Jibu limepatikana: Walisubiri Padri auawe?
SERIKALI haina utetezi wa kutosha dhidi ya tuhuma kuwa inahusika na machafuko ya kidini yanayoshika kasi nchini pote.
Unahitaji kuwa na akili za “mwenda wazimu” kudiriki hata kuitetea serikali dhidi ya malalamiko haya. Sababu zinazoinyima utetezi ni hizi hapa:
Kwanza, serikali “inaposhindwa” kuwakamata wauaji, tafsiri rasmi ni kuwa ndiyo iliyohusika na kwa hiyo haiwezi kujikamata. Pili, uhai wa wananchi unalindwa na serikali kwa mujibu wa katiba yetu na kwa hiyo, kudai kuwa wananchi wajilinde si sawa. Tatu, tahadhari nyingi zilitolewa huko nyuma kuhusu vitisho vya kuwaua viongozi wa dini, lakini serikali ilikaa kimya au kuamua kuwalinda wachache ambao ina maslahi mapana nao. Tujikumbushe mifano michache ya tahadhari hizo.
Oktoba mwaka jana (2012), maaskofu wa KKKT walisema haya:
Tumeshuhudia wizara zetu zikivamiwa mchana kweupe na kushinikiza kuachiwa kwa watuhumiwa wa uhalifu; tumeshuhudia vituo vya polisi vikichomwa moto; mahakama zikilazimishwa kufunga shughuli zake, misikiti ikitekwa, uhai wa viongozi wa dini ukitishiwa hadharani na viongozi wastaafu wakizabwa vibao hadharani kwa sababu zinazoitwa harakati za kidini. Tumefikia kuhoji, watu hawa wavamie nini ndipo hatua zichukuliwe?
Wachome nini ndipo viongozi wenye dhamana ya kulinda mali na uhai washtuke?Wamwue nani ndipo iaminike kuwa watu hawa ni tishio kwa usalama wa taifa letu?
Vitendo vya raia kuuawa wakiwa mikononi mwa polisi vimezidi kuongezeka. Matukio ya viongozi kujeruhiwa au kuuawa pia yameongezeka.
Aliuawa Mchungaji mmoja huko Mto wa Mbu, baadaye akapigwa risasi padre huko Zanzibar, ikafuatia hatua ya kumwua Mchungaji mmoja huko Buseresere-Geita. Katika matukio hayo yote, serikali haikushtuka kama ilivyoshtuka kwa kifo cha Padre Evarist Mushi. Maaskofu walipohoji ni nani auawe ili serikali ishtuke, kwa sasa ni kama wamejibiwa kuwa walikuwa wanasubiri hiki kifo cha Padre Mushi.
Wakati haya yakiendelea kutokea, wenye hekima walionya na hata bungeni wapo waliosimama kudai Jeshi la Polisi liundwe upya. Walipuuzwa na kuendelea kuumwagia sifa kemkem, uongozi wa Jeshi la Polisi. Hata vyombo vingine vya usalama hapa nchini vimekuwa kwenye kikaango cha lawama za wananchi kuwa havina weledi wala umakini wa kutosha.
Hawakusikilizwa. Inashangaza sasa, baada ya Padre Evarist Mushi kuuawa, ndani ya saa chache, serikali iliagiza waletwe majasusi toka nje ili kuchunguza tukio hilo. Hivi kweli, walisubiri padre auawe ndipo wajue pana haja ya kuchukua hatua?
Hivi ni mpaka aseme Rais ndipo wahalifu watakamatwa ndani ya muda mfupi? Mbona wauaji wengine mpaka sasa hatujaambiwa wako wapi?
Vyombo vya habari viliandika mfululizo mwishoni mwa mwaka jana juu ya mpango wa kundi fulani kumdhuru au kumwua kiongozi wa juu ya dini ya Kiislam hapa nchini. Iliandikwa baadaye kuwa serikali imeweka ulinzi wa kutosha ili kuhakikisha yuko salama.
Taarifa za uchochezi unaoenezwa kwa njia ya kanda za video, CD na DVD zimelalamikiwa mara nyingi. Katika tamko la Jukwaa la Wakristo lililotolewa katika Sikukuu za Krismas, mwaka jana, uchochezi huu ulilalamikiwa. Kwa vipimo vya serikali, waliona bado huo uchochezi hautoshi kuondoa amani ya nchi.
Vinara wa uchochezi huo wanaonekana na kusikika wakiagiza waumini kuwa ni ruksa kumwua kiongozi wa dini kama kardinali, askofu, padre na mchungaji. Uhai wa viongozi wanaotajwa umefanywa kuwa kitu chepesi mdomoni mwa mtoa amri. Wakati makamanda wa vyombo vya dola wanasita kutoa amri ya kumpiga mwizi au mbakaji, hapa tuna watu wanatoa amri kwa waumini wawaue viongozi wa kijamii. Hatari ya matamshi yao kwa sasa haiko katika utekelezaji wa amri zao bali katika kusitasita kwa serikali kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria.
Kuna hoja mbili muhimu ambazo wachochezi hawa wanazitumia kujenga sababu ya kuwaua viongozi wa kikiristo. Kwa Tanzania Bara ni hicho kinachoitwa “Mfumo Kristo”na kwa Tanzania Visiwani ni kupinga “ukafiri” ndani ya Visiwa hivyo vitakatifu.
Hata kwa hoja hizi mbili, bado hatari haiko katika utoaji wa hoja, bali katika kimya cha serikali kuhusu madai haya.
Madai ya kuwapo kwa “mfumo Kristo” katika serikali isiyo na dini ni hoja nyepesi mno. Lakini pamoja na wepesi wake, ina haki ya kujibiwa na watawala wetu waliochaguliwa ili kuelimisha umma juu ya kero zao.
Matokeo ya kutokujibu hoja hizi, ndipo linakuja suala la watu kudhani wanaweza kuuondoa mfumo Kristo kwa njia ya panga na risasi. Na wale wanaopinga ukafikiri wanadhani njia sahihi ya kuondoa ukafiri ni kwa kutumia panga, moto na risasi.
Matumizi ya nguvu ili kuondoa kitu kinachoitwa mfumo (system) ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu. Kitu kikiitwa mfumo ina maana kimeingia hapo kilipo kwa utaratibu fulani, sera fulani, mipango fulani ya muda mrefu na mfupi, na mikakati endelevu isiyo ya zima moto.
Kwa mifumo yote miwili inayopingwa Bara na Visiwani (Mfumo-Kristo na Ukafiri), ni uendawazimu kwa mtu kudhani anaweza kuiondosha kwa panga na risasi. Uzoefu unaonyesha kuwa njia za nguvu na vurugu huifanya mifumo ijiimarishe zaidi kwa sababu, zaidi ya yote, mifumo ya namna hiyo ni ya kiimani zaidi kuliko uhalisia.
Mateso, mauaji, na ubaguzi wa kidini huzifanya zile dini zinazobaguliwa zijiimarishe zaidi. Kupinga dini ya mtu ni sawa na kumwamuru aile kama chakula, ainywe kama maji kuliko alivyokuwa anafanya kabla hajapingwa. Kwa ujinga huu wa kupinga mfumo Kristo usiokuwapo, kuna hatari huko mbele kuufanya uwepo rasmi au kwa fikra.
Katika serikali na dola zote za kidini ulimwenguni, hakuna dola isiyojuta kwa hatua yake ya kuunganisha serikali na dini. Ziwe serikali za kikiristo au za kiislamu, zote zinajuta kwa sababu katika ndoa bandia hiyo kati ya dini na serikali, wote wanakosa uhuru kamili wa kufanya mambo yao.
Ndiyo maana hivi sasa, nchi nyingi zilizokuwa za Kikristo ama zimeachana na mfumo na kuyaachia makanisa yawe huru au zimo njiani kuachana nayo. Hata katika falme na dola za Kiislamu, upo mnyukano mkali juu ya dini kujiondoa katika kufungamana na serikali zao kwa sababu kila wakati serikali zinazidi kuwa za kisekura (secular) na dini zingependa kuwa za kihafidhina.
Lakini ukiwaangalia wanazuoni wetu – Wakristo na Waislam, hutaacha kugundua kuwa, dhana zinazoitwa “mfumo Kristo”, “ukafiri” au “udini” zinapewa maana nyepesi sana.
Picha wanayotoa kama kiashiria cha kuwapo kwa mfumo huo, ni idadi ya watu walio katika nafasi fulani tu. Mtizamo wao huo ndio unaoelekea kusababisha machafuko hapa nchini kwa sababu watu wanajengewa fikra kuwa waumini wa dini fulani walio katika nafasi hizo, wanatekeleza matakwa ya dini zao.
Kimsingi, dini yoyote itakuwa inajidanganya kufikiri inaweza kusaidiwa na serikali kupata waumini au kugawa sakramenti. Dini ya kweli ni ile inayotamani uhuru wa kuondokana na mikataba ya serikali na serikali ya kweli ni ile inayotamani dini ziwe mbali nayo katika utendaji wake wa kazi.
Tumefikaje hapa? Hakuna haja ya kujiuliza kwa sababu tumeishafika. Tunaondokaje hapa? Hilo ni gumu, lakini tukijua waliotufikisha hapa itasaidia. Ni ama waturudishe tulikotoka au tuondokane nao, turudi wenyewe.
Maaskofu walionya Ijumaa kule Arusha kwenye maziko ya Askofu Laizer. Jumapili asubuhi padre akauawa. Watawala wetu wanakimbilia kuagiza majasusi kutoka nje ili waje kuchunguza. Hili nalo jepesi sana. Unapoagiza majasusi kutoka nje, ni tangazo kwa majasusi wako kuwa wao ni magaidi si majasusi tena.
Source: Raia Mwema
No comments:
Post a Comment