Mganyizi Martin (kulia) wa Kagera Sugar, akimtoka
mlinzi wa Yanga , Nadir Haroub 'Cannavaro' wakati wa mechi yao ya ligi
kuu ya Tanzania Bara kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam
Haruna Niyonzima 'Fabregas' aliibeba Yanga kwa mara
nyingine baada ya kufunga goli 'kali' lililowapa ushindi wa 1-0 dhidi ya
Kagera Sugar katika mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.
Matokeo hayo yaliwaweka 'Wanajangwani' katika nafasi nzuri ya
kuelekea ubingwa baada ya kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi kwa
tofauti ya pointi sita dhidi ya Azam wanaowafuatia katika nafasi ya
pili.
Yanga wamefikisha pointi 42 baada ya kuteremka dimbani mara 18,
wakifuatiwa na Azam waliocheza idadi hiyo pia ya mechi. Mabingwa
watetezi, Simba, ambao walipata kipigo kisichotarajiwa cha bao 1-0
kutoka kwa Mtibwa Jumapili, wanaendelea kusuasua katika nafasi ya tatu
baada ya kufikisha pointi 34.
Niyonzima ambaye ndiye aliyefunga goli pekee pia lililowapa Yanga
ushindi wa 1-0 wakati walipocheza dhidi ya Azam Jumamosi, alifanya
juhudi binafsi kwa kuwatoka mabeki kadhaa wa Kagera na kutishia kutoa
pasi kabla ya kugeuka na kupiga shuti lililomshinda kipa Hannington na
kujaa wavuni katika dakika ya 66.
Goli hilo liliibua shangwe kubwa kutoka kwa mashabiki wa Yanga
ambao tayari walishaanza kuingiwa na hofu kutokana na kiwango cha cha
juu cha wapinzani wao kilichowapa 'jeuri' kutawala mechi hiyo katika
kipindi cha pili.
Mshambuliaji wa kimataifa kutoka Burundi, Didier Kavumbagu
aliikosesha Yanga kupata goli la utangulizi kwa njia ya penati katika
dakika ya 45 baada ya shuti lake kupaa juu ya lango.
Refa Simon Mberwa aliamuru ipigwe penati hiyo baada ya kipa wa
Kagera, Hannington kudaka mguu wa Kavumbagu wakati akijaribu kuokoa na
kipa huyo alionyeshwa kadi ya njano kwa kosa la kujaribu kupinga adhabu
hiyo na kutishia kutoka uwanjani kabla ya kurejeshwa na kocha wake
Abdallah Kibaden.
Katika dakika ya 49, Frank Domayo alipiga shuti kali lililompita
kipa wa Kagera na kugonga mwamba kabla ya mpira kurejea uwanjani.
Kagera walionyesha soka safi na kulishambulia zaidi lango la Yanga
katika kipindi cha pili lakini wenyeji walisimama imara na kuokoa hatari
kadhaa.
Said Bahanunzi alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumvuta jezi George Kavilla wa Kagera katika eneo la kati ya uwanja na Nadir
Haroub 'Cannavaro' alionyeshwa pia kadi ya njano katika dakika ya 82 baada ya kumkwatua Paul Ngwai aliyekuwa anaelekea kufunga.
Wachezaji Nizar Khalfan na David Luhende wa Yanga walifanya jumla
ya kadi zote za njano kwa klabu yao jana kufikia tano wakati
walipoadhibiwa wakiwa nje ya uwanja kwa kosa lililoonekana kuwa ni
kugomea maelekezo waliyopewa na refa wa mezani. Kadi hizo zilimaanisha
kuwa 'Wanajngwani' wajiandae kutozwa faini ya Sh. 500,000 kwa mujibu wa
kanuni za ligi kuu ya Bara kuhusiana na adhabu kwa timu inayopata kadi
za idadi hiyo katika mechi moja.
Baada ya mechi kumalizika, mashabiki wa Yanga waliojawa na furaha
waliliendea basi liliolowabeba wachezaji wao na kuimba huku
wakiwapongeza kwa kuwataja majina na kushangilia kwa kupuliza
'vuvuzela'.
Akizungumza jana, kocha wa Yanga, Mholanzi Ernst Brandts alisema
amefurahi timu yake kushinda kwani walicheza dhidi ya timu ngumu
iliyowafunga 1-0 katika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, hasa
ikizingatiwa kuwa wachezaji wake walikuwa wamechoka baada ya kucheza
mechi nyingine ngumu pia dhidi ya klabu ya Azam Jumamosi.
"Kiasi hatukucheza katika kiwango chetu kwa sababu wachezaji
walichoshwa na mechi iliyopita (dhidi ya Azam) iliyokuwa ngumu na
ushindani mkali," alisema Brandts.
Kocha wa Kagera, Abdallah Kibaden, aliwasifu wachezaji wake kwa
kucheza vizuri licha ya kuchoshwa na urefu wa safari ya kutoka kwao
Bukoba.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo jana, Ruvu Shooting
waliwashikilia wenyeji Coastal Union kwa sare ya 0-0 kwenye Uwanja wa
Mkwakwani jijini Tanga huku bao pekee lililofungwa na Nahoda Bakari
katika dakika ya 51 likiwapa Polisi Morogoro ushindi wa 1-0 dhidi ya
Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Jamhuri na Mtibwa walishindwa kufungana na
Prisons kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani Morogoro.
Vikosi:
Yanga:- Mustafa Barthez,Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub
'Cannavaro', Kelvin Yondani, Athumani Iddi 'Chuji', Simon Msuva, Frank
Domayo, Didier Kavumbagu/Hamis Kiiza (dk.60), Said Bahanunzi/Jerry
Tegete (dk.68), Haruna Niyonzima.
Kagera:-Hannington Kalyesubula, Benjamin Asukile, Muganyizi Martin,
Malgesi Mwangwa, Amandus Nesta, George Kavilla, Julius Mrope/Paul Ngwai
(dk.62), Juma Nade, Darlington Enyinna, Shija Mkina, Daud Jumanne.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment