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa sheria ya uraia..ametimiza umri wa miaka arobaini, ni mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa…”
MUUNGANO
Kuhusu Muungano, Sitta alipendekeza wa sasa uendelee, huku akipinga kuwapo kwa serikali tatu kwa madai kwamba itavunja umoja kwa kuwa kila serikali itakuwa inaangalia mambo yake yenyewe.
Pia alisema kilichomo kwenye katiba ya sasa kuhusu haki kinafanya kundi lingine la watu hasa wananchi walio wanyonge wasitendewe haki kwa vile inawalinda wenye mali.
Alisema katiba ya sasa ina ibara zinazozungumzia haki, lakini ya mtu mmoja mmoja na si wengi.
Waziri Sitta alisema kutokana na upungufu huo, falsafa ya katiba ya sasa inaonyesha mwenye mali ndiye anayetetewa sana kuliko mnyonge.
Alisema hali hiyo inatokana na katiba hiyo kuonyesha mtu mmoja analindwa sana kutokana na kuingiza falsafa za nchi za Magharibi.
Alipendekeza haki za wengi zipewe kipaumbele kwenye katiba mpya kwa kuweka kifungu cha sheria kinachomlinda na kumtetea mwananchi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment