WIKI iliyopita niliandika kuhimiza
uchapaji kazi nchini, na kusema kwamba maendeleo haya ambayo CCM na serikali
yake wanayatambia hivi sasa yana walakini, kwa sababu, kwa kiasi kikubwa,
hayatokani na uchapaji kazi wetu mkubwa; bali ukopaji wetu mkubwa.
Nataka kuuendeleza kidogo mjadala huu
kwa sababu kiwewe hiki cha kukopa cha Serikali ya Rais Kikwete hadi kwenye
mabenki ya biashara na mashirika ya hifadhi za jamii nchini, kisipodhibitiwa
kitatuletea madhara makubwa huko mbele ya safari.
Wiki iliyopita nilipendekeza tuidhibiti
hali hii kwa Bunge kuweka ukomo wa ukopaji (debt ceiling); yaani kiwango
fulani kikishafikiwa hakuna tena kukopa mpaka madeni yaliyopo yapunguzwe kwanza
hata kwa asilimia 50. Nadhani nilieleweka.
Msingi wa hoja yangu ni kwamba
maendeleo yaliyokamilika na ya kujivunia ni yale yanayotokana na uchapaji kazi
wetu katika kila sekta ya uzalishaji nchini kuanzia kilimo vijijini hadi kwenye
viwanda, maofisini, sekta za utalii, madini nk.
Hatma ya uchapaji kazi huo ni kukua kwa
uchumi wetu, hali ambayo inatuweka katika mazingira mazuri ya kujiletea wenyewe
maendeleo tunayoyahitaji – iwe ni uboreshaji miundombinu, ujenzi wa viwanda,
uboreshaji huduma za afya, elimu nk.
Japo mimi si mchumi, sihitaji kuwa
mchumi kuelewa kwamba kama tutachapa kazi zaidi sekta ya utalii nk na kuzalisha
zaidi katika kilimo na viwandani, na hapo hapo tukatoza kodi stahiki makampuni
ya madini na mengine makubwa nchini, tukakomesha ufisadi, na pia tukapunguza
matumizi ya serikali na hasa ukubwa wake, tunaweza kujiletea wenyewe maendeleo
tunayoyahitaji bila Serikali kulazimika kukopa sana nje au kukopa sana mabenki
ya kibiashara hapa nchini na hata kwenye asasi za hifadhi ya jamii.
Lakini kwa sababu tumeacha kuchapa
kazi, na kwa sababu viongozi wetu wameacha kabisa kuzunguka nchini kuhimiza
uchapaji kazi, kidogo kidogo tumegeuka taifa la wavivu - taifa linalotegemea
misaada na pesa za kukopa kujiletea haya tunayoambiwa na CCM kuwa ni “maendeleo
makubwa”.
Kwa sababu ya utamaduni huu wa uvivu
tulioukumbatia, watawala wanalikimbia tatizo kwa kutegemea mikopo ya ndani na
nje ya nchi kuendesha nchi. Na ndiyo maana ndani ya kipindi cha miaka mitano
tu, Serikali ya Kikwete imeongeza deni la Taifa kutoka Sh. trilioni 6 hadi Sh.
trilioni 21!
Ni hoja yangu kwamba kama tunataka
maendeleo ya kweli na ya kujivunia, hatuna budi kuujenga upya utamaduni wa
kuchapa kazi na kuuvunjilia mbali utamaduni wa uvivu ambao umeanza kutamalaki
nchini.
Binafsi, sikumbuki mara ya mwisho
kumsikia Rais Kikwete au Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakitoa hotuba za kuhimiza
uchapaji kazi nchini kwa namna ile walivyofanya Nyerere na Sokoine. Ni nadra
kuwasikia watawala wetu wa sasa wakihimza uchapaji kazi kwa wakulima vijijini
au kwa wafanyakazi viwandani au hata maofisini!
Na ma-DC wao wengi huko wilayani
ni hivyo hivyo. Wanaochapa kazi ni wachache mno. Wengi hawaonekani vijijini.
Kutwa nzima wako maofisini wakipanga namna ya kutumia vyeo vyao vipya
kujitajirisha. Kama wakienda vijijini ni pale tu wanapopokea taarifa za
migogoro inayotishia amani.
Kwa hakika, tangu Mwalimu Nyerere
anga’atuke madarakani na baadaye kufariki, suala la watawala wetu kuhimiza
uchapaji kazi nchini ‘limefariki’ naye!
Sasa niambieni:Ni taifa gani duniani
ambalo linaendelea kwa kasi kwa sababu ya kukopa na kukopa zaidi na si kwa
sababu ya uchapaji kazi uliotukuka? Si zile nchi za Mashariki ya Mbali
zinazoitwa Asian Tigers na wala si India au Brazil.
Katika uvivu wetu huu ambao Watanzania
tunaogelea nao, tunazungukwa na kuishi na matatizo; lakini hatuchukui hatua yo
yote ya kujaribu kuyatatua mpaka aje mgeni (Mzungu) atuonyeshe namna ya
kuyatatua, hata kama tulikuwa tunajua namna ya kuyatatua.
Saratani hii ya utegemezi wa mikopo na
wafadhili (dependency syndrome) – kwa fikra, mawazo na hata kwa matendo,
inaanzia serikalini. Zaidi ya asilimia 40 ya bajeti yetu ni pesa za wafadhili.
Sehemu kubwa ya miradi mikubwa ya maendeleo inayoendelea nchini ni mikopo
ya vyombo vya fedha vya nje na vya ndani. Zaidi ya asilimia 50 ya mipango yetu
ya maendeleo inaanzia kwanza kwenye fikra za kukopa nje na ndani ya nchi, na si
kwenye pesa zetu wenyewe.
Tumefika mahali sasa tumeanza kuamini
kuwa kazi ya rais kuongoza nchi sasa inarahisishwa na uhodari wake wa kukopa. Anayependwa
na wafadhili ndiye tunayemtaka awe rais wetu kwa sababu tunajua kuwa itakuwa
rahisi kwetu kukopeshwa na mataifa makubwa atakayoyafuata kuomba mikopo au
misaada!
Ilivyo sasa, tumeaminishwa kuwa
anayehitajiwa si rais mchapakazi na mbunifu, bali ni yule anayewasikiliza
wafadhili na anayekubaliwa na wafadhili. Ni yule ambaye ni hodari wa kutembeza
bakuli la omba omba Ughaibuni kabla ya kikao cha bajeti cha bunge letu!
Hatuna maadili yetu wenyewe. Hatuna
dira yetu wenyewe. Hatuna mipango yetu wenyewe ya maendeleo isiyo na mkono wa
wafadhili au wa mkopeshaji iwe ni IMF, World Bank, Exim Bank ya China au NSSF
ya hapa nyumbani nk!
Hali hii ya kutegemea mikopo ya nje na
ya ndani ya nchi kwa karibu kila mradi mkubwa wa maendeleo nchini imeua kabisa
ule moyo wa kufikiri, kubuni, kuchacharika wa viongozi wetu. Imeua ule moyo wa
kujitegemea uliojengwa katika kipindi cha utawala wa Mwalimu Nyerere.
Hali hii ya utegemezi kwa kila kitu
imewalemaza na kuwabwetesha si tu viongozi wetu, lakini hata na sisi wananchi
wa kawaida. Kule kwetu Upare kulikuwa na utaratibu wa kazi za kujiletea
maendeleo ulioitwa Msaragambo ambao Wapare tuliurithi kutoka kwa mababu
zetu. Zama hizo, kila tatizo la kijiji lililowagusa wanavijiji wote
lilishughulikiwa kwa pamoja kwa njia ya Msaragambo.
Kama ni kuharibika kwa barabara au
mfereji mkubwa unaotumika kwa kilimo cha umwagiliaji, basi, ilipigwa mbiu na
wanavijiji walijitokeza kukalafati mfereji huo kwa njia ya Msaragambo.
Asiyejitokeza alipigwa faini ya pesa kidogo au vitu kama vile kuku au mbuzi!
Lakini sasa Msaragambo na
matumizi ya nguvukazi ya wanavijiji kutatua matatizo yao wenyewe, hakuna
tena Upareni. Kinachosubiriwa ni pesa za Halmashauri au za wafadhili au pesa za
mkopo!
Zamani utegemezi wa pesa za Wazungu au
za Halmashauri kwa kazi ambazo wanavijiji wenyewe walimudu kuzifanya haukuwepo
hata kidogo. Leo hii, hata kujenga choo tunasubiri pesa za wafadhili au za
mkopo! Hata kufukia madimbwi ya maji ambayo ni mazalio ya mbu wanaosababisha
malaria, tunasubiri tufanyiwe na wengine.
Miaka kadhaa iliyopita niliwahi
kutembelea kijiji kimoja cha wilaya moja ya mkoa wa Tabora ambako nilitembezwa
katika bwawa la mfano la kufugia samaki lililojengwa kijijini humo kwa pesa za
wafadhili (Wazungu)!
Katika hali iliyonishangaza kabisa,
wenyeji wetu waliona fahari kutuonyesha bwawa la kawaida kabisa lililojengwa
kutokana na fedha za wafadhili! Hii maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba
tumekuwa mazezeta tusiofanya lolote kujisaidia wenyewe mpaka waje Wazungu
kutufanyia hata mambo tunayomudu kuyafanya sisi wenyewe.
Sasa, ungetaraji watawala wetu
wangehaha kuuzima moto huu wa dependency syndrome usisambae kwa kasi
nchini kwa kutembea kote nchini kuhimiza uchapaji kazi na kuhubiri juu ya manufaa
ya dhana ya kujitegemea. Je; ndivyo wanavyofanya?
Jibu langu ni hapana. Na hawawezi
kufanya hivyo kwa sababu wao wenyewe ni waumini wakubwa wa maendeleo
yanayotokana na fedha za mikopo, na ndiyo maana miaka mitano tu deni la Taifa
limeruka kutoka Sh. trilionji 6 hadi Sh. trilioni 21!
Mtunzi maarufu wa vitabu wa Nigeria,
Chinua Achebe, akizungumzia hali ya mambo ilivyo katika nchi yake na katika
nchi nyingine za Afrika, alipata kunukuliwa akisema: “We have to begin to
learn to rule ourselves again” ; yaani: tunapaswa kuanza kujifunza namna ya
kujitawala wenyewe tena” (tafsiri ni yangu).
Naamini Achebe hakukosea kusema hivyo,
na naamini pia kwamba nasi Tanzania tunapaswa kuanza kujifunza upya kujitawala;
maana yaelekea baada ya Nyerere kufariki tumesahau namna ya kujitawala.
Vinginevyo tusingejivunia mno maendeleo
yanayotokana na pesa za kukopa na kukopa zaidi hata kutoka katika asasi za
hifadhi za jamii zinakotunzwa pesa za masikini wastaafu wetu!
Tafakari.
Source:
Raia Mwema: Johnson Mbwambo
No comments:
Post a Comment