Ndugu zangu,
Kwa siku kadhaa nimekuwa nje ya mitandao. Hata magazeti, redio na televisheni zimenipitia kando. Jioni hii wakati nikipitia taarifa mbalimbali nimekutana na hili la hoja ya baadhi ya Waislamu kutaka sensa ya watu na makazi itakayofanyika kesho Jumapili igomewe kwa vile haina kipengele ama dodoso linalotaka kujua dini ya mtu.
Kabla sijatoa maoni yangu juu ya hilo ningependa niitafsiri dhana ya ‘ Kiumbe mzito’ kama tulivyoambiwa na wahenga wetu. Huenda si wengi kati yenu wasomaji wenye kufahamu maana hasa ya usemi wa Wahenga kuwa ‘ Kiumbe mzito’.
Ndio, Mwenyezi Mungu ametuumba wanadamu kwa usawa kwenye mambo mengi. Wala hakutaka kubagua; ona unyayo wa mwanadamu. U sawa, iwe kwa tajiri au masikini. Wewe na miye tumepata, ama wenyewe au kusikia mtu akilalamika kuwa soli ya kiatu chake imechakaa, kwamba anakwenda kwa fundi viatu kubadilisha soli. Lakini, wewe au miye hatujapata kumsikia mwanadamu mwenzetu akilalamika kuwa unyayo wake umechakaa, anataka kwenda kwa fundi awekewe unyayo mwingine!
Ndio, wewe na miye ama tumeshuhudia au kusikia kuwa upepo umeangusha mti, nyumba, ghorofa, gari na hata meli. Lakini, jiulize, je, umepata kumwona mwanadamu mwenzako anayetembea kwa miguu akiangushwa kwa upepo?
Binafsi hilo la mwanadamu kuangushwa na upepo sijapata kulisikia au kuliona kwa macho yangu. Mwanadamu hata awe mwembamba kiasi gani, haiyumkini akaangushwa kwa upepo. Na ukimwona mwanadamu mwenzako anaanguka barabarani, basi, ama ni mgonjwa, au ni mlevi. Na hilo la mwisho haliwezi kuwa na maana ya mwanadamu huyo kaangushwa na upepo, bali kaangushwa na pombe alizokunywa.
Naam, kiumbe mzito.
Na kesho ndio siku yenyewe ya Watanzania kuhesabiwa. Kuna wenzetu hususan kwenye Uislamu wenye kudai kuwa watagoma kuhesabiwa; Kisa? Hakuna dodoso lenye kutaka kujua dini ya mtu. Mimi naamini walioamua suala la dini ya Mtanzania lisiingizwe kwenye sensa walifanya uamuzi wa busara na wenye hekima sana.
Sisi ni Watanzania. Ni watu wamoja kwa asili. Na tujiulize kwanza; kwa nini tunahitaji kujihesabu. Ndio, sensa ina maana ya kujua idadi yetu kama Watanzania ili iisaidie Serikali katika kupanga mipango ya maendeleo ya nchi yetu. Mipango ya maendeleo ya nchi haibagui dini ya Mwananchi. Kama ni huduma ya maji, basi, maji hayo watakunywa Watanzania; wawe Waislamu, Wakristo, Wahindu au Wapagani. Hivyo hivyo kwa huduma nyingine muhimu za kijamii.
Bila shaka, Sensa ya watu na makazi ni mpango madhubuti wa Serikali kwa maendeleo ya watu wake na wenye kugharimu mabilioni ya shilingi. Si busara na hekima kwa baadhi ya viongozi wa madhehebu ya dini kushiriki kuhujumu mpango huu wa Serikali kwa manufaa ya wananchi wakiwamo waumini wa dini mbali mbali na hata wasio waumini. Na kubwa zaidi hapa ni ukweli huu; kuwa nchi yetu haina dini.
Naam, kiumbe mzito, hata kama Sensa ingeingiza kipengele cha dini, basi, wangetokea wachache wa kuhoji; iweje leo watu wakaulizwa dini zao, ama ni njama za kutaka kuwabagua na kuwakandamiza zaidi kimaendeleo Watanzania wa dini fulani au ni mbinu ya kutaka kudhibiti kuongezeka kwa idadi ya waumini wa dini fulani. Ndio, kuna ambao wangepambana kutaka kipengele cha dini kiondolewe na hata kutishia kugomea sensa.
Naam, kiumbe mzito, na mgumu pia!
Shime Watanzania na hususan ndugu zangu Waislamu, kesho ikifika na tuwe tayari kuhesabiwa kwa maendeleo ya nchi yetu. Kwa maendeleo yetu.
Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
No comments:
Post a Comment