WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, August 29, 2014

Mambo manne yaliyotikisa kamati za Bunge la Katiba


Siku 15 za kamati 10 kati ya 12 za Bunge la Katiba ambazo zilikuwa zinajadili vifungu mbalimbali vya Rasimu ya Katiba zimekamilika na sasa wenyeviti wake wapo kwenye hatua za uandishi wa ripoti kwa ajili ya kuiwasilisha ndani ya Bunge Septemba 02, mwaka huu ili mjadala wa wazi uanze .

Kamati zilianza kufanya kazi hiyo Agosti 06, mwaka huu, katika kumbi mbalimbali mjini Dodoma na zilijikita katika kujadili, kuboresha na kuongeza masuala mbalimbali kwenye Rasimu hiyo.

Wakati kamati hizo zikiwa zimejichimbia katika kumbi hizo, kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), limesusia mchakato huo tangu Aprili 16, mwaka huu, kwa kile walichoeleza ni kutoridhika na mwenendo wa Bunge hilo ambalo linaundwa na wajumbe wengi kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM)

Umoja wa Ukawa unaundwa na vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi na CUF ambao kwa nyakati tofauti wameapa kutorejea ndani ya Bunge hilo huku wakishinikiza kusitishwa kwa mchakato huo kwa kuwa hauwezi kuleta Katiba bora.

Mambo manne yaliyojadiliwa kwa kina na kuumiza vichwa vya wajumbe na kuamua kuunda kamati ndogo ndani ya kamati na kwenye kamati ya uongozi ambayo wajumbe wake ni wenyeviti wa kamati zote.

Muundo wa Bunge, uraia pacha, Mahakama ya Kadhi na kamati ya pamoja ya fedha kati ya Bara na Zanzibar ndiyo mambo yaliyoumiza vichwa vya wajumbe hao kwenye kamati na kusababisha mpasuko mkubwa.

Kamati namba moja, Tatu, tano, nane na kumi zilijitokeza mbele ya waandishi wa Habari na kueleza jinsi suala hilo lilivyokuwa na mjadala mpana huku mapendekezo ya wajumbe yakitofautiana.

Mapendekezo ya wajumbe wanaopinga muundo wa sasa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ambalo linajumuisha wabunge wa Bara na wachache kutoka Zanzibar, wametaka kuwepo kwa Bunge litakaloshughulikia masuala ya Muungano pekee, Bara kuwa na Bunge lao la kuzungumzia masuala yao na Zanzibar kuendelea na Baraza la Wawakilishi.

Wengine wametaka kuwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano na chemba mbili kwa ajili ya masuala ya Zanzibar na Bara ambayo yataamuliwa majina na mahali pa kukutana.

Mwenyekiti wa kamati namba moja, Ummy Mwalimu, anasema kamati yake imeshindwa kufanya maamuzi juu ya suala hilo kwa kuwa wapo wajumbe wanaokubaliana na muundo wa sasa na wengine wanapinga.

" Matatizo ya nchi hayawezi kutatuliwa kwa muundo wa mabunge matatu, mfumo uliopo unatosha kabisa kutatua matatizo ya nchi na siyo kutaka kuwepo kwa Bunge jingine la Tanganyika," anasema Makamu Mwenyekiti, Prof. Makame Mbalawa.

Pia, Mahakama ya Kadhi, wajumbe wengi wametaka liingizwe kwenye Rasimu hiyo ili iweze kuhudumiwa na serikali huku wajumbe wengine wakitaka liachwe kwenye dini husika na siyo serikali kuingilia.

Mwenyekiti wa kamati namba nane, Job Ndugai, anasema kamati yake imependekeza kuwepo kwa Bunge la Seneti na mabunge mawili kwa ajili ya Bara kujadili masuala yao na Zanzibar wajadili masuala yao.

Anasema wabunge wa Bunge la Seneti ambalo litakuwa na jukumu la kujadili mambo nyeti ya nchi ikiwamo ya Muungano na wabunge wake watoke kwenye pande za Muungano.

" Wajumbe wengi walisema Zanzibar imepata nafasi ya kuwa na Baraza la Wawakilishi ambalo hujadili masuala yao, bado wanaingia kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano ambalo hujadili masuala ya Bara," anasema.

Mwenyekiti wa kamati namba tatu, Dk. Fransis Michael, anasema kamati yake imependekeza kuwepo kwa Bunge la juu na chembe mbili ambazo zitaruhusu Bara kujadili mambo yao na Zanzibar pia na wachache kuwakilisha kwenye Bunge la juu.

"Muundo wa Bunge zilikuja nadharia nyingi, wabunge wa Zanzibar wanapokuwa huku na miswada ikitoka Bungeni lazima iridhiwe na Baraza la Wawakilishi kwanza, tukakubaliana tuwe na Bunge lenye session mbili, ya kwanza wajadili ya Bara, ya pili wajadili ya Zanzibar na wachache waingie kujadili ya Muungano," anasema.

Mwenyekiti wa kamati namba 10, Anna Abdalah, alisema kamati yake nimeridhika na muundo wa Bunge uliopo na imefuta vyeo vya kuteuliwa ambavyo kwenye Rasimu vimetajwa kuwa viongozi wake lazima wathibitishwe na Bunge.

Anasema kusema kila upande uwe na Bunge lake ni dhambi ya ubaguzi ambayo haitakiwi kwa kuwa muundo uliopo sasa siyo kero.

" Tubaki na muundo uliopo sasa hauna tatizo lolote, kutaka mabunge matatu hata uyape majina gani ni sawa na kutaka serikali tatu ambazo zitavunja Muungano, haikubaliki kamati yetu tunajadili Rasimu kwa maudhui ya serikali mbili hivyo tunaondoa mambo yote yanayohusu serikali tatu," anasema.

Anasema kufanya hivyo ni mwingiliano wa mihimili kwa kuwa muhimili mmoja hauwezi kuwajibisha mtu ambaye hawana mamlaka naye.

" Bunge siyo mwarobaini wa mambo kila mtu ana sehemu yake, kuna muhimili wa serikali, Mahakama na Bunge, tusiingiliane kila mmoja athibitishe watu wake...mfano Mwenyekiti wa Tume ya Maadili na Uwajibikaji athibitishwe na Bunge na wakati huo huo anawasimamia wabunge itatoa nafasi ya kujipendekeza ili achaguliwe," anafafanua.

Makamu mwenyekiti wa kamati namba 11, Hamad Yusuph Masauni, anasema kamati yake imependekeza kuwepo kwa Bunge la Muungano na mabunge mengine ambayo yatajadili masuala ya nchi husika na kukutana kwenye masuala ya pamoja pekee.

Masuala mengine yaliyozua mjadala mkali ni uraia pacha, kiasi cha Bunge kukaribisha mtaalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Boneventure Rutinwa, ambaye alitoa elimu ya suala hilo lakini bado halikuafikiwa kwenye kamati zote na kupelekwa kwenye kamati ndogo ya uongozi.

Hamad Rashid Mohamed, Mwenyekiti wa Kamati namba tano, anasema walijadili kwa kina kwa kujiuliza iweje mtu aliukana uraia wake na kutaka apate haki nyingine na kuliangalia kwa jicho la pana,'' anasema

Masauni anasema kwenye kamati yake wamepitisha uraia pacha, lakini mtu asiwe na haki ya kuchagua au kuchaguliwa katika nafasi yoyote ya uongozi.

Baadhi ya wajumbe wamepinga muundo wa sasa wa Bunge kwa madai kuwa Zanzibar inapata upendelea kuliko Bara na wabunge wake kushiriki, kupiga kura na kuamua juu ya masuala ambayo hayawahusu.

Mjumbe wa kamati namba moja, Alli Kessy, anasema ili kuondokana na kero za Muungano ni lazima kuwe na mabunge matatu ambayo ni Bunge la Muungano, Baraza la Wawakilishi na Tanganyika.

Bunge la Muungano wabunge wake watokane na mabunge ya chini kwa kila moja kuwa na wabunge kumi na kukutana kwa ajili ya kuzungumza masuala ya msingi yanayozikabili nchi husika.

"Kwa sasa wabunge wa Zanzibar wanaingia kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano na kujadili masuala yasiyowahusu kama ya Tamisemi, kilimo, ujenzi na Mifugo ili hali mambo yao wanayajadili kwenye Baraza la Wawakilishi ambalo hakuna Mbunge wa Tanzania anaingia," anasema.

" Lazima Bara tupewa haki yetu ya kujadili masuala yetu kama ilivyo kwa Baraza la Wawakilishi ambalo hatuliingilii kabisa, iweje Mbunge wa Mkajageni apate nafasi ya kujadili na kuamua masuala ya Nkasi ambayo hayamuhusu nami sipati nafasi ya kujadili masuala yao," anafafanua.

Mjumbe mwingine, Ester Bulaya, anasema ni lazima watanganyika wawe na Bunge lao kwa maana ya kuwa na mabunge matatu ya Muungano, Tanganyika na Zanzibar ili kutoa nafasi kwa kila upande kujadili masuala ya msingi ya eneo lao.

" Si lazima tuwe na serikali tatu bali mabunge matatu, yale ya Muungano tuyazungumze kwenye Bunge la pamoja, wenzetu wana Baraza la Wawakilishi wanajadili na Bara hakuna anayeingia ila inapokuwa kujadili masuala ya bara wanashiriki ilihali hayawahusi," alifafanua.

Anasema kuendelea na Bunge la sasa ni kuwanyima haki watu wa Bara hivyo wakati umefika kupewa nafasi ya kujadili na kupanga mambo yao bila kuingiliwa na kuamuliwa.

" Sipati nafasi ya kujadili masuala ya Dole ila wao wanajadili masuala ya Bunda na kwingine kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano, kwa sasa tutenganishe yale ya Muungano ndiyo tuyazungimze kwenye Bunge la Muungano," alibainisha.

Mwenyekiti wa kamati ndogo inayoshughulikia masuala hayo, Suluhu anasema wamemaliza kujadili na kuandika mapendekezo ya masuala ya Mahakama ya Kadhi na uraia pacha ambayo yamewasilishwa kwenye kamati kwa ajili ya kufanya maamuzi ngazi ya kamati.

Kwa upande wake Dk. Michael anasema kamati yake imependekeza kuwa iwapo mgombea urais atatoka Bara, mgombea mwenza atoke Zanzibar na Rais wa Zanzibar awe Makamu wa pili wa Rais.

Tofauti na kamati nyingine, kamati ya Mwalimu na Masauni imependekeza Rais wa Zanzibar awe Makamu wa kwanza wa Rais ili anapokwenda nje ya nchi apate hadhi kama Rais wa Tanzania na Makamu wa pili awe Waziri Mkuu.

Agosti 22, mwaka huu, kamati zilipokea maoni mapya kutoka kwa makundi, taasisi, wananchi na serikali ambayo yatajadiliwa na kuangalia kama wanaweza kuunda sura mpya.

Mapendekezo yaliyoletwa na serikali kupitia kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha Rose Migiro yanahusu masuala ya ardhi, maliasili, mazingira na serikali za mitaa.

Yaliyoletwa na wananchi na taasisi ni nchi kuwa na uchumi imara, haki za wanunuzi wa bidhaa mbalimbali na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( Takukuru), kutaka iruhusiwe kushughulikia wahujumu uchumi.

Kwa mujibu wa kanuni za Bunge hilo kamati itapiga kura kuamua masuala mbalimbali ingawa hazina mamlaka ya kutoa maamuzi ya mwisho na badala yake maamuzi hayo yatatolewa na Bunge zima kwa kupiga kura ili kupata theluthi mbili ya Zanzibar na Bara.

Makundi ya wakulima, wafugaji na wavuvi nayo yaliwasilisha maoni yao kwa uongozi wa Bunge yakitaka matatizo yao yaingizwe kwenye Katiba mpya.
CHANZO CHA HABARI: Na Salome Kitomary: NIPASHE

No comments:

Post a Comment