WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, August 15, 2014

Ya Katiba na kisa cha mtego wa panya


Profesa Seithy Chachage anasema;

“ Haitoshi  kabisa kulifahamu jambo. Kuambiwa ni habari tu, unaambiwa na unafahamu, unajua kwamba tukio fulani limetokea. Gumu zaidi ni kuelewa mantiki ya hilo jambo, na hata baada ya kufikiria na kulifahamu, ugumu mwingine huja pale ambapo inabidi ulieleze lieleweke na maelezo yakajitosheleza yenyewe na kumfanya kila asikilizaye kuridhika kwamba jambo linaeleweka.

Haitoshi wewe kulielewa, bali na wewe kulielezea na mtu mwingine akaelewa. Hapa umuhimu wa kufikiria unachukua nafasi ya pekee. Hii ndiyo maana ya mawasilino.” – Profesa Chachage Seithy Chachage ( Makuadi Wa Soko Hurua, ukurasa 117)

 Naam, mengine tuandikayo tulishayaandika zamani. Tunayarudia maana yanayotokea sasa ishara zake tulishaziona, isipokuwa, tu mahodari sana wa kupuuzia.

Haya ya UKAWA na CCM kuna ambao tunaweza kuyapuuzia leo tukidhani hayatuhusu, kumbe, yatatudhuru sote. Ya UKAWA na CCM ni mgogoro wa kisiasa. Ni sharti umalizwe kwenye meza ya mazungumzo.

Unahusu Katiba mpya, na ni busara na hekima, kuwa Katiba hiyo ipatikane kwa pande zinazohusika, kuanza na mazungumzo ya kindugu na kufikia maridhiano yatakayozaa Katiba ya Maridhiano.

 Maana, kwetu wanadamu, mengi yanayotufanya tufarakane na hata kugombana yanatokana na sisi wenyewe wanadamu. Na ndivyo ilivyo hata kwa ndege na wanyama.

 Ukiwaona ndege wanagombana, ukiwaona kuku wanagombana, na hata ng’ombe, basi, sababu kubwa ni ya viumbe hao wenyewe. Na mara nyingi, kugombana huku hutokana na kugombania kisichotosha.

 Hivyo basi, suluhu ya yale tunayogombania kama wanadamu yapaswa itokane na sisi wanadamu wenyewe. Na tangu karne ya 17 kuna wanadamu walioliona hili.

 Mwanafalsafa Thomas Hobbes alibainisha, kuwa migogoro mingi miongoni mwetu hutokana na ushindani wa kugombania kisichotosha. Kwa vile sote tuna mahitaji yenye kufanana, basi, Thomas Hobbes anasema, kuwa migogoro hii itaendelea, kugombania kisichotosha.

 Na Hobbes huyu anaamini, kutokana na hatari hii, basi, jukumu muhimu na kubwa kwa Serikali yeyote ile iwe ni kulinda amani ya nchi. Kwamba kwa kutofanya hivyo, jamii itarudi katika hali ya kutokuwa na taratibu; vurugu, kuuana, umasikini na kupelekea maisha mafupi.

 Hata hivyo, tunaamini pia, kuwa siku zote, pasipo haki na usawa hakuna amani, ingawa, katika jamii yeyote ile, uwepo wa amani na utulivu ni msingi mzuri katika kutafuta haki na usawa, kwa njia ya majadiliano.

 

Nimepata kusimulia kisa cha mtego wa panya uliosababisha madhara hata kwa wasio panya.

 Panya kwenye nyumba aliubaini mtego wa panya uliowekwa na mwenye nyumba uvunguni mwa kitanda. Panya yule akamwendea jogoo wa mwenye nyumba. Akamwambia:

 “Ewe jogoo, kuna mtego umewekwa uvunguni mwa kitanda. Tusaidiane namna ya kuutegua kabla haujatudhuru wote."

 Jogoo akajibu: "Ondoka zako, mie mtego wa panya unanihusu nini wakati sina kawaida ya kufika uvunguni mwa kitanda?"

  Panya yule akaenda hadi kwa mbuzi wa mwenye nyumba. Akamwambia:

 "Ewe mbuzi mwema, unajua kuna mtego wa panya uvunguni mwa kitanda cha mwenye nyumba. Tusaidiane mawazo ya kuutegua kabla haujatudhuru sote."

Mbuzi akajibu: "Hivi tangu lini ukaniona nikiingia chumbani kwa mwenye nyumba? Mtego huo wa panya haunihusu mie mbuzi."

Panya akaenda hadi kwa ng'ombe wa mwenye nyumba. Akamwambia: "Ewe ng'ombe wa Bwana, kuna mtego wa panya umewekwa uvunguni mwa kitanda. Tusaidiane mawazo namna ya kuutegua kabla haujatuletea madhara."

 Ng'ombe akajibu akionyesha mshangao! ;"Sijapata kusikia jambo la ajabu kama hilo. Yaani, mie ng'ombe nidhurike na mtego wa panya ulio uvunguni mwa kitanda! Hilo halinihusu."

 Basi, ikatokea siku moja, nyoka akaingia chumbani kwa mwenye nyumba. Katika kutambaa kwake uvunguni mwa kitanda, mkia wa nyoka ukanasa mtegoni. Kishindo kilisikika. Mwenye nyumba alikwenda kwa furaha akiamini hatimaye panya aliyekuwa akimsumbua sasa amenaswa. Hapana, ni nyoka aliyenaswa mkia. Na ni mwenye hasira pia. Akamng'ata mguu. Sumu kali akamwachia. Mwenye nyumba akafa.

 Jirani wakafika msibani. Siku ya kwanza watu walikuwa wachache. Wakahitaji kitoweo. Akakamatwa jogoo wa mwenye nyumba. Jogoo akachinjwa. Siku ya pili watu wakaongezeka. Kilihitajika kitoweo pia. Akakamatwa mbuzi wa mwenye nyumba. Mbuzi akachinjwa. Na siku ya maziko watu wakawa wengi zaidi. Akakamatwa ng'ombe wa mwenye nyumba. Naye akachinjwa!

Ni jogoo, mbuzi na ng'ombe wa mwenye nyumba walioamini kuwa madhara ya mtego ule wa panya yasingewahusu wao. Walikosea. Panya alikuwa sahihi, na wala mtego haukumdhuru panya!

 Kuna cha kujifunza kutoka kwenye kisa hiki. Tutafakari hili tukiyaangalia na ya kwetu yanayotokea sasa bungeni Dodoma, Zanzibar na kwingineko.

Source: raiamwema.co.tz/ya-katiba-na-kisa-cha-mtego-wa-panya- Maggid Mjengwa

No comments:

Post a Comment