NA SHARON SAUWA
Siku moja baada ya kuuawa Mchungaji wa Kanisa la TAG mkoani Geita, Mathayo Machila (45), Rais Jakaya Kikwete amesema mgogoro wa dini ni fedheha na kwamba serikali itawashughulikia wote waliohusika.
Aliyasema hayo mjini Dodoma jana alipokuwa akiwatambulisha wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa wanachama.
Aliwataka Watanzania kuishi kama mwanzo walivyokuwa wakiishi kwa kuvumilia na kila mmoja kuheshimu hisia za mwenzake.
“Hatujawahi kupigana Waislamu na Wakristo kwa masuala ya dini, lakini jana (juzi) lilitokea na maisha ya watu yalipotea, ni jambo la fedheha na la kusikitisha,” alisema na kuongeza: “Serikali tutaendelea na yale yanayotuhusu kulinda amani, kubaini wachochezi na kuwashughulikia.”
Alisema viongozi wa dini wana mchango mkubwa katika masuala yanayohusu amani na kwamba watakapowaambia waumini wao jambo watafanya na wakiwaeleza wasifanye hawatafanya.
Alitaka kujiuliza ni kwanini tumefika hapa na kuhakikisha kuwa mambo hayo hayatatokea tena.
“Cha msingi tujiulize tumefika hapo na kwanini tumefika hapo?” alihoji na kuendelea: “Kwani vita ya dini haina mshindi kwani kila mmoja yuko sahihi kwa imani yake, hamuwezi kupata mshindi.”
“Tumeishi kwa zaidi ya nusu karne, tukiwa watulivu hivyo tusiruhusu vitendo vya aina hiyo kuharibu utulivu wetu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment