WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, September 5, 2014

JK ataka maombi kunusuru Katiba

NA WAANDISHI WETU

5th September 2014

Rais Jakaya Kikwete

Rais Jakaya Kikwete amewaomba Watanzania kuombea mazungumzo kati yake na vyama vikiwamo vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) yanayotarajiwa kufanyika tena Septemba 8, mwaka huu ili kuunusuru mchakato wa katiba mpya.

Amesema maombi hayo yatasaidia mazungmzo hayo kwenda vizuri na kuondoka walipo na kufikia hatua nzuri ya kupatikana kwa katiba mpya.

Rais Kikwete alisema katika mkutano uliopita kati yake na vyama hivyo vilivyojumuisha viongozi wa vyama vyenye wawakilishi bungeni, walikuwa na mazungumzo mazuri ya mashauriano na walipeana majukumu muhimu ya kufanya, na ambayo wanatarajia kuyawasilisha katika kikao hicho.

“Katika mkutano uliopita, ambao nilihudhuria kwa kualikwa na Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), tulipeana majukumu muhimu ya kufanya... ambayo tunatarajia kuyawasilisha katika kikao kingine cha maridhiano,” alisema Rais Kikwete.

Aliongeza: “Sipendi kuzungumza mambo mengi katika hili, lakini ninaomba Watanzania waombee mazungumzo haya ili tuweze kuondoka hapa tulipo katika mchakato huu wa katiba na hatimaye tufikie katika hatua nzuri ya kupata katiba.”

Mchakato huo uliofikia hatua ya Bunge Maalumu, upo njiapanda baada ya wajumbe wa Ukawa kususia kwa madai kuwa kinachojadiliwa ni tofauti na kilichomo katika rasimu ya katiba iliyowasilishwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Ukawa huundwa na wajumbe watokao katika vyama vikuu vya upinzani nchini vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi.

Baada ya Ukawa kususia Bunge hilo, kumekuwa na hisia tofauti miongoni mwa jamii na makundi mbalimbali ya kijamii, huku baadhi wakimtaka Rais Kikwete kulisitisha na wengine wakiwasihi Ukawa kurejea bungeni kuungana na wenzao kutengeneza katiba mpya.

Msimamo wa Ukawa ulikuwa ni kukutana na Rais Kikwete ili kuzungumzia suala hilo na kwamba, hawatarejea bungeni hadi hapo watakapohakikishiwa kuwa itakayojadiliwa katika Bunge hilo ni rasimu iliyowasilishwa na Tume hiyo, ikiwa ni pamoja na kuzingatia maoni ya wananchi yaliyotaka muundo wa Muungano wa serikali tatu.

Rais Kikwete alikutana na viongozi wakuu wa vyama vya siasa Ikulu ndogo, mkoani Dodomaa Agosti 31, mwaka huu.

Baadhi ya viongozi wa Ukawa waliohudhuria kikao hicho, ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu.

Mbali na viongozi hao, viongozi wengine wa vyama waliokuwapo, ni Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo, Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema, Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa.

Viongozi hao wa vyama walikutana na Rais Kikwete kwa takriban saa tatu, kuanzia saa 6: 20 mchana na baada ya kikao hicho kumalizika, waliondoka Ikulu na kufanya kikao chao cha faragha kwa muda wa saa moja.

Mwenyekiti wa TCD, Cheyo alisema mazungumzo yao na Rais Kikwete yalikuwa mazuri na kwamba, walizungumzia ajenda kuu mbili, moja ilihusu mchakato wa katiba mpya na nyingine ilihusu uchaguzi mkuu ujao mwakani.

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete jana aliendelea kuwatia moyo Watanzania katika sekta ya elimu nchini, kwa kusema kuwa jitihada zinaendelea kufanywa ili kuiboresha ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa maabara katika shule za sekondari ifikapo Novemba, mwaka huu.

Kutokana na hilo, aliwaagiza watendaji wa serikali katika sekta hiyo kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa miundombinu hiyo ya maabara ifikapo muda huo kama alivyoagiza kwani vinginevyo hatawaelewa.

“Ukifika muda huo, mimi sitataka kupewa sababu za wa nini sijakamilisha,” alisisitiza.Rais Kikwete alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wazee wa Dodoma katika ukumbi wa Chuo cha Mipango mjini humo.

Pia alisikitishwa na kuona idadi kubwa ya wasichana wadogo katika mkoa huo wakiwa wajawazito na wenye watoto akisema kuwa ndiyo matokeo ya wengi kutomaliza masomo yao ya elimu ya msingi na sekondari.

Kadhalika, alisikitishwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaonza elimu ya msingi kutoweza kuhitimu masomo yao.Alisema kati ya wanafunzi 54, 301 waliojiandikisha kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka 2007, waliofanikiwa kufanya mtihani huo walikuwa 39, 387 na hivyo wanafunzi 14, 914 wakikosa kumaliza elimu ya msingi mwaka huo mkoani humo.

Alizitaka shule za mkoa huo na nchini kote kwa ujumla kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula cha mchana shuleni, kwani kazi hiyo haikuwa ya Shirika la Chakula Duniani (WFP).

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, mbali na WFP kuacha kutoa huduma ya uji pekee shuleni, shule zote zinatakiwa kutoa chakula cha mchana, kwani shirika hilo lilikuwa linaonyesha mfano.

“WFP walikuwa wanaonyesha mfano, siyo kwamba wakiondoka wale basi na sisi tunaacha. Je, tunashindwa kweli kuchangia debe la unga kwa ajili ya wanafunzi wetu? Haiwezekani,” alisema Rais Kikwete.

Alisema utaratibu wa kutoa chakula shuleni utaongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.Alisema pia serikali itahakikisha kuwa ifikapo mwaka 2016 kila mwanafunzi awe na kitabu chake, huku Sh. milioni 500 zikitarajiwa kupelekwa kwa kila halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu.

Kuhusu umeme, alisema serikali imejiwekea malengo ya kuhakikisha kwamba, ifikapo mwaka 2015, asilimia 30 ya Watanzania wote wanafikiwa na huduma hiyo na kwamba, hadi sasa imeshafanikiwa kuwaunganishia wananchi kwa asilimia 36 na hivyo kuvuka malengo.

Alisema serikali katika kufanikisha hilo, imeshatenga Sh. bilioni 44 kwa ajili ya kupeleka nishati hiyo katika vijiji 1993 vya mkoa wa Dodoma.

Kuhusu huduma ya maji, Rais Kikwete alisema serikali imejipanga vya kutosha kuhakikisha kwamba, ifikapo mwaka 2025 hakuna mwananchi atakayetembea umbali wa mita 400 asipate maji.

Alisema hadi sasa wakazi wa mijini wanapata huduma hiyo kwa asilimia 60 na asilimia 65 kwa wale wa vijijini.Alishangazwa na jinsi wakulima katika Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma, ikiwa ni pamoja na wale wa Kijiji cha Kibaigwa jinsi, ambavyo wanalanguliwa mazao yao na walanguzi na hivyo kutonufaika na jasho lao.

Hata hivyo, alisema alishazungumza na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, kukabiliana na hilo. 
Alishtushwa na wakulima wa eneo hilo la Kibaigwa kutokana na migogoro kati yao na wafugaji, kwani akiwa ziarani katika eneo hilo, alikuwa anaonyeshwa jinsi watu walivyochomewa mashamba na kuharibiwa zana zao za kilimo za kisasa.

Alitaka mikoa mbalimbali nchini kuwa na mipango ya matumizi ya ardhi ili kuepusha migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Pia alizitaka mamlaka zitambue uwezo wa ardhi wa kubeba kiasi cha mifugo na pia kuwapo kwa usimamizi wa dhati ili kuhakikisha mipango iliyowekwa inatekelezwa ili kuepusha migogoro kati ya wanaofuga na wale wasiofuga.

“Lazima patengenezwe utaratibu mzuri wa mahali pa kuishi na siyo popote…hivi ni kweli unaweza kusema naweza kuweka mifugo yangu eneo la Oysterbay, lakini kama utaratibu uliowekwa na kwa makubaliano haufuatwi, watu wataendelea na migogoro na kuuana,” alisema Rais Kikwete.
Aliupongeza Mkoa wa Dodoma kwa kupungua kwa maambukizi ya Ukimwi kutoka asilimia 3.9 mwaka 2008 hadi asilimia 2.9 sasa.

Pia aliupongeza mkoa wa Morogoro kwa kuweka utaratibu wa kuwa na vituo vya kusubiria kinamama wajawazito kujifungulia na hivyo kupunguza idadi kubwa ya vifo wakati wa kujifungua.

Kuhusu ugonjwa Ebola, ambao unaweza kusambazwa na popo, wanyama aina ya nyani, sokwe na swala, alisema bado ni tishio, kwani hauna kinga wala dawa ya kurefusha maisha.

Hata hivyo, alisema hadi sasa hakuna Mtanzania aliyeripotiwa kuwa na ugonjwa huo mbali na wanne kuhisiwa kuwa nao.

Alisema serikali imejipanga vya kutosha kukabiliana na janga hilo, ikiwa ni pamoja na kuunda kikosi kazi kinachoongozwa na Dk. Donan Mmbando, huku Sh. milioni 500 zikiwa zimeshatengwa dhidi ya hilo.

Rais Kikwete alisema timu za maafa za mikoa zimeshaandaliwa, vifaa 12, 750 vya kujikinga vimeshasambazwa katika wilaya na kanda 37 nchini.
Alisema pia kumetengwa vituo maalumu kwa ajili ya watakaobainika kuwa na dalili za ugonjwa huo ikiwamo Hospitali ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Pia kufungwa kwa mitambo maalumu katika viwanja vya ndege kupima joto na dalili za ugonjwa huo.Maeneo hayo ni pamoja na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Juliusi Nyerere (JNIA),  Mwanza, Namanga na kwamba tayari watumishi 100 tayari wameshapewa mafunzo dhidi ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Alisema pia serikali imeshapeleka  watumishi watatu nchini Kongo kujifunza zaidi.Alisema pia serikali itaboresha  maabara za nchini ikiwano ya NIMR  na kwamba tayari mwongozo umeshatolewa kiloa mkoa.

Hadi jana mashirika ya habari ya kimataifa yaliliripoti kuwa takribani watu 1900 tayari wameshafariki kutokana na Ebola katika baadhi ya nchi za Afrika Magharibi.

Imeandikwa na Augusta Njoji (Dodoma na Isaya Kisimbilu na Elizabeth Zaya (Dar).
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment