WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, August 8, 2014

Ukawa wapata pigo jingine

Mbunge Said Arfi wa Chadema akijisajili kushiriki Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma jana.
Wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi Ukawa waliojisajili kushiriki vikao vinavyoendelea vya mkutano wa Bunge Maalumu la Katiba wameongezeka kutoka wawili hadi kufikia sita huku watatu kati yao wakichukua kabisa posho zao za siku saba mfululizo.

Idadi hiyo inafuatia wajumbe wanne, wakiwamo watatu kutoka Chama cha Wananchi (CUF) na mmoja kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kufanya usajili jana.

Vyama hivyo vikubwa vya upinzani nchini, pamoja na NCCGR - Mageuzi, ndivyo vinavyounda Ukawa na maagizo yaliyotolewa na viongozi wao ni kutorejea bungeni kwavile hawako tayari kuona mapendekezo ya rasimu ya katiba yaliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji mstaafu Joseph Warioba yakibadilishwa kutoka kuwa na muundo wa muungano wa serikali tatu kama ilivyotakiwa na wananchi wengi kupitia maoni waliyotoa kwa tume na kuwa (muungano) wa serikali mbili unaopendekezwa na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Waliofanya usajili jana ni Fatma Mohamed Hassan na Jamila Abeid waliongia kupitia kundi la 201 kutoka CUF na Ali Omar Juma ambaye ni Mbunge wa Jimbo la ......kupitia CUF. Na kila mmoja miongoni mwao ameshachukua posho zote za siku saba, sawa na takriban Sh. milioni 2.1.
Mjumbe mwingine kutoka Ukawa aliyejisajili ni Makamu Mwenyekiti wa zamani wa Chadema na Mbunge wa Mpanda Mjini kupitia chama hicho, Said Arfi.

Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahya Hamis Hamad, ndiye aliyethibitisha kujisajili kwa wajumbe hao na baadhi kuchukua posho zao wakati alipozungumza na NIPASHE jana.

Katibu huyo alisema kufuatia ongezeko la wajumbe hao wanne, sasa idadi kamili ya wajumbe wa Ukawa waliofika na kujisajili ili kuendelea na mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya wamefikia sita hadi kufikia jana na hivyo kuifanya akidi ya wajumbe wa Bunge hilo kuongezeka.

Wengine wawili kutoka Chadema walishajisajili kuanzia Agosti tano, ambao ni Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda na Mbunge wa Viti Maalum, Leticia Nyerere.

Alisema wajumbe hao wapo mjini Dodoma hivi sasa wakiendelea kushiriki vikao vya kamati za bunge vinavyoendelea kujadili sura 15 za rasimu ya katiba zilizosalia baada ya kukamilika kwa mjadal wa sura za kwanza na za sita zilizozungumzia muundo wa muungano.

Wajumbe hao watatu wa CUF wamo katika kundi la watu 16 muhimu ambao wanaweza kuamua hatma ya upigaji kura kufikia theluthi mbili kutoka Zanzibar katika Bunge hilo baadaye, kuanzia Oktoba 10 hadi 21 mwaka huu wakati zoezi la kura litakapoanza rasmi.

“Wajumbe watatu wa Ukawa kutoka Zanzibar wameshawasili na wameanza vikao vya kamati vinavyoendelea na nilivyozungumza na wahasibu wangu wamenitaarifu kwamba wamewalipa posho ya siku saba,” alisema Katibu huyo.

Alisema wajumbe wengine ambao ni Arfi, Shibuda na Leticia wamefanya usajili lakini hawajalipwa chochote mpaka sasa kwa sababu ushiriki wao wa moja kwa moja haujaonekana kwenye kamati za bunge.

ARFI ANENA
Akizungumza na NIPASHE jana kuhusiana na uamuzi wake wa kurejea bungeni, Mjumbe wa Bunge hilo, Arfi alisema ana haki ya kuingia kwenye vikao vya Bunge hilo akiwa kama Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kauli hiyo aliitoa jana bungeni alipokwenda kwa ajili ya kufanya usajili wa kushiriki kwenye vikao vya Bunge hilo vinavyoendelea mjini hapa.

Alisema ameamua kurejea kwenye vikao hivyo kwa ajili ya kutimiza wajibu wake kwa kuwawakilisha wananchi wake.

“Nimekuja kuangalia taratibu za kujisajili kwa sababu mimi ni mjumbe wa Bunge maalum la Katiba na nimechaguliwa kuingia katika bunge hili kwa mujibu wa sheria," alisema Arfi.

Aliongeza: “Sheria tuliitunga na tukakubali kabisa (kuwa) makundi matatu yashiriki katika Bunge Maalum, wakiwamo Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mimi ni miongoni mwa hao wabunge wa Jamhuri... wengine ni wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na pia kundi kutoka katika jamii pana ya watanzania ambayo watu 201 waliteuliwa na Rais.”

Alipoulizwa kuhusu kupingana na chama chake (Chadema), alisema vyama vinataka kupokonya mamlaka ya wananchi hivyo iwapo wataendelea kukubali hali hiyo hawatawatendea haki wananchi na hivyo, si vizuri kuruhusu vyama vifanye vinavyotaka.

Alisema katika Bunge Mmaalum la Katiba, wajumbe wa bunge hilo wako katika sura tofauti na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambako huko huwa wanaingia kama makundi ya vyama na ndiyo maana kuna kambi rasmi ya upinzani.

“Humu ndani ya Bunge kuna makundi mawili tu…kundi la Watanzania Bara na Wazanzibar, kwa hiyo mimi nawakilisha kundi la Watanzania Bara,” alisema.
Mwenyekiti wa Chadema ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Hai na pia ni kiongozi wa Ukawa, Freeman Mbowe, hakupatikana jana kuzungumzia suala la kina Arfi kurejea bungeni.

PROFESA LIPUMBA
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema Ukawa wamejiwekea utaratibu wa kila chama kuwawajibisha wabunge wake ambao watakuwa wakikiuka maamuzi waliyojiwekea ya kutoshiriki vikao vya bunge la katiba linaloendelea mjini Dodoma.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Profesa Lipumba alisema Ukawa wamejiwekea utaratibu wa kila chama kudhibiti wabunge wake watakaokiuka maamuzi hayo.

“Mbunge wetu Mama Clara (Mwituka) yeye alionekana bungeni kabla ya Bunge kuanza. Siyo dhambi kwa mbunge kuonekana katika bunge hilo na hakuna zuio la nani awepo katika maeneo hayo ya bunge na nani asiwepo kwa hiyo yeye hakushiriki kikao chochote cha bunge hilo,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema watakaoonekana kushiriki vikao vya bunge hilo, kila chama kitakuwa na wajibu wa kuwawajibisha wabunge hao kama walivyokubaliana na kufikia muafaka wa kutoshiriki vikao hivyo.

Kuhusu fedha ambazo watalipwa wabunge hao kwa kila mjumbe zaidi ya Sh. milioni 20 kwa siku zote watakazokuwa kwenye bunge hilo, alisema hiyo siyo hoja ya kuwa kishawishi cha kuwafanya Ukawa kurejea bungeni.
Alisema yeye hilo haliofii kwani wabunge wa Ukawa hawakushiriki Bunge hilo kwa ajili ya kupata fedha bali kutetea katiba ya wananchi.

“Suala la fedha wanazolipwa haliwezi kuwa sababu ya vishawishi vya wabunge wa Ukawa kurudi bungeni. Hatukushiriki katika bunge hilo kwa ajili ya kupata posho bali kwa ajili ya kutetea maslahi ya wananchi. Hata suala la kupanga posho tulipwe kiasi gani hatukushiriki, hivyo siyo sababu ya msingi,” alisema Profesa Lipumba.

SITTA: UKAWA WATARUDI TU
Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, alisema ana uhakika wajumbe wanaounda Ukawa wataendelea kurudi bungeni mmoja baada ya mwingine.

Kauli hiyo aliitoa jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya maendeleo ya kamati za bunge hilo na pia kuwapo kwa ongezeko la wajumbe wa Ukawa wanaorejea, hasa baada ya kujisajili kwa kina Arfi jana.
“(Ukawa) wataongezeka tu... tunafahamu,” alisema Sitta
“Huku (kwenye) bunge maalum yanazungumzwa masuala yanayohusu wafugaji, unatoka kwenye wilaya ya wafugaji halafu wewe unasema mimi niligomea muundo kwa hiyo hata wafugaji siwatetei… nani atakuelewa?

“Tutakapoanza tarehe 2 Septemba mwaka huu mambo ya wananchi yataguswa, tutazungumzia ardhi, haki za binadamu na huyu anayegoma kwa sababu tu muundo anaoutaka yeye haujamridhisha ni ajabu kwa sababu sura 17 hazigusi muundo peke yake," aliongeza Sitta.

Alipoulizwa kama kuna mazungumzo yoyote na wajumbe wa Ukawa, Sitta alisema hana taarifa zozote za Ukawa kwani uongozi wa umoja huo ulikataa kuzungumza naye pamoja na kamati yake.

“Sisi walitugomea kabisa, hawataki kabisa kuzungumza na mimi (Sitta) wala kamati yoyote niliyonayo. Kwa hiyo mimi nasubiri kama kuna vyama vinaongea sijui, maana hata huko pia walikataa. Lakini nadhani kikubwa ni kwamba sisi tuliopo hapa ndani ya sheria tunaifuata sheria na katiba ilivyo,” alisema.

Kuhusu maendeleo ya kamati za bunge hilo, alisema wajumbe walipewa miongozo kwamba, wajadili kwa utaratibu kuanzia sura ya pili na kuendelea na ndivyo kamati zinavyofanya kwa sasa.

“Taarifa za awali tulizonazo ni kwamba, mijadala ni mizuri na ndivyo tulivyokuwa tunategemea kwa kweli kwa kuwa lengo hapa ni kuboresha tu hiyo Rasimu na ndiyo kazi wanayoifanya kwa sasa,” alisema Sitta.

Aliongeza: “Baada ya kupokea taarifa watakuwa na kikao na Katibu wa Bunge Maalum la Katiba na Makamu Mwenyekiti kwa hiyo nitakuwa na mambo mengi ya kusema na kuzungumza na waandishi wa habari.”

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Suluhu alisema: “La kufurahisha ni kwamba hata wale wenzetu ambao walitoka mwanzo lakini jana (juzi) tuliwakuta kwenye kamati,”

Imeandikwa na Jacqueline Massano na Godfrey Mushi (Dodoma) na Mary Geofrey (Dar).
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment