RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein, amewataka waumini wa dini ya Kikristo kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha majonzi yanayotokana na kifo cha Padri, Evarist Mushi.
Wito huo wa Rais, ulitolewa jana na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Vuga, Mjini Unguja.
Wito huo wa Rais, ulitolewa jana na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Vuga, Mjini Unguja.
Aboud alisema mtandao wa matukio hayo ni mkubwa na kwamba unapaswa kuvunjwa lakini wananchi wasiposhirikiana na Serikali kwa kutoa taarifa kwa Jehsi la Polisi , kazi hiyo itakuwa ni ngumu kufanikiwa.
“Tunataka kumaliza huu mtandao kwa hivyo wananchi watoe ushirikiano kwa vyombo vyetu vya ulinzi, ili kufanikisha hili, bila ya ushirikiano matumaini ya kuwamaliza wahalifu yatakuwa madogo,” alisema.
Aboud alisema Rais Kikwete na Rais Shein wote hawapendi kusikia wala kuona vitendo vya kihalifu na uvunjifu wa amani vikitokea Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
Waziri huyo alikanusha kuwa wachunguzi kutoka nje wamewasili Zanziabr na kwamba madai hayo ni ya kuwatia hofu wananchi.
Alisema hata hivyo kuna jitihada za kuongeza nguvu za ulinzi.
“Kuwaomba walinzi kutoka nje ni kuwatia hofu wananchi, lakini kuna haja ya kuongeza nguvu kwa vyombo vyetu vya Serikali kwa sababu wenzetu wana uzoefu mkubwa wa masuala hayo,” alisema Aboud.
Aliwaambia waandishi wa habari kwamba zipo kasoro kwa Jeshi la Polisi lakini pia wamekuwa wakifanya kazi vizuri na kuwataka wananchi kuwaunga mkono kwa kuwasaidia kuwafichua wahalifu ambao wanaonekana kuendeleza matukio ya kihalifu.
Akizungumzia kuwapo kwa bandari bubu zinazotumika kupitishia silaha, Aboud alikiri na kwamba bandari kama hizo haziepukiki.
“Zanzibar ni kisiwa, na kwenye kisiwa bandari kama hizo zisizo rasmi haziwezi kukosekana na hilo la kuingizwa silaha tunalifahamu lakini bado tunasema kwamba tutaongeza nguvu ya kuweka ulinzi katika bandari hizo,” aliongeza.
source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment