Ndugu zangu,
Jioni yote ya jana nilikuwa nimepumzika kujisomea tu, hata taarifa ya habari ilinipita.Nilipoingia mtandaoni nikakutana na habari hii ya kusikitisha; matokeo mabaya ya kidato cha nne!
Namkumbuka jamaa yangu aliyeniuliza; " Maggid, unatarajia nini pale unapoona mwalimu anahonga ili apewe nafasi ya kwenda kusahihisha mitihani?" Kioja hiki!
Nakumbuka pia miaka kadhaa iliyopita. Mzazi kule Musoma alikwenda kulalamika kwa Mwalimu Mkuu aliposikia mtoto wake amefaulu mtihani wa darasa la saba na amechaguliwa kujiunga na Sekondari. Mzazi yule akauliza kwa kushangaa; " Hivi aliyefaulu ni mtoto wangu huyu huyu ambaye mpaka hii leo hajui vema kusoma na kuandika?"- Kioja!
Na nimeona, kwenye matokeo yaliyotoka hii leo, kuwa kwenye shule iliyopewa jina la Sekondari ya J. M. Kikwete wanafunzi wote wamefeli! Kioja hiki!
Tunajifunza nini?
Tuna MGOGORO WA ELIMU- Education Crisis. Ni mgogoro wa kitaifa. Tuna lazima ya kutafuta suluhu ya pamoja kama taifa. Hapa si mahala pa kutanguliza siasa za vyama. Inahusu taifa letu na mustakabali wake.
Hivi tunajua? Kuwa umejengeka mfumo sasa wenye kuashiria kuwa kuna ' Ubaguzi wa Kielimu'. Kwamba matokeo haya mabaya ya Form Four yanawahusu zaidi watoto wa makabwela na kwenye shule za makabwela.
Ni matokeo ya Serikali kutowekeza rasilimali nyingi kwenye shule za Msingi na Sekondari za umma ( Public
Kuna tunaokumbuka, kuwa enzi zile, sisi tuliosoma kwenye Sekondari za Serikali, ndio tulioonekana kupata bahati ya kwenda kwenye shule zilizo bora kuliko zile za binafsi. Ni kwa sababu, mfumo wetu wa elimu haukuwa wa kibaguzi. Kwamba darasa la shule ya msingi niliyosoma mimi pale Kinondoni , alisoma pia mtoto wa Waziri wa Maji, Gwassa Sebabili.
Sekondari ya Tambaza niliyosoma mimi alisoma pia mtoto wa Mzee Ali Hassan Mwinyi, huyu huyu Dr. Hussein Mwinyi. Hivyo, Baraza la Mawaziri lilipokutana na kuzungumzia matatizo ya elimu, kimsingi walizungumzia matatizo ya elimu ya watoto wao katika shule ambazo watoto wao wamechanganyika na watoto wa makabwela.
Leo hii kama kwenye Baraza la Mawaziri atatokea Waziri atakayezungumzia matatizo ya shule ya Sekondari ya Kata anayesoma mwanawe pale Makumbusho, basi, kuna wenzake watakaomwangalia kwa mshangao, na kujiuliza pia; " Hivi huyu Mheshimiwa ameshindwa kumpeleka mwanawe hata pale Sekondari ya Saint nanihii!"
Naam, tunachokiona sasa ni kichuguu cha tatizo, mlima wenyewe hatujaufikia.
NI SIKU YA KUSIKITISHA SANA. ( Picha hiyo juu niliipiga shule ya msingi Ikuvala, Kilolo, Iringa, miaka kadhaa iliyopita)
Maggid Mjengwa,
Iringa
0788 111 765
No comments:
Post a Comment