Submitted by Mjengwa on 14.12.11
Ndugu zangu,
Ni dhahiri kauli ya Spika
Anne Makinda kuwa wabunge wanaongezewa posho kwa vile gharama ya maisha Dodoma
iko juu inaonyesha udhaifu walionao viongozi wetu wengi; kukosa uelewa wa hali
halisi.
Kiukweli, kwa kauli ile, Spika Anne Makinda alichemsha. Na ili tuelewe ni vema tukaingalia picha pana badala ya kipande cha picha. Tatizo hapa si Anne Makinda bali ni mfumo. Ndio, Anne Makinda ni kielelezo cha tatizo la kimfumo. Kwamba mfumo wetu, mbali ya udhaifu mwingine, unaowafanya viongozi wetu wawe ’ masultani’. Wakae kwenye nyadhifa za kisiasa na kiserikali kwa muda mrefu sana kiasi cha kupoteza uelewa wa hali halisi za wananchi wanaowaongoza.
Kwa mfano, tangu niko shule ya msingi nimelisikia jina la Anne Makinda katika nafasi za uongozi. Hivyo hivyo nimeyasikia majina ya akina Samwel Sitta, Malecela , Pius Msekwa na wengineo. Ndio, ni ukweli, kuwa nchi yetu ambayo asilimia kubwa ina raia vijana inaongozwa na wazee waliostahili kumpumzika na kuwaachia nafasi vijana.
Sina maana kuwa wazee hawana sifa za kuongoza, isipokuwa, tufanye sasa juhudi za makusudi za kuandaa mifumo itakayotufanya nafasi za uongozi zisishikiliwe kwa muda mrefu na watu hao hao. Tuanze sasa kufikiria kwa dhati kuandaa utaratibu wa kuwaandaa vijana ili waje kuwa viongozi bora. Vile vile, utaandae utaratibu utakaofanya Mbunge asikae bungeni zaidi ya vipindi viwili kwa maana ya miaka kumi.
Angalia sakata hili la wabunge na posho . Kwa hakika ni moja ya mambo ya kuhuzunisha yanayotufungia mwaka. Kwamba imefika mahali wabunge wetu wamefikiria kuongezewa posho kutoka shilingi elfu sabini hadi laki mbili kwa siku, tena katika wakati huu mgumu kiuchumi ambao mamilioni ya WaTanzania wanaupitia. Huu ni usaliti kwa nchi yetu na si kitu kingine.
Kwa Spika Anne Makinda , kama mwanadamu yumkini alighafirika. Ulimi hauna mfupa na hakuna mwanadamu asiye katika hatari ya kunena lililo baya masikioni mwa wanadamu wenzake. Spika Makinda hajachelewa. Atoke sasa, na kwa sauti yake mwenyewe, awaombe radhi WaTanzania. Akifanya hivyo atasamehewa. Maana atambue, ya kwamba kuwaambia WaTanzania maisha ya Dodoma kwa Wabunge ni ya gharama ya juu inatoa tafsiri mbaya.
Ni kauli mbaya maana Wabunge wetu ukilinganisha na mamilioni ya WaTanzania, hata bila posho ya shilingi hamsini kwa siku, bado watakuwa na maisha ya neema kubwa kuliko wapiga kura wao wengi. Yawezekana kabisa unavyosoma makala hii kuna mama MTanzania anayejifungua akiwa amelala sakafuni, au kuna mtoto wa KiTanzania anayekufa kwa malaria kwa vile zahati haina dawa. Ndio hali halisi. Huu ni wakati kwa viongozi wetu kuacha kuendekeza ubinafsi.
Viongozi wakiwamo Wabunge waanze sasa kuwafikiria wananchi ambao wengi wako katika hali mbaya kiuchumi. Ni wananchi hawa ambao miongoni mwao kuna wakulima. Ni wakulima hawa ambao posho ya laki mbili kwa siku kwa mbunge ingetosha kwa mkulima huyu kununua mbolea mifuko mitatu ya kilo hamsini kwa mfuko. Ni mbolea ya kupandia na kukuzuia kwa ekari moja. Tujiulize; tuko sasa kwenye ” Kilimo Kwanza au Wabunge Kwanza?”
Ndugu zangu, hii ni sehemu ya makala yangu ya juma hili kwenye gazeti la Raia Mwema. Nahitimisha.
Maggid,
Iringa.
Jumatano, Novemba 14, 2011
Habari hii kwa hisani ya Mjengwablogspot.com
No comments:
Post a Comment