NIMEKUWA nikisema, na sijachoka kusema, kwamba tunatakiwa kujenga taifa kubwa, na nimekuwa nikisisitiza kuhusu sifa za taifa la aina hiyo, sifa zinazotofautisha baina ya nchi kubwa yenye taifa dogo ndani yake na nchi ndogo yenye taifa kubwa ndani yake.
Sifa hizo ni nyingi, baadhi zikiwa ni kubwa na nyingine zikiwa ni ndogo, nami nimekuwa nikizijadili, pamoja na kujadili sifa zinazofanya taifa kuwa dogo hata pale linapokuwa ndani ya nchi kubwa, kama Kongo mathalan. Sifa moja inayoifanya nchi yo yote isiweze kujenga taifa kubwa, hata kama nchi yenyewe ni kubwa kama Kongo, ni uroho wa watu wake na watawala wake.
Haitawezekana aslani kwa nchi yo yote, hata ingekuwa kubwa kiasi gani na ikawa na utajiri wa El Dorado, kujenga taifa kubwa iwapo watu wake na watawala wake ni waroho, walafi, waporaji, wanyang’anyi, waongo, wanafiki na mabazazi. Kila nchi ina watu wa aina hii, na ni haki ya kila nchi na kila taifa kuwa nao, lakini wakiwa ndio wengi zaidi kuliko watu wema nchi hiyo haiendi ko kote.
Nimesema pia kwamba nchi inayotarajia kujenga taifa kubwa haina budi kujenga misingi ya haki, usawa, mshikamano na upendo, tabia ya kujuliana hali na kusaidiana inapotokea shida, na pia uwezo wa kujua namna ya kugawana kile kinachopatikana kama riziki ya taifa bila kunyang’anyana kila kakipatikana kanyama kadogo.
Zogo linaloendelea kuhusu gesi asilia nchini linadhihirisha kwamba hatuna nia ya kujenga tafia kubwa na badala yake tumejifunga katika udogo wetu wa siku zote. Tunapoteza akali, mantiki inayeyuka, staha inatutoroka, adala inatuacha, na haya zinatuishia kwa sababu ya kanyama kadogo kama gesi asilia. Najiuliza, hali itakuwa vipi iwapo tutalaaniwa na kupata vitu vikubwa zaidi? Si tutamalizana?
Miongoni mwa sababu zinazotufanya kuwa taifa dogo ndani ya nchi kubwa ni nakisi ya utashi wa kujifunza kutokana na yale yaliyo ndani ya uwezo wetu kujifunza. Tumezungukwa na nchi zenye utajiri mkubwa ambao unawafanya wananchi wake na watawala wake waparurane, wakwaruzane, wachinjane kwa sababu ya utajiri huo. Sisi tunakataa kujifunza kutoka kwao, kana kwamba tunatamani tuwe kama wao.
Tunajua kwamba nchi hizo, pamoja na utajri mkubwa wa maliasili, ni nchi zenye wananchi mafukara kama Lazaro, na kwamba ufukara huo katikati ya utajiri mkubwa ndiyo kichocheo kikubwa cha uhasama na vita, lakini na sisi tunataka kwenda huko huko.
Tumeona kwamba wananchi wanapokuwa wamechoshwa na viongozi waroho wataasi tu, hata kama majeshi yatasambazwa katika kila kijiji na kila mtaa, nasi tunataka kwenda huko huko.
Aidha tumeona, na tunajua kwa sababu hili tumeliona mara kadhaa, kwamba suluhisho la matatizo yetu ni mazungumzo ya kutafuta maelewano, lakini tunaendelea kuamini kwamba tunaweza kumaliza matatizo yetu kwa matumizi ya nguvu, hasa pale inapotumika dhidi ya wananchi wasio na silaha. Tumeingia katika zahma kubwa, zahma isiyo ya lazima, kwa sababu tu tunakataa kufikiri kidogo na kuchukua hatua za kusawazisha mambo kabla hayajawa makubwa.
Mzozo kuhusu gesi na maliasili nyingine si jambo jipya kwa wale wanaojisumbua kuangalia nchi za wenzetu na kusoma na kuielewa historia ya dunia.Tatizo kubwa ni uongozi katika ngazi zote kutokuwa na umakini unaohitajika kukabiliana na changamoto zinazotokana na hii laana tunayokumbana nayo tunapopata neema ya kugundua utajiri.
Imefikia hatua kwamba wanadiplomasia wa nje nao wanatutanabahisha kuhusu maliasili na jinsi ya kuzishughulikia, kana kwamba sisi wenye hatujui nini tufanye. Namsikia balozi akituambia, “Hey, nyie, tahadharini na gesi na mafuta; vitu hivi ni hatari kwa watu kama nyie kwa sababu hamjakaa vizuri; vitawaumizeni!” Hii ni lazima kwa nchi yenye umri wa miaka hamsini u shey?
Tunaijua Angola? Tunaijua Nigeria? Tunazijua Kongo zote mbili? Tunaijua Nigeria? Tunaijua Equatorial Guinea? Tunaijua Gabon? Tunaijua Libya? Nini tumejifunza huko kote? Hekima inatufundisha kwamba ni vyema kujifunza kutokana na makosa yaliyopita… siyo makosa yako, bali makosa ya wengine, kwani ukisubiri kujifunza kutokana na makosa yako mwenyewe, gharama zake zitakuwa kubwa mno.
Wakuu wa serikali, wakuu wa siasa, mashirika mbali mbali na wananchi kwa ujumla, sote tunahitaji kutulizana na kufanya tafakuri ya lazima. Nilipodokeza kwamba mchakato wa ‘Katiba Mpya’ unaoendelea sasa ulikosewa kwa sababu ni sawa na kutanguliza mkokoteni mbele ya punda, inawezekana sikueleweka, lakini sasa tunaona athari zake.
Wakati ule nilisema kwamba kuna haja ya mjadala mkuu wa kitaifa ili kuweka misingi ya maelewano ya kitaifa kuhusu mustakabali wa nchi yetu. Hii ni rai niliyoitetea tangu wakati Rais Benjamin Mkapa alipoingia madarakani mwaka 1995. Mara kadhaa nilisisitiza kwamba taifa letu limepoteza mwelekeo na linahitaji kuketi na kujitafuta. Bila shaka kwa nia njema, Mkapa hakuiona mantiki hiyo.
Niliirejea rai hii Rais Jakaya Kikwete alipoingia madarakani, katika Barua Ndefu ya Wazi kwake (sikuzungumza naye ana kwa ana jinsi nilivyozungumza na Mkapa), lakini naye hajaliona hili, na badala yake ameanzisha mchakato wa kupata ‘Katiba Mpya.’
Bado nasisitiza kwamba hatujajiweka sawa, hatujatulizana, hatujaelewana na hatujaridhiana na hatujaafikiana. Mengi tunayoyafanya tunayafanya kwa kupuyanga, alimradi liende, ilhali tukijua kwamba haliendi. Uwezekano wa kuumia huko tuendako ni mkubwa mno, hususan iwapo tutapata bahati mbaya ya kulaaniwa kwa mkosi wa kugundua mafuta ya petroli.
source: Raia mwema:Jenerali Ulimwengu
No comments:
Post a Comment