·
Rafu za mtandao zawakutanisha Salim, Mangula
KUUNDWA
kwa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2015 ni pigo jipya kwa watu wanaotajwa kuweza kuwania nafasi ya kuteuliwa
kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Raia Mwema, limebaini.
Taarifa
zinasema fursa ya kujieleza mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ilikuwa
ni kete nyingine kwa wagombea hao watarajiwa, Samuel Sitta, Edward Lowassa na
Benard Membe kuomba kura za wajumbe ili wachaguliwe kuwa wajumbe wa Kamati Kuu
kama majina yao yangepenedezwa na Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete.
Inaelezwa
kuwa ingefahamika mgombea yupi mtarajiwa kati yao ana ushawishi wa kura za NEC
yenye wajumbe ambao ndio hao hao watakaopitisha majina ya wagombea urais kwenda
Mkutano Mkuu 2015.
Hadi
sasa, kati ya wanaotajwa ni Membe pekee ndiye aliyejipima ubavu katika vikao
vya kitaifa vya CCM katika hekaheka ya kuomba kura, akiwa amejitosa kuwania
ujumbe wa NEC kwa kupigiwa kura na Mkutano Mkuu ambao ndio hupitisha jina la
mgombea urais.
Wenzake
ambao nao wanatajwa kuweza kuwania urais 2015, Lowassa aligombea u-NEC katika
Wilaya ya Monduli anakotoka, wakati Sitta aligombea u-NEC kupitia nafasi za
wabunge wa CCM.
Wengine
wanaotajwa katika kinyang’anyiro cha urais ambao nao hawakupata nafasi ya
kupima ubavu wao wa kuomba kura za NEC, ni pamoja na Dk. John Magufuli na Dk.
Harrison Mwakyembe.
Kwa
hiyo, kwa mujibu wa vyanzo kadhaa vya habari, majina ya wagombea hao watarajiwa
kutopendekezwa na Kikwete ni pigo moja lakini pigo jingine ni kwao kushindwa
kupima nguvu zao ndani ya NEC mpya.
Pigo
jingine zaidi kwao linatajwa kuwa ni kushindwa kuwamo katika Kamati Kuu (CC),
kikao kinachotajwa kutengeneza mizengwe kuhusu mbinu za kumpata mgombea, kama
wangeingia wangeweza kukuza mikakati yao ya kisiasa kwa kutumia mwenendo wa
vikao hivyo vya CC.
Hata hivyo,
kuwa mjumbe wa Kamati Kuu si tiketi ya moja kwa moja ya kujihakikishia ushindi.
Mifano ya kuthibitisha hilo pamoja na yaliyojitokeza kwa Benjamin Mkapa mwaka
1995. Wakati huo hakuwa mjumbe wa Kamati Kuu, lakini kwa kutegemea zaidi nguvu
za ushawishi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alishinda.
Wapo
pia waliowahi kuwa wajumbe wa Kamati Kuu na wakaanguka kwenye mbio za urais
ndani ya CCM, hao ni pamoja na Frederick Sumaye, akiwa Waziri Mkuu, 2005 Cleopa
David Msuya (1995) na John Malecela (2005), akiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM.
Kamati Kuu mpya ya CCM
Kurejea
kwa Dk. Salim Ahmed Salim kwenye siasa za juu za CCM, mapema wiki hii mjini
Dodoma, ambaye katika kinyang’anyiro cha urais 2005 alichuana na Jakaya Kikwete
na kupigwa mzengwe kunatafsiriwa kuwa ni ishara nyingine ya chama hicho kupuuza
siasa za kimtandao zilizokuwa zikiendeshwa kwa takriban miaka zaidi ya 10 sasa.
Hata
hivyo, inaelezwa kwamba mwendelezo wa siasa hizo za kimtandao kwa sehemu kubwa,
pamoja na udhaifu wa serikali, vimetoa nguvu kwa siasa za upinzani kukomaa
nchini kwa sababu CCM ilijikuta ikitumia muda mwingi kukabili mashambulizi ya
ndani, hadi kuundwa kwa Kamati Maalumu kukabili mpasuko.
Kamati
hiyo maalumu iliongozwa na rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi na wajumbe Pius
Msekwa na Katibu Mkuu wa sasa wa CCM, Abdulrahaman Kinana. Wakati huo, kambi
mbili kuu bungeni zilikuwa zikitafunana kwa kujitambulisha kwa majina ya kambi
ya mafisadi na kambi ya wapinga ufisadi.
Rafu zawarejesha wakongwe
Ukiondoa
wajumbe wengine wapya wa Kamati Kuu hiyo mpya, bado jina la Dk. Salim
linaendeleza mjadala kwa kuhusishwa na siasa za maji taka alizowahi kufanyiwa
mwaka 2005 na kundi linalotajwa kuwa la mtandao.
Wajumbe
hao katika orodha hiyo inayomjumuisha Dk. Salim ni pamoja na Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka; Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Bunge na Uratibu), William Lukuvi; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Uhusiano), Stephen Wassira, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi
Vuai Nahodha na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Wengine
ni Mbunge wa Viti Maalumu, Pindi Chana; Meya wa Manispaa ya Ilala (Dar es Salaam)
Jerry Silaa; Meya wa Manispaa ya Dodoma, Adam Kimbisa; Waziri wa Afya na Ustawi
wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi; mwanasiasa mpya, Profesa Makame Mbarawa; Dk. Maua
Daftari, Khadija Aboud pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano), Samia Suluhu Hassan.
Ni kwa
kuichambua orodha hiyo mpya ya wajumbe wa Kamati Kuu iliyopitishwa Dodoma
mwanzoni mwa wiki hii, inabainika ya kwamba, kurejea kwa Dk. Salim na
kukubaliwa kwake na kura za waNEC kuwa Kamati Kuu ni mjadala mpana zaidi.
Katika
vikao vya Kamati Kuu Salim atakutana na majeruhi mwenzake wa siasa za
kimtandao, Philip Mangula, ambaye kwa wakati huo, mwaka 2005, alipoteza ukatibu
mkuu wa CCM ghafla, akijikuta hana gari ya kurejea mjini Dodoma kutokea ukumbi
wa mkutano wa CCM-Chimwaga, baada ya gari la hadhi ya Katibu Mkuu kuchukuliwa.
Makamba ndiye aliyerithi mikoba yake.
Kwa
sasa, taarifa zinaeleza uzito wa Kamati Kuu na hadhi yake inapewa nguvu mbele
ya umma kutokana na kuwapo kwa Dk. Salim, Mangula, Kinana na katika mtazamo wa
kimataifa, Profesa Tibaijuka na Dk. Asha Rose Migiro, huku nafasi ya vijana
ikibebwa na Nape Nnauye, Jerry Silaa na Mwigulu Nchemba.
Hata
hivyo, katika Kamati Kuu hiyo wapo wajumbe ambao wanatiliwa shaka kuendeleza
siasa za makundi na wengine wakiwa na harufu ya rushwa, wakihusishwa katika
vitendo vya rushwa katika changuzi za chama hicho zilizopita.
Source:
Raia Mwema
No comments:
Post a Comment