WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, August 15, 2014

Kiburi cha kupendwa kimefanya upinzani kuvaa u-CCM – III


 

KATIKA sehemu ya pili ya makala haya nilihitimisha kwamba kadri upinzani unavyokua ndivyo unavyozidi kufanana na CCM kimuundo na matendo ya viongozi wake. Niliahidi kumalizia mada yangu kwa kufafanua dhana hii ya upinzani kufanana na CCM.

Ninamalizia makala haya kwa kueleza baadhi ya viashiria vunavyofanya upinzani uanze kufanana na CCM. Kiashiria cha kwanza ni matumizi ya dhana ya usaliti. Tulipoanza mfumo wa vyama vingi miaka ya tisini CCM walitumia sana dhana ya usaliti katika kuvidhoofisha vyama vya upinzani. Kwamba wapinzani ni vibaraka wa wazungu na wanatumiwa katika kuharibu amani ya nchi.

Wapinzani wakatangazwa kwamba ni wasaliti wa nchi kwa kupingana na chama tawala kilicholeta amani, utulivu na mshikamano. CCM hawakupinga upinzani kwa hoja, bali kwa kuwaaminisha wananchi kwamba hawa ni watu hatari. Mwanzoni wananchi walikubaliana na dhana hii na ilihitaji moyo mkuu katika kujipambanua kwamba wewe ni mpinzani. Lakini ilikuwa ni suala la muda tu.

Hatimaye ukweli ulijulikana na wananchi sasa wanaelewa kwamba kumbe hata wapinzani ni Watanzania wenye nia njema na nchi yao, na wanashindana katika namna bora zaidi ya kutawala na kuendesha nchi. Sasa miaka zaidi ya ishirini baada ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi, upinzani nao wanaanza kutumia mbinu hiyohiyo ya dhana ya usaliti katika kuzima sauti kosoaji ndani ya vyama vyao. Kwamba leo mwanachama yeyote anayethubutu kuwakosoa viongozi anaitwa msaliti.

Tena usaliti wenyewe ni pale ambapo mwanachama anathubutu kutaka kugombea nafasi fulani ya uongozi na anaonekana kuwa na uwezekano wa kushinda hiyo nafasi anayoitaka. Mwanachama wa namna hii atatangazwa dunia nzima kwamba ni msaliti na anatumiwa na chama tawala katika kudhoofisha upinzani. Lakini ukweli ni kwamba dhana nzima ya demokrasia imejengwa katika hoja kinzani na ushindani katika chaguzi. Uimla na uhodhi ni dhana za kikomunisti.

 Katika mfumo wa kikomunisti, viongozi wapo sahihi wakati wote na yeyote anayewakosoa anakuwa msaliti mkubwa. Vilevile katika mfumo wa kikomunisit viongozi hutokana na kundi dogo la wateule wa uongozi na yeyote asiyeteuliwa na kundi hili ni msaliti na hafai. Hivi ndivyo CCM ilivyojengwa huko nyuma na ndio maana akina Oscar Kambona ilibidi wakimbie nchi pale walipotamani kukwea ngazi za juu za uongozi wakati walikuwa hawatoki katika kundi la wateule.

Sasa leo hii wakati dunia nzima ikiachana na ukomunisti, vyama vya upinzani ndio kwanza vinavaa utamaduni wa kikomunisti wa kuwambambikizia usaliti wanachama wao wanaodiriki kukosoa viongozi na kutamani nafasi za juu za uongozi ndani ya vyama vyao. Dhana ya usaliti katika vyama vya upinzani inajengwa pia kwa wabunge wanaokwenda kinyume na misimamo ya vyama vyao.

Kwa mfano, sasa hivi kuna baadhi ya wabunge wanaotokana na vyama vinavyounda kundi la UKAWA wameamua kwenda kinyume na vyama vyao kwa kuhudhuria vikao vya Bunge Maalumu la Katiba vinavyoendelea mjini Dodoma. Wabunge hawa wametangazwa dunia nzima kwamba ni wasaliti na wameambiwa watafukuzwa wakati wowote ili wabaki kuwa wabunge wa mahakama. Hii nayo ni dalili ya ushamba na kutokuelewa dhana ya demokrasia katika mfumo wa vyama vingi. Ukweli ni kwamba katika utamaduni wa mfumo wa vyama vingi kuna wabunge wachache hutokea kuwa na misimamo huru na vyama vyao. Hii ni kwa sababu dira ya utumishi wa mbunge wakati wote huongozwa na mambo manne, ambayo ni utashi wake mwenyewe, wananchi wa jimbo lake, taifa na chama chake.

 Inapotokea kwamba kuna mgongano wa kiutashi baina ya mambo haya, mbunge ana haki ya kuamua kadri nafsi na uelewa wake unavyomtuma. Kwa sababu nilizozieleza hapo juu ni jambo la kawaida sana wabunge duniani kwenda kinyume na misimamo ya vyama vyao. Kwa mfano, mwezi Aprili mwaka huu wabunge 20 wa Chama cha Conservatives cha Uingereza walipinga muswada uliokuwa umependekezwa na Waziri Mkuu, David Cameron wa kuruhusu vyombo vya dola kuingia umbali wa mita 500 wa nyumba za watu binafsi wakati wowote kwa ajili ya upekuzi kwa sababu za kiusalama.

Muswada huu ulipita kwa mbinde baada ya kuungwa mkono na wabunge wa chama cha upinzani cha Labour. Vilevile mwezi Machi mwaka jana, wabunge wa Conservatives, akiwemo Waziri wa Mazingira, Owen Paterson, walipinga muswada wa ushoga uliopendekezwa na serikali na ulipita tu baada ya kuungwa mkono wa wabunge wa chama cha Labour.

 Lakini wabunge hawa wa Conservatives hawakuitwa wasaliti. John McCain ni mbunge maarufu na mkongwe wa chama cha Republicans nchini Marekani. Huyu anajulikana kama ‘maverick’ kwa sababu ya misimamo yake ya kuwa mbunge huru ambaye amekuwa akienda kinyume na misimamo ya chama chake, hasa wakati wa utawala wa Rais George Bush. Huyu hakuitwa msaliti na hata alipata fursa ya kugombea nafasi ya urais. Kwa ushamba wetu wa dhana ya demokrasia ingekuwa kwetu angefukuzwa siku nyingi na angeitwa msaliti kwa kutumiwa na chama pinzani.

 Ni aibu kwamba vyama vya upinzani vinazidiwa hata na CCM katika kuwavumilia wakosoaji wao. Kwa tabia ya uhodhi, uimla na ufashisti inayojionyesha ndani ya upinzani, wabunge kama akina Deo Filikunjombe, Kangi Lugola, Samweli Sitta, n.k. wangeshafukuziliwa mbali kama wangekuwa wanachama wa upinzani kwa misimamo yao ya kwenda kinyume na chama chao mara kwa mara.

Tutakumbuka kwamba Filikunjombe ni miongoni mwa wabunge waliosaini waraka wa kutaka kumng’oa waziri mkuu. Lakini hakuitwa msaliti na chama chake. Sijui hali ingekuwaje kama ingetokea mbunge wa upinzani angesaini waraka wa kutaka Kiongozi wa Upinzani Bunge ang’olewe! Pengine jambo la kutisha zaidi ni kauli iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CHADEMA hivi karibuni kwamba chama hiki sasa kilikuwa kinaachana na uanaharakati na sasa kinajiandaa kuwa chama dola.

Kauli za namna hii ni za hatari na zinatoa tu kiashiria cha dhamira ya baadhi ya viongozi katika muktadha wa demokrasia katika mambo mawili. Mosi, dhana pana ya neno harakati ni ile hali ya kupigania haki za watu au kundi fulani la watu, hasa wanyonge, na ni kazi mojawapo muhimu sana kwa chama chochote cha siasa, na hasa chama cha upinzani. Sasa chama kinapotangazia dunia kwamba kinaachana na harakati maana yake ni kwamba kimeamua kuachana na kupigania haki za watu.

 Pili, sababu mojawapo ya kutaka kuiondoa CCM madarakani ni ukweli kwamba chama hiki ni chama dola ambacho kimejipenyeza katika kila maisha ya umma. Kwa muundo wake, ni vigumu kwa CCM kuendelea kuwepo bila dola na vyama vya aina yake vilikufa mara moja baada ya kupoteza dola kama ilivyotokea kwa KANU na UNIP. Chama hiki kilitengeneza mazingira kwamba mtu yeyote afanyaye kazi katika utumishi wa umma, kwa mfano, sharti aunge mkono na kuisaidia CCM.

 Wafanyabiashara nao wanahisi kwamba biashara zao haziwezi kwenda bila mkono wa chama hiki. Sasa tunapambana ili kuwaweka huru watu wote wasijikute wanaishi maisha ya ufungwa kwa kulazimika kuunga mkono chama fulani cha siasa. Ndio maana hatuhitaji tena vyama dola katika siasa zetu kwa sababu vyama vya namna hii ni vyama vya kikomunisti. Kwa hiyo Katibu Mkuu anapotuambia kwamba wanataka kubadilisha chama chao kiwe chama dola maana yake anatuambia kwamba anatutengenezea CCM nyingine katika maisha yetu!

 Sijui kama alielewa dhana ya chama dola vizuri wakati anatoa hii kauli. Lakini upinzani unafanya makosa yote haya kwa sababu viongozi wakewamefuga washabiki ambao kazi yao kubwa ni kushangilia kila walisemalo na wanalitendalo. Katika vyama hivi wanachama na wafuasi wanaoitwa kwa kiingereza ‘critical followers’ hakuna na wakijitokeza wachache wanashughulikiwa. Kwa hiyo kwa muundo wake na matendo ya viongozi wake, vyama hivi haviwezi kuzalisha akina ‘John McCain’, na kwa sababu hiyo havina wakosoaji wanaoweza kuwafanya wajitazame. Kwa sababu hii vimejenga kiburi cha kupendwa kwamba hata wakifanya mambo ya kipuuzi watashangiliwa. Athari za muda mrefu ni kwamba wananchi watashindwa kuvitofautisha na CCM.

 Ndio maana katika utafiti wa shirika la Twaweza uliotolewa wiki iliyopita ulionyesha kwamba asilimia sabini (70%) ya watanzania hawaamini kwamba upinzani utafanya tofauti na CCM katika kupambana na rushwa! Ujumbe wangu ni kwamba lazima upinzani ufanye kazi ya ziada katika kutengeneza taswira chanya kwa kukumbatia demokrasia kwa uhalisia wake, na kuacha kufanya mambo ya ki-CCM. Vinginevyo, wananchi watatuone ni walewale tu! –

No comments:

Post a Comment