WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, August 17, 2012

YALIYOJILI OLIMPIKI 2012 TANZANIA TUMEVUNA TULICHOPANDA:



  • USHINDANI WA MICHEZO SIO SIASA NI UBUNIFU WA MAZOEZI NA KUJITUMA KWA WANAMICHEZO;


  • JE VIONGOZI NA WANAMICHEZO WANATUMIA KODI ZA WALALA HOI KWA AJILI YA KWENDA KUTEMBEA NA KUWASHANGILIA WENGINE?


  • KWA NINI NCHI NYINGINE ZA AFRIKA MASHARIKI ZIMEFANIKIWA NA SISI TUNAENDELEA KUBURUZA MKIA?


  • TUKIBADILISHA MSIMAMO NA MAWAZO FINYU OLIMPIKI YA 2016 TUNAWEZA KUSHINDA MEDALI NYINGI.


Rais wetu wa awamu ya Pili mzee wetu Ali Hassan Mwinyi aliwahi sema kuwa “Tanzania kwenye michezo ni sawa na kichwa cha mwendawazimu” kwa tafsiri rahisi ni kuwa Tanzania kwenye michezo ni  Ni aibu sana. Sawli ninaloendelea kujiuliza ni tatizo la viongozi, ubunifu wao umejaa kutu, au ni tatizo la serikali kuto kutoa kipau mbele kwenye michezo, au ni tatizo la wanamichezo wetu kutuzingatia maelekezo ya walimu wao na hali ngumu ya maisha yanayowazunguka?

Kama ni tatizo la viongozi kwa nini viongozi hao wasiachwe, na kama taifa  tuanze upya, kama mwana zuoni mmoja alivyosema “hakuna haja kuendelea kuwa wataliii na kutumbua pesa ya walalahoi kama posho ambazo wanazitumia wanashiriki masindano husika”


Tatizo la uozo na aibu ya kushindwa katika michezo ya kimataifa limedumu kwa muda mrefu sana kama mwandishi mmoja alivyowahi andika kuwa “Tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere hadi leo Tanzania ikiwa awamu ya nne, ni medali mbili tu za fedha”.

Lazima tukubali kuwa tupende tusipende  kama Thadeo alivyowahi sema kuwa “mwenendo wa michezo nchini siyo mzuri sana, kwani bado hatujafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, mwenendo sio mzuri kwa sasa, "

Je kushindwa kwetu kunachangiwa vile vile na ubinafsi wa viongozi wa michezo ambao wanafikiria zaidi faida binafsi na sio faida kwa taifa?

Tathimini ya mashindano ya olimpiki:

Michuano ya olimpiki ni michuano mikubwa kuliko yote duniani pamoja na kwamba ni mashindano yanayofanyika kila baada ya miaka minne, yakitoa nafasi kubwa kwa wadau kujiandaa,tumekuwa tukishikwa na kigugumizi kila mwaka kwani maandalizi yetu yamekuwa daima ni ya kuchechemea tu; Je, nini kinatukwaza? Yawezekana ni ukosefu wa mipango na kujituma katika kuitekeleza, tukiachia tu kila mmoja kwenye nyanja yake aoneshe nguvu zake. Je, katika wingi wa vipaji vilivyosambaa kote mikoani Bara na Visiwani, wanakosekana wanamichezo 100 wa kufuzu?


Uzuri wa Tanzania ni kwamba inavyo vitu vyote vya msingi kwa ajili ya maendeleo katika nyanja zote, michezo ikiwamo. Wapo watu waelewa wanaoweza kutoa uongozi mzuri na wamebarikiwa kwa rasilimali nyingi. Ili yote haya yafanikishwe lazima kuwe na dira ambayo inaweza tu kuwekwa Watanzania wakiwa na ndoto moja itakayowaongoza mwelekeo mmoja.

Mwandishi mmoja aliwahi sema kuwa Katika vijiji vingi Tanzania kuna vipaji vya ajabu kwenye michezo karibu yote 25 ya Olimpiki. Ni jinsi tu ya kuvikuza na kufungua fikra za wachezaji na kuwaingiza kwenye hali ya kisasa ya sayansi kiutandawazi. Katika Olimpiki hakuna michezo ya kutoka sayari nyingine, ni michezo ya kawaida tu – kuogelea, kulenga shahaba, soka ya wanawake na wanaume, tenisi, vishale, mpira wa pete, kikapu…yote inachezeka.
Mwanazuoni mmoja aliuliza kuwa ni katika msingi huo, naona kwamba kwa Filbert Bayi na Suleiman Nyambui kuiletea Tanzania medali za fedha kutoka Olimpiki, si tiketi ya wawili hao kuwa viongozi wa michezo. Medali za Olimpiki zitabaki ndoto ikiwa Tanzania haitasafisha nyumba yake – kwa wadau kuondoa woga, ubinafsi na kuacha kula vilivyotengwa kwa ajili ya watoto wa Olimpiki. Hakuna tena muda wa kupoteza, hivyo basi, ujenzi wa ndoto hiyo uanze sasa.

Anasema matayarisho mabovu ya wanariadha na ukosefu wa uongozi kutoka kwa mameneja katika mashirika ya michezo ndio sababu kubwa ya utendaji wa Tanzania wa kuvunja moyo katika michezo ya Olimpiki mwaka huu.

Anasema serikali ingechukua uongozi kutoka mashirika ya michezo, hata kama ni kwa muda, kama ilivyofanya kwa timu ya taifa ya mpira tangu mwaka 2007.

Maro alisema “mashirika ya michezo pia yanahitaji kupewa mafunzo ili kuwa na stadi zinazofaa za uendeshaji. "Uwezo wa viongozi wa mashirika ya michezo ni mdogo sana, aliiambia Sabahi. Wanaweza wakaweka rekodi za riadha na masumbwi, lakini hii haitoshi. Lazima wawe na uwezo wa kuandika mapendekezo ya gharama na kupanga michezo, badala ya kungojea serikali."

Kocha wa Riadha, Samwel Tupa analaumu maandalizi mabovu. Kwani hatukujua miaka minne iliyopita kuwa kuna Olimpiki mwaka huu? Umefika wakati wa kuingizwa watu wenye fikra mpya kwenye Kamati yetu ya Olimpiki. Haiwezekani, kwa ' Taifa Kubwa' kama letu kushindwa hata kufika fainali ya mchezo wowote kwenye Olimpiki. 


Kama mwariri wa gazeti la Tanzania Daima alivyowahi sema kuwa “ tukiwa miongoni mwa wadau wa maendeleo ya michezo nchini, tunasikitishwa na matokeo ya aibu kwa nchi yetu kwani tumeshindwa hata na nchi kama Libya na nyinginezo za Afrika ambazo muda mwingi, zimekuwa kwenye migogoro ya kisiasa.

Ni wakati sasa kwa serikali yetu kujifunza kutokana na makosa haya, kwani wakati nchi nyingi duniani zikiwekeza kwenye sekta ya michezo kwa vitendo, sisi viongozi wetu wamekuwa wakifanya hivyo kinadharia zaidi, hivyo kushindwa kung’ara kimataifa.

Wahenga walisema ‘kuvunjika kwa koleo, sio mwisho wa uhunzi’, hivyo kushindwa huku kuwe somo na chachu ya kujipanga zaidi kwa ajili ya mashindano mengine ya kimataifa, zikiwemo fainali zijazo za Olimpiki zitakazofanyika mwaka 2016.

Kwa kutumia mbinu, mikakati na mipango kama iliyotumiwa na mataifa jirani ya Kenya, Uganda, Ethiopia na Afrika Kusini yaliyopata medali huko London, kupitia wadau tutaweza kujiweka sehemu sahihi kimaandalizi kutung’arisha siku za usoni.


Serikali kupitia wizara husika, viongozi wa vyama vya michezo, wanamichezo, wadau na mashabiki kwa ujumla, kila mmoja achukulie matokeo ya kufanya kwetu vibaya kwa uchungu na kuamsha harakati mpya za kupata mafanikio siku zijazo. Tunaamini, hiyo ndio njia pekee itakayowezesha kufufua morali iliyokufa miongoni mwetu kufuatia matokeo hasi waliyopata wawakilishi wetu.”

Nakubaliana kabisa na mawazo ya mhariri wa Tanzania Daima kwa maoni yake mazuri lakini lazima tukubali kuwa “ kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi” lakini hii koleo yetu nafikiri imevunjika kiasi kwamba hatuwezi kuitengezeza kiurahisi. Kama taifa hivi sasa tunahitaji kusafisha wahunzi wa koleo yetu ya michezo wanaongoza kwa sasa. Nafikiri tunao masonara wazuri tu ambao hawajepatiwa nafasi ya kuonyesha ujuzi wao; lazima tukubali kuwa sasa ni wakati wa kusafisha nyumba yetu hebu tuanze na hii nyumba inayoitwa “TOC”;

Serikali inatakiwa kuandaa sera nzuri ya michezo 2016 olimpiki vison tukifanya hivyo nina imani kabisa kuwa tutaweza kuwa na timu nzuri ambayo itatuletea ushindi na medali mpaka ya dhahabu; tukiamua na tukianza kujisafisha na kugundua udhaifu wetu tutafanya vizuri zaidi ya Kenya, Uganda na Ethiopia.


Na nina imani kubwa kuwa waandishi wa michezo wananafasi kubwa ya kutelimisha na kutuonyesha mapungufu kama taifa katika swala nzima la michezo;  mabadiliko yeyote yale yatapatikana kama waatalamu wataweza kutufichulia udhaifu wa viongozi wanaohusika, wanamichezo wenyewe na Taifa kwa ujumla;

LAZIMA TUKUBALI KUKOSOLEWA KWA MANUFAA YA HESHIMA YA KIZAZI KIJACHO.

No comments:

Post a Comment