JAHAZI la Simba limeendelea kuzama
baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar katika mechi ya
Ligi Kuu Tanzania Bara iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es
Salaam.
Beki Salvatory Ntebe aliifungia Mtibwa
Sugar bao pekee katika dakika ya 18 akiunganisha vizuri pasi nzuri ya Vicent
Barnabas katika mchezo huo ambao Simba walimaliza wakiwa 10 baada ya beki Juma
Nyoso kupewa kadi nyekundu katika dakika ya 86.
Kwa matokeo hayo Simba imebaki ikiwa
nafasi ya tatu na pointi zake 31, huku Yanga wakiendelea kuongoza wakiwa na
pointi 39, wakifuatiwa na Azam (36) katika mbio hizo za kusaka ubingwa.
Kocha wa Simba, Patrick Liewig alisema
nafasi ya timu yake kutwaa ubingwa ni ndogo kwa sasa kutokana na matokeo hayo.
“Uchovu wa safari ndefu iliyoifanya
timu yake hivi karibuni mikoani na kucheza mechi za mfululizo ni sababu ya
kupoteza mchezo wa leo,” alijitetea kocha huyo.
Naye Mecky Mexime aliwasifu wachezaji
wake kwa kucheza vizuri na kufanikiwa kupata ushindi huo mzuri dhidi ya Simba.
Katika mechi hiyo dakika ya pili, beki
Amir Maftah alipitisha krosi nzuri kwa Shomari Kapombe aliyepiga shuti kali
lililopaa juu ya lango la Mtibwa Sugar.
Katika dakika ya 18, pasi ya Barnabas
ilimkuta Ntebe aliyepiga shuti kali lililomshinda kipa Juma Kaseja na kujaa
wavuni hivyo kuipa Mtibwa Sugar bao la kuongoza.
Kuingia kwa bao hilo kuliamsha ari ya
Mtibwa Sugar kwani katika dakika ya 23, shuti la mshambuliaji Hussein Javu
lilipanguliwa kwa ustadi mkubwa na kipa Kaseja.
Simba ilijaribu kurudi mchezoni katika
dakika ya 28, ambapo Felix Sunzu alipiga shuti kali, lakini lilipaa juu ya
lango la Mtibwa.
Katika mchezo huo kocha wa Simba,
Liewig hakuwaanzisha wachezaji wake mahiri, Amri Kiemba pamoja na Mrisho
Ngassa, lakini baadaye alifanya mabadiliko kwani aliwatoa Ramadhani Chombo,
Haruna Moshi na Haruna Chanongo na kuwaingiza Kigi Makasi, Kiemba na Ngassa.
Katika hali ya kushangaza wachezaji
Chombo na Moshi baada ya kutolewa walikwenda moja kwa moja kwenye vyumba vya
kubadilishia nguo badala ya kukaa katika benchi.
Pamoja
na mabadiliko hayo, Simba ilishindwa kurudi mchezoni, ambapo zikiwa zimebaki
dakika nne kabla ya mchezo kumalizika, mwamuzi Ibrahim Kidiwa ‘Mdudu’ alitoa
kadi nyekundu kwa Nyoso kwa kumchezea vibaya Barnabas.
Vikosi
Simba:
Juma Kaseja, Nasoro Masoud, Amir Maftah, Juma Nyoso, Komanbil Keita, Shomari
Kapombe, Ramadhan Chombo/Kigi Makasi, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Haruna
Moshi/Amri Kiemba na Haruna Chanongo/Mrisho Ngassa.
Mtibwa
Sugar: Hussein Shariff, Said Mkopi, Issa Rashid, Salvatory Ntebe, Salum Sued,
Shaaban Nditi, Jamal Mnyate, Rashid Gumbo, Hussein Javu, Shaaban Kisiga na
Vicent Barnabas.
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment