WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, August 5, 2014

Ukawa wawatia kiwewe Wassira, Mwigulu, Lukuvi
Moshi/Dar. Mawaziri Stephen Wassira na Mwigulu Nchemba wamesema kuwa japo Bunge Maalumu la Katiba litaendelea na vikao vyake kuanzia kesho mjini Dodoma, halitakuwa na uhalali wa kisiasa.

“Tunakwenda bungeni kuendelea na vikao kwa sababu hatuvunji sheria. Kumbukeni hata walipotoka (Ukawa) wakati ule tuliendelea na vikao kwa sababu akidi inaruhusu, japo hatutakuwa na uhalali wa kisiasa lakini kisheria tuna uhalali,” alisema Wasira ambaye ni Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais, Uratibu na Uhusiano).
Hoja hiyo ilisisitizwa na Nchemba ambaye ni Naibu Waziri wa Fedha kuwa vikao hivyo havitakuwa na uhalali wa kisiasa japo kisheria vina uhalali.
“Unajua kilichosababisha mkwamo huu ni kila kundi kushikilia upande wake, kama kila kundi lingeweka masilahi ya Taifa tusingefika huko. Tunakwenda bungeni, ingawa hakutakuwa na uhalali wa kisiasa lakini tutaendelea kujadili mambo ya kitaifa,” alisema Mwigulu.
Viongozi hao walisema hayo baada ya mdahalo wa Katiba uliofanyika Dar es Salam jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi akisema wanakwenda bungeni kuendelea na mijadala japo katiba haitakuwa na afya... “Nawaomba Ukawa warejee bungeni, ikishindikana sisi tutakwenda, tutajadiliana, tutawaletea Katiba bora ila haitakuwa na afya bila Ukawa.”
Wengi waendelea kupinga Bunge
Mbali na mawaziri hao, idadi ya wajumbe wa Bunge hilo wanaopinga vikao hivyo kuendelea bila kushirikisha wenzao wa Umoja wa Bunge la Wananchi (Ukawa) inazidi kuongezeka.
Maoni ya wajumbe hao, baadhi yao wakiwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kutoka CCM, yanatokana na Bunge la Katiba kugubikwa na giza nene baada ya Ukawa, kusisitiza kuwa hawatashiriki vikao hivyo.
Maoni ya wajumbe hao, baadhi yao wakiwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kutoka CCM, yanatokana na Bunge la Katiba kugubikwa na giza nene baada ya Ukawa, kusisitiza kuwa hawatashiriki vikao hivyo.
Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe alisema jana kuwa haungi mkono mpango wa wabunge wenzake wa CCM kuendelea na Bunge la Katiba bila maridhiano.
“Pengine niwakumbushe wabunge wenzangu wa CCM kuwa kinachoandaliwa kwenye Bunge la Katiba ni Katiba ya Watanzania wote na si Katiba ya CCM. Hatua tuliyofikia siiungi mkono, kitendo cha wabunge wenzangu wa CCM kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya kwa sababu suala la Katiba halina mshindi ni jambo la maridhiano.
“Kitendo cha sisi wabunge wa CCM kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya ni matumizi mabaya ya wingi wetu mle bungeni. Ni kweli CCM ina wabunge wengi na ni kweli kwenye demokrasia wengi wape, lakini pia demokrasia pevu na yenye tija ni ile inayoheshimu na kuyafanyia kazi maoni ya wachache.”
Hata hivyo, mbunge huyo alisema wajumbe wa Ukawa walipaswa kubaki ndani ya chombo hicho na kujenga hoja zao.
“Ni lazima (Ukawa) watambue sisi wajumbe siyo waamuzi wa mwisho. Tutafanya yote lakini waamuzi wa mwisho ni wananchi kwani ndiyo wanaoweza kupiga kura ya kuikataa au kuikubali,” alisema.
Mjumbe mwingine wa Bunge hilo, Maria Sarungi alisema Katiba inapaswa kuwa mkataba wa pamoja lakini bila maridhiano inakuwa ni waraka unayokosa uhalali wa kukubalika kwa jamii.
Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli alimsihi Rais Jakaya Kikwete kuangalia njia bora ya kunusuru fedha za walipa kodi maskini zinazotumika katika mchakato wa Katiba Mpya.
“Kama Katiba ni ya wananchi tulipaswa kuwa kitu kimoja, kwamba tunaingia mle ndani kwa masilahi ya Watanzania lakini kama hakuna mwafaka hadi sasa huko mbele ni giza nene.
“Kwa maoni yangu hekima itumike. Ni busara tu imebaki kwa wakubwa kuona fedha za Watanzania zinatumika vizuri. Rais Kikwete awatazame Watanzania kwa macho ya huruma,” alisema.
Mbunge wa Mchinga (CCM), Said Mtanda alisema wajumbe kutoka CCM wanaweza kuendelea na vikao vya Bunge la Katiba, lakini lingekuwa jambo muhimu iwapo yangefanyika maridhiano ya pande mbili zinazovutana.
“Kama akidi itatimia vikao vitaendelea kama kawaida. Lakini hata kama itatimia nadhani si busara vikao vya Bunge kuendelea kwa mtindo huo, binafsi naona turidhiane ili kunusuru hali hii,” alisema.
Hata hivyo, Mtanda aliwataka Ukawa kutambua kuwa si lazima kila jambo wanalolitaka litakubaliwa na kuwa iwapo watashikilia msimamo huo ipo siku wananchi watawahukumu.
Mbunge wa Longido (CCM), Lekule Laizer alisema lingekuwa jambo la busara kama vikao vya Bunge hilo vingeitishwa baada ya pande mbili zinazovutana kukubaliana.
Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamisi Kigwangalla alisema, “Yangefanyika maridhiano kwanza na kama hilo litashindikana ni vyema viongozi wa vyama vya siasa wangeondolewa kuwa sehemu ya Bunge hili, ili kuondoa hali ya kila upande kuvutia kwake.”

Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango alisema hata bila Ukawa vikao vya Bunge hilo vitaendelea kwa sababu wajumbe wa kundi hilo walisusia kikao cha maridhiano kilichoitishwa na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta.
“Bunge la Katiba lina wajumbe 629 na kama Ukawa wasipokuja sidhani kama watazuia vikao kuendelea kwa sababu hata watu 100 hawafiki. Kikao cha Sitta ndicho kilikuwa kizuri kwa maridhiano,” alisema Kilango
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ali Keissy alisema, “Katiba ni ya wananchi wote ni vyema tungekubaliana kwanza.”
Tangu wajumbe wa Ukawa kususia Bunge, baadhi ya wajumbe, wakiwamo wabunge wa CCM wamekuwa wakitoa maoni yanayoonyesha kuwa bila wenzao hao, katiba itakayopatikana haitakuwa ya kidemokrasia.
Miongoni mwa wabunge hao ni Ridhiwani Kikwete wa Chalinze alisema katika mahojiano maalumu na gazeti hili kuwa iwapo wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka CCM watalazimisha mambo bila ushiriki wa wenzao wa Ukawa, kuna hatari ya kupata Katiba isiyokuwa na misingi ya kidemokrasia.
“Kwa mazingira tuliyonayo wabunge wa CCM wanaweza kuamua kwamba walazimishe vitu, lakini ile misingi ya demokrasia haitakuwapo,” alisema Ridhiwani na ambaye pia ni mtoto wa Rais Kikwete na kuongeza: “Kwa sababu kupata Katiba ya kidemokrasia ni lazima taratibu zifuatwe na Ukawa washiriki, lakini bila wao kushiriki huwezi kusema Katiba tuliyopata ni ya kidemokrasia, tutakuwa tunajiongopea.
“Wao (Ukawa) wasipokuja na kama busara ya viongozi wetu wa chama, busara za Bunge letu na busara ya Rais itatuonyesha kwamba tukutane tu na tujadili, sisi tutakuja, tutajadili na tutaipitisha lakini mwisho wa siku, ule uhalali wa document (kilichopitishwa) hautakuwepo.”
Wiki iliyopita gazeti hili liliwanukuu wabunge wengine wa CCM wakipendekeza kusitishwa kwa Bunge hilo ili kutafuta maridhiano kwanza.
Miongoni mwao ni Charles Mwijage (Muleba Kaskazini) ambaye alisema, “Kukosekana kwa Ukawa bungeni kutaathiri upatikanaji wa Katiba Mpya...Ningekuwa na uwezo, ningeamua mchakato huu usitishwe na tuendelee kutumia Katiba iliyopo kwa sababu suala hili linahitaji zaidi maridhiano,” alisema.
Mjumbe mwingine, Ezekiah Oluoch (Kundi la 201) alisema: “Katiba haipatikani kwa ubabe au wengi wape, bali inapatikana kwa maridhiano na mwafaka bila kujali wingi wa wajumbe.”
Mbunge wa Mbeya Vijijini, Lackson Mwanjali alisema kitendo cha Ukawa kukataa kurejea bungeni ni pigo katika mchakato wa Katiba Mpya kwa sababu Katiba inatengenezwa kwa majadiliano na kufikia mwafaka.
Imeandikwa na Elias Msuya, Daniel Mjema na Fidelis Butahe
SOURCE: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment