WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, September 4, 2014

Taarifa ya Wawakilishi wa Dini


TAARIFA YA WAWAKILISHI WA TAASISI ZA DINI WA BUNGE MAALUM LA KATIBA TOKA WAJUMBE 201 KUHUSU MWENENDO WA SHUGHULI ZA BUNGE MAALUM LA KATIBA

Sisi Wawakilishi wa Jumuiya na Taasisi za Dini, tuliopendekezwa na Taasisi zetu na baadaye kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kushauriana na Rais wa Zanzibar kuwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, na kula kiapo cha utekelezaji wa jukumu hili kubwa.

Tukiamini kuandaa Katiba Mpya kwa maridhiano ya Kitaifa kwa wananchi wote, tulipokea jukumu hili kama wajibu wetu Kitaifa.  Aidha tunaamini kwamba katika kupata maridhiano ya Kitaifa ni muhimu kuheshimu kila wazo na fikra inayotolewa na kuunganisha fikra hizo kwa usahihi, kwa njia ya kidemokrasia kwa kupiga kura na kukubaliana na matokeo ya wengi.

Kama ilivyoelezwa hapo awali, kabla ya kuanza shughuli za Bunge Maalum, kila mjumbe alikula kiapo cha kuwa mwaminifu na mtiifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa kadiri ya uwezo wake na ufahamu wake, kufanya kazi zinazomhusu, bila upendeleo na kumuomba Mwenyezi Mungu amsaidie. 

Tumeshangazwa na kusikitishwa sana kuona kwamba mchakato wa kutayarisha Katiba itakayopendekezwa na Bunge hili kwa wananchi, unachafuliwa taswira yake.  Bunge Maalum la Katiba linachafuliwa na, shughuli zake kuingiliwa na kupotoshwa na wajumbe wenzetu walio nje ya Bunge, Makundi, Taasisi na Vyombo mbali mbali vya habari, uhalali na ukweli wa shughuli za BungeMaalum la Katiba unapotoshwa.  Wananchi wanaaminishwa yasiyo na ukweli.

Upotoshwaji huu umezua mijadala mbali mbali katika jamii ya Watanzania na bado linaendelezwa kama ifuatavyo:

1.  Kwamba Bunge Maalum la Katiba halina uhalali kwa kuwa hao wajumbe wenzetu walioondoka wameliondolea uhalali wake kwa vile hwapo, wakiwepo Bungeni basi uhalalai wake utakuwepo - utapatikana;
2.  Inadaiwa kwamba Kanuni za Bunge Maalum la Katiba zinavunjwa ovyo ovyo;
3.  Inadaiwa pia, kwamba kinachojadiliwa sasa katika Bunge hili ni Waraka mwingine na si Rasimu iliyotayarishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyowasilishwa rasmi Bungeni na kuanza kujadiliwa na wajumbe;
4.  Inadaiwana watu na Taasisi mbali mbali, kwamba viongozi wa dini, wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, na wajumbe wa Kundi la 201, wanapewa rushwa. Isitoshe Vyombo vya habari vimeandika tuhuma kama hizi.
5.  Inadaiwa pia kwamba wajumbe waliomo katika Bunge hili ni wachache, ukilinganisha na hao walioko nje ya Bunge hilo;
6.  Bunge hili,kwatuhuma hizo, lazima lisitishwe au livunjwe na Mhe. Rais.

Kabla ya kuanza kuusahihisha upotoshwaji huo, sisi Wawakilishi wa Taasisi za Dini mbali mbali na Wajumbe wa Kundi la 201 katika Bunge Maalum la Katiba, tunapenda kufahamisha umma wa Tanzania mchakato wa kutayarisha Katiba Mpya ulivyo kisheria.

Tunapenda kuwafahamishaWatanzania wenzetu kwamba mchakato huu una hatua tatukwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.  Mpaka hivi sasa nihatua moja imekamilika.  Hatua ya pili ndiyo inayoendelea,na hatua ya tatu bado haijaanza.

Hatua ya kwanza ni ile ya uandaaji wa Rasimu. Sheriaya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 iliunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya kifungu cha tano cha sheria hiyo.  Tume hii ilipewa jukumu la kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi juu ya Katiba, kuanisha na kuchambua maoni ya wananchi na kisha kuandaa rasimu ya Katiba.  Kazi hiyo ilifanyika kwa kipindi cha takriban miaka miwili na hatimaye Rasimu ya Katiba ilikamilika.

Hatua ya pili ilikuwa ni kuipeleka Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalum la Katiba, ambalo liliundwa kwa shughuli maalum ya kuandika Katiba inayopendekezwa, ili ifikishwe kwa wananchi ambao wataamua waikubali au waikatae kwa kuwa wao ndio wenye maamuzi ya mwisho.  Hawa ni Watanzania wote wenye uwezo wa kupiga kura kwa kutoa maoni yao.  Hoja ya Mamlaka ya Bunge hili hatujazungumzia kwa vile imefikishwa Mahakama Kuu ya Tanzania ili kupata tafsiri sahihi ya mamlaka ya Bunge hili.  Tunachoweza kusema ni kwamba jukumu kuu la Bunge hili ni kutengeneza Katiba inayopendekezwa na Bunge ili ifikishwe kwa wananchi  waipigie kura ya maoni.  Hatua hii ya pili bado inaendelea.

Hatua ya tatu ni pale Bunge Maalum la Katiba tutamkabidhi Mhe. Rais Katiba inayopendekezwa ambayo itafikishwa kwa wananchi ili waikubali kama wataridhika nayo au kuikataa kama haikidhi matarajio yao.


Hatua hii ni ya mwishowananchi wakiikubali tunapata Katiba Mpya wakiikataa, tunaendelea na Katiba tuliyonayo.

Kilichotokea ni kwamba, wajumbe wenzetu walio nje ya Bunge hili wameamua kuukiuka utaratibu uliowekwa kisheria.  Badala yake wamepeleka Rasimu ya Katiba kwa wananchi wakati mchakato wa kutayarisha Katiba inayopendekezwa bado haujakamilika.

Sisi Wawakilishi wa Taasisi za Dini, ambao kuuhubiri, kuutangaza na kuusimamia ukweli ni moja ya majukumu yetu katika jamii, tumesikitishwa sana na taarifa potofu zinazosambazwa kwa makusudi na makundi, taasisi na vyombo vya habari mbali mbali na tukiwa wajumbe wa Bunge hili ambao tunafahamu kwa kina na tunaridhika na kila hatua ya mchakato huu.  Tuna wajibu wakusahihisha upotofu huu, unaoendeshwa kwa makusudi na hivi kuwaeleza Watanzania ukweli na hali halisi inayojiri hapa Bungeni.  Watanzania msifadhaishwe na wala msibabaishwe.  Hali ni shwari.  Mchakato unaendelea kwa amani na utulivu.

Katika kusahihisha upotofu unaozungumzwa kupitia mijadala na midahalo mbali mbali katika jamii, tunaomba kufafanua hali ilivyo kama ifuatavyo:-

TUHUMA KWAMBA BUNGE MAALUM LA KATIBA KUKOSA UHALALI
Jambo hili si kweli hata kidogo kwani kuna wajumbe wa aina tatu Bungeni ambao wamewekwa na kutambuliwa kisheria.  Hawa ni kama wafuatao:
1.  Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
2.  Wajumbewa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
3.  Wajumbe 201 walioteuliwa na Mhe. Rais, baada ya kupendekezwa na Taasisi, Mashirika na makundi mbali mbali nchini,

Uhalali waBunge unakuwapo wakati wajumbe kutoka makundi hayo matatu wapo Bungeni, na si Vyama vya Siasa pekee.  Iwapo kwa mfano wajumbe wa 201 wakiamua kutoshiriki katika shughuli za Bunge, basi sehemu moja muhimu ya Bunge haitakuwapo na uhalali wa Bunge hautakuwepo.

Hata hivyo, Kanuni za Bunge Maalum la Katiba zimeweka idadi ya akidi ambayo ni nusu ya wajumbe wote wa Bunge Maalum.  Akidi hii ikifikiwa Bunge huendelea na shughuli zake.  Akidi hii hufikiwa kila wakati BungeMaalum linapokutana.  Hii inamaanisha kwamba Bunge Maalum la Katiba linaendesha shughuli zake kwa misingi ya sheria na taratibu zilizojiwekea.  Bunge lina uhalali wa kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria.

TUHUMA KWAMBA KANUNI ZA BUNGE MAALUM LA KATIBA ZINAVUNJWA
Suala hilo halijawahi kutokea.  Kanuni za Bunge Maalum la Katiba zilipitishwa nawajumbe wote kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sheria Namba 83.  Vile vile uendeshaji wote wa shughuli za Bunge zinafanywa kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Maalum.  Kanuni hizo zinatoa fursa ya Bunge Maalum kuzirekebisha pindi inapobainika ipo haja ya kufanya hivyo kwa mujibu wa kanuni Namba 87.

WARAKA MWINGINE UNAJADILIWA NA SI RASIMU YA TUME
Hili nalo si kweli.  Tunawahakikishia Watanzania wote kwamba sisi kama Wawakilishi wa Taasisi za Dini miongoni mwa wajumbe wa Kundi la 201, kwa ujumla tunasema hii si kweli.Ni upotoshaji wa makusudi.  Tunaijadili Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ibara kwa ibara.  Ibara nyingi zimeachwa kama zilivyo.  Kuna ibara ambazo zimeboreshwa au kurekebishwa, kuna ambazo zimeondolewa na kuna nyingine mpya ambazo zimewekwa ili kuweka mambo ya msingi ambayo Rasimu haikuyazingatia au haikuyaona.

WAWAKILISHI WA TAASISI ZA DINI, WAJUMBE WA KUNDI LA 201 WA BUNGE LA KATIBA KUPEWA AU KUPOKEA RUSHWA
Sisi Wawakilishi wa Taasisi za Dini na Wajumbe wa Kundi la 201 wa Bunge hili tumesikitishwa sana na taarifa hii iliyosambazwa na baadhi ya watu, na kukaririwa na baadhi ya vyombo vya habari aidha kupitia kwenye mijadala, midahalo na makongamano  mbali mbali.  Baadhi yetu sisi Viongozi waKiroho tumeapishwa viapo vya uadilifu katika uongozi wetu wa kiroho na tuko mstari wa mbele kuongoza waumini wetu kuepuka dhambi ya tamaa ya fedha, na kusema uongo.  Taarifa kama hizo hazionyeshi heshima kwa dini au nafasi zetu za kipekee katika uongozi wa kiroho.  Taarifa hizi zinatangazwa kwa makusudi na watu mbali mbali  kupita vyombo vya habari kwa malengo ya kisiasa na kutudhalilisha sisi Viongozi wa kiroho mbele ya umma.  Tunaomba tabia hii ikomeshwe.

TUHUMA KWAMBA BUNGE KUWA NA WAJUMBE WACHACHE
Hili nalo si kweli.  Wajumbe wanaohudhuria Bunge wanakidhi akidi inayohitajika kwa mujibu wa kanuni.

HOJA YA KUSITISHWA AU KUVUNJWA KWA BUNGE MAALUM
Hii ni hoja inayozungumzwa katika mijadala mbali mbali katika jamii.  Msingi wa hoja hiyo ni kutokuueleza umma ukweli ulioko Bungeni kwa kupeleka taarifa potofu kwa wananchi kwamba Bunge Maalum limekosa mwelekeo.  Hatuoni sababu za hoja hii kutiliwa maananikwa kuwa hakuna sababu za msingi na za kisheria za kufanya hivyo. 

HITIMISHO
Kumekuwa na taarifa mbali mbali zenye malengo ya ama kuingilia shughuli za Bunge hili au kutudhalilisha sisi wajumbe ambao si Wabunge au Wawakilishi.  Wajumbe201, ambao mchango wao katika mijadala ya Kamati mbali mbali umekuwa na uzito wa pekee, hautambuliki katika taarifa hizo ambazo zimejaa malengo ya kisiasa zaidi kuliko ukamilishaji wa shughuli za Bunge Maalum.

Kuna taarifa nyingine zimesambazwa zikiwa na upotoshaji mkubwa, licha ya kwamba Taasisi zinazosambaza taarifa hizo zina wajumbe wake katika Bunge Maalum.  Wajumbe hao wangeweza kuzielimisha Taasisi zao ukweli ulipo hapa Bungeni, na hivyo kuwafikishia wasomaji wao taarifa zilizo za kweli na ili kulijengea Bunge hili heshima machoni pa umma wa Tanzania na Kimataifa.  Udhalilishaji kama huu unatuumiza hata sisi wajumbe ambao kwa hiari yetu tuliamua kubaki Bungeni na kuyatimiza hayo ambayo tulitumwa tuje tuyakamilishe.

Kama tulivyosema hapo awali ni wajibu wetu kama Viongozi wa Dini na Wajumbe wa Bunge hili kuutaarifu umma hali halisi katika shughuli za Bunge Maalum na kuwasihi wapotoshaji kwamba wauheshimu ukweli na wawaheshimu watanzania kwa kuwaeleza ukweli.

Ahsanteni sana.



…………………….                              …………………………
SHEIKH HAMID MASOUD JONGO      ASKOFU AMOS JOSEPH MUHAGACHI
BAKWATA                                        KIKRISTO




                                      TAREHE 3 SEPTEMBA, 2014

No comments:

Post a Comment