WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, August 8, 2014

Demokrasia ya kimagharibi chanzo cha fujo Afrika

Dk.Peter Kafumu
Miaka ya hivi karibuni suala la demokrasia ya vyama vingi kujengwa katika nchi za Afrika limekuwa ni mdahalo mkali kwenye majukwaa ya kisomi, kijamii na kisiasa.

Baadhi ya wasomi, wataalamu wa masuala ya siasa na wanaharakati wamekuwa wakiwalaumu viongozi wanaochaguliwa kwa kutoifahamu na kuifuata demokrasia hii ipasavyo, kiasi cha kusababisha fujo, mgawanyiko na hata mauaji katika nchi maskini zinazoendelea.

Kwa maoni yangu demokrasia hii yenye msingi wake katika nchi zilizoendelea za Ulaya na Marekani haifai kujengwa Afrika kutokana na historia ya bara hili na hali ya kiuchumi na utamaduni wake kwani demokrasia hii imekuwa chanzo cha migogoro miongoni mwa Waafrika.

Ghasia zikihamasishwa na chuki baina ya vyama vinavyoshindana ndani ya jamii limekuwa ni jambo la kawaida katika siasa za Afrika. Mataifa ya Kusini mwa Jangwa la Sahara kama vile Kenya, Zambia, Zimbabwe, Malawi na Tanzania ni mifano mizuri ya madhara ya demokrasia ya kimagharibi katika nchi maskini na zinazoendelea.

Kwa kweli, kuijenga na kuiishi demokrasia ya kimagharibi katika nchi za Afrika limekuwa ni jambo tete.

Pamoja na hayo Afrika pia imeshuhudia nchi za kimagharibi zikijaribu kuziingiza kwa nguvu kwenye demokrasia ya vyama vingi nchi zilizokuwa na amani lakini hazikuwa na demokrasia kamili kwa vigezo vya nchi zilizoendelea.

Nchi hizo kabla ya kulazimishwa kuingia katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi zilikuwa na utawala wa sheria kadiri ya mazingira ya nchi hizo.

Mifano ya nchi hizo zilizolazimishwa kwa nguvu kuingia katika mfumo wa demokrasia ya kimagharibi ni kama Libya, Tunisia, na Misri. Mataifa haya yalionekana awali kuwa na hali ya ustawi kutokana na uchumi mzuri uliojengwa chini ya utawala unaolingana na matakwa ya nchi hizo.

Kwa sasa chuki na mgawanyiko vimekuwa ni tishio kubwa kwa dola hizo ambazo zilikuwa na utulivu na ustawi. Watu wake wamegawanyika kutokana na demokrasia ya vyama vingi iliyopandikizwa na Wamagharibi na mauaji sasa yanatokea kwa sababu ya kukiukwa kwa haki za binadamu.

Kwa hakika hali katika nchi hizi inaonyesha ubeberu uliokomaa.

Hii inanikumbusha maneno ya mmoja wa waasisi wa Bara la Afrika, Rais wa kwanza wa Ghana Dk. Nkwame Nkurumah, ambaye aliona demokrasia ya kimagharibi kama silaha ya mabeberu kuendeleza ukoloni mamboleo na hakukosea kwani tukiangalia yaliyotokea na yanayoendelea katika nchi za Libya, Misri na Syria yanadhihirisha ukweli huo.

Kwa sasa watu wengi wanaamini kwamba demokrasia ya kimagharibi haitekelezeki barani Afrika kwa sababu haifai kwa nchi maskini.

Waafrika hawajaandaliwa kiuchumi kuingia katika demokrasia hii.

Wasomi wengi leo wanakubali kwamba si sahihi kutumia mifumo ya kidemokrasia ya kimagharibi katika nchi za Bara la Afrika. Bara la Afrika linahitaji demokrasia ambayo itahamasisha umoja na utulivu miongoni mwa watu, ili kuleta mazingira ya kukuza uchumi kwa faida ya vizazi vijavyo.

Afrika ni maskini sana kwa demokrasia; hali ya uchumi wa nchi nyingi bado ipo katika ngazi ya ujima na haijafikia hali ya maendeleo ya viwanda, ikilinganishwa na hali ya nchi za Magharibi.

Bara la Afrika bado ni soko la bidhaa za viwanda na teknolojia, na linaanguka kiuchumi kutokana na kuiga (kwa kulazimishwa) mahitaji ya kidemokrasia ya kimagharibi yanayodai uhuru wa kisiasa uliopitiliza na jamii iliyowazi bila mipaka. Uhuru unaosahau masilahi ya taifa husika.

Katika mustakabali wa kujenga demokrasia hiyo ngeni, nchi hizi hujikuta zimefunikwa na harakati za kujenga demokrasia huku zikisahau masilahi na umoja wa taifa hilo na kazi ya kujenga uchumi wake.

Katika hali yakusahau, nchi hizi zimejikuta katika mgogoro mkubwa wa mgawanyiko wa watu wake.

Demokrasia iliyokamilifu na ya kweli; inahitaji uchumi wenye nguvu, kuwapo kwa mahitaji muhimu kwa jamii kabla ya kujiingiza katika demokrasia ya ushindani ya kimagharibi isiyo na mipaka.

Nchi zilizoendelea kama vile Marekani, Uingereza, Norway, Ufaransa, Ujerumani na nchi nyingi za Ulaya ziko kwenye demokrasia hii kutokana na hatua nzuri zilizofikia kiuchumi, ambapo masuala ya huduma za msingi za watu wake zipo.

Na hivyo mashindano ya kisiasa katika demokrasia hayaathiri maisha ya kawaida ya raia wake. Kwa maneno mengine uchumi wa nchi hizi unahimili utoaji wa maisha bora kwa kila raia na suala la wananchi kugombanishwa wakati wa uchaguzi halipo tena, masilahi ya nchi yanalindwa wakati wote.

Nchi hizi zilijenga uchumi wake kwanza kabla ya kuingia kwenye demokrasia hii gawanyi. Katika nchi nyingi baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, zilijikita sana katika kujenga uchumi wake na baadaye kuangalia masuala ya demokrasia.

Nchi ya Marekani kwa mfano hadi kufikia mwisho wa miaka ya 50 hakukuwa na uhuru wowote katika uchaguzi, watu weusi na wanawake hawakuruhusiwa kupiga kura, hadi leo katika nchi ya Marekani kuna Majimbo na Maseneta wenye kura ya turufu inapotokea kuwa ni lazima kulinda masilahi ya taifa katika uchaguzi.

Nchi nyingi za Ulaya pia, pamoja na kuwapo kwa demokrasia huria, wafalme wanayo nafasi yao ya kutawala bila kuchaguliwa ili kulinda umoja, mshikamano na utaifa wa nchi hizo.

Kimsingi demokrasia ya kimagharibi imefaa zaidi katika nchi zenye uchumi uliokomaa.

Siyo sahihi kuanza kujenga demokrasia kwanza na baadaye kujenga uchumi, ni vyema kutetea masilahi ya taifa na kujenga uchumi kwa lazima na baadaye kuingia kwenye demokrasia ya vyama vingi.

Nchi zinazoendelea na maskini za Afrika kutokana na uhaba wa huduma za jamii, Serikali na Chama tawala katika nchi hizi maskini hushutumiwa kwa kasoro zote katika utoaji wa huduma hizo na maendeleo ya kiuchumi.

Chama chochote kitakachoshinda kwenye uchaguzi katika nchi nyingi za Bara la Afrika na kuwa chama tawala hukutana na lawama zilezile katika chaguzi zinazofuata.

Katika kila uchaguzi, fujo, na vurugu huchochewa na kuendelea baada ya uchaguzi kiasi kwamba ujenzi wa uchumi husahaulika kabisa katika mazingira hayo ya siasa za ugomvi.

Mifano ya hali hii ni kama vile wakati chama cha ukombozi cha Kenya cha KANU kilipoondolewa madarakani Wakenya wengi walidhani matatizo yao ya kiuchumi yamekwisha kwa sababu mafisadi wameondoka, lakini badala yake nchi ya Kenya ilishuhudia kuundwa kwa vyama vya kila aina vilivyotokana na ugomvi wa kisiasa uliohamasishwa na ubeberu kutoka nje ya Kenya.

Kwanza Chama cha Upinde wa Mvua cha NARC kiliundwa, lakini muda si mrefu ugomvi ukaendelea katika chama hicho na kufikia kuundwa chama cha umoja wa kitaifa PNU, baadaye chama cha ODM viliibuka.

Mabadiliko yote haya yaliifanya Kenya kuwa katika fujo za kisiasa zisizotabirika kila mwanasiasa akipigania kuingia Ikulu tena kwa nguvu. Katika hali hiyo wananchi raia waliteseka na baadhi walikufa.

Kila chama kipya kilipopata madaraka nchini Kenya wananchi walitumaini kwamba wangesonga mbele lakini chama hicho kiliambulia kukumbana na vikwazo vilevile kama vya awali. Na chaguzi zilizofuata Kenya ikashuhudia mauaji ya raia wasio na hatia kwa sababu chama tawala kilituhumiwa tena kwa kushindwa kujenga uchumi na kuboresha huduma za jamii kulingana na matarajio ya wananchi.

Tunajiuliza katika mazingira haya, hivi kweli Afrika inahitaji demokrasia ya namna hii inayogawanya na kugombanisha watu wake na kusababisha mauaji.

Zimbabwe ni nchi nyingine ya mfano katika nchi hizi za Afrika inayolazimishwa kujenga demokrasia huria ya kimagharibi.

Katika hali hiyo uadui na ugomvi mkubwa miongoni mwa wanachama wa chama cha ukombozi cha Zimbabwe cha ZANU - PF kinachoongozwa na Rais Robert Mugabe na kile cha MDC cha Morgan Shangirai.

Japokuwa hapo awali Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilileta amani ya muda, lakini uchaguzi uliopita tulishuhudia shutuma zilezile za mgawanyiko kwa wananchi wa Zimbabwe, wakihasimiana na kushindana bila kujali umoja wa taifa lao.

Zambia nayo ni mfano mwingine ambapo demokrasia ya kimagharibi haijaleta maendeleo ya kiuchumi yaliyotarajiwa. Chama cha ukombozi cha UNIP kilipoondolewa madarakani na mpinzani wake MMD, Wazambia walitarajia mageuzi makubwa sana ya kiuchumi lakini hadi leo taifa hilo linasuasua.

MMD baada ya kuwa madarakani vipindi vinne kilimaliza muda wake hali ya kiuchumi ya nchi hiyo ikizidi kudorora, baadaye chama cha PF cha Michael Sata kiliingia madarakani kikiahidi kuwaondoa wawekezaji wote kwa kufuta mikataba tata ya uwekezaji kwenye madini ya shaba, lakini hadi leo wawekezaji na mikataba yao wapo na bado Zambia ni nchi maskini.

“Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alipoulizwa kuhusu demokrasia hii alionya na kusema; ...demokrasia siyo chupa ya Coca-Cola unayoweza kuiagiza kutoka nje...sijawahi kwenda kwenye nchi yoyote na kuona vyama vingi halafu nikaamini kwamba nchi hiyo inayo demokrasia ya kweli...huwezi kuamini kuna demokrasia eti kwa sababu kuna vyama vingi.”

Baba wa Taifa aliamini pia kuwa demokrasia ya vyama vingi si kitu cha Waafrika ni jambo la Kimagharibi na si lazima kwa Afrika na kinaweza kuleta mgawanyiko miongoni mwa watu wa Tanzania, taifa lenye makabila zaidi ya 127.

Maneno ya Muasisi wa Taifa letu yanathibitisha kuwa hapa Tanzania demokrasia ya kimagharibi ya vyama vingi ni jinamizi lisilojulikana linatupeleka wapi.

Vyama vya siasa vinaendelea kuwagawanya wananchi . Baadhi ya vyama vimepata nguvu kwenye baadhi ya maeneo na makabila fulani, na si ajabu kuona watu wa makabila fulani kupendelea kuwa wanachama wa chama fulani tu.

Taifa letu sasa umoja wake uko majaribuni na hasa katika kipindi hiki cha kuandaa katiba mpya, tusipokuwa waangalifu tunaweza kulipasua taifa kutokana na uroho wa baadhi ya viongozi wa vyama wa kupata utawala wa dola. Viongozi wetu leo badala ya kuangalia masilahi mapana ya nchi wamegubikwa na tamaa ya kutawala.

Katika siasa hizi gawanyishi, wananchi wanahamasishwa kuamini kuwa chama tawala na serikali ni vya kulaumiwa kwa kila ugumu wa maisha na uchumi duni, bila kufahamu kuwa tatizo letu kubwa sasa tumesahau kujenga uchumi tumefungwa na siasa za kulaumiana na kutukanana, tumepofushwa na propaganda za kigeni za kuamini kuwa matatizo yetu yapo katika demokrasia kumbe tumesahau kujenga utamaduni wa kujenga uchumi wetu kwa nguvu hata za kidikteta.

Ama kwa hakika michakato ya ujenzi wa demokrasia katika nchi maskini za Afrika, badala ya kuleta ustawi na maendeleo ya kiuchumi imehamasisha na kuleta chuki, wivu, choyo na uroho wa ama kung’ang’ania madaraka ama kutaka kuingia kwa nguvu madarakani.

Michakato hii pia imehamasisha jamii itengane na kuchukiana. Hii inatokana na baadhi ya viongozi kuhamasisha chuki na utengano kwa kisingizio cha Demokrasia.

Tumeshindwa kujenga hoja na utamaduni wa kushindana bila kutukanana wala kupigana, tumeshindwa kujenga utamaduni wa kuthamini kwanza masilahi mapana ya Taifa na kujikita katika kujenga uchumi wetu badala yake viongozi wa kisiasa wanajenga hoja za kuchonganisha jamii na kuleta utengano na chuki miongoni mwa wananchi.

Chuki zinazoendelezwa leo katika kukumbatia demokrasia hii ya kimagharibi ni chachu na chumvi mbaya itakayoleta vurugu na mauaji ndani ya taifa letu huku wakubwa wakichekelea.

Pengine twaweza kujifunza kutoka Jamhuri ya Watu wa China ambapo katika nchi hiyo kuna Chama kimoja chenye nguvu na kinatawala na wengine ni mfano tu. Kitu kikubwa kinachofanya chama hicho tawala ni kujenga uchumi wa taifa hilo ili liwe lenye nguvu duniani.

Nchi nyingine ya kujifunza ni Malaysia, ambako pamoja na kuchagua serikali kwa demokrasia ya vyama vingi nafasi ya ufalme katika ujenzi wa uchumi na umoja wa taifa ni kubwa sana. Nchi nyingine ni Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), na Saudi Arabia ambazo suala la kujenga uchumi na kuleta ustawi wa watu wake ni la kufa na kupona.

Mwandishi wa makala hii ni Mbunge wa Igunga kwa tiketi ya (CCM).
SOURCE: NIPASHE

2 comments:

  1. nimeipenda sana it good una heri dunian na mbinguni yes yes yes

    ReplyDelete
  2. I like that whats you explained and its fact yes yes--------------

    ReplyDelete