WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, February 2, 2013

JK: Uhalifu wa Mtwara haukubaliki


NA WAANDISHI WETU

Rais Dk. Jakaya Kikwete

Rais Dk. Jakaya Kikwete, amesema uhalifu uliotokea Mtwara haukubaliki na kwamba vyombo vya dola vitawashughulikia waliohusika ili liwe fundisho kwa wote.

Kadhalika, alieleza kusikitishwa na kufadhaishwa na vitendo vya kuua, kuchoma moto na kuharibu majengo ya serikali, nyumba na kuiba mali za watu.

Katika hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi, aliyoitoa jana Dk. Kikwete uliuita uhalifu usio na maelezo na haukubaliki.

Aliwapa pole wana-Mtwara na Masasi kwa usumbufu walioupata kufuatia ghasia zilizofanywa kupinga uwekezaji wa gesi.

“Serikali inawathamini na kuwajali wana-Mtwara nakuwapuuza na kuwatupa mkono wananchi wa mikoa ya Kusini. “

Alikumbusha kuwa mikoa hiyo haijasahaulika na kwamba daraja la Mto Rufiji maarufu kama Daraja la Mkapa ni uthibitisho. 

“Hii ilikuwa ni hatua ya awali kutatua matatizo ya usafiri ya mikoa ya Kusini, serikali yangu imekamilisha ujenzi wa barabara za lami kufikia darajani na kuunganisha mikoa ya  Mtwara na Ruvuma tumeitekeleza vizuri na sasa tunakaribia kuimaliza,” alisema.

KUHUSU GESI NA VURUGU
Rais Kikwete alisisitiza kuwa suala la bomba la gesi limefika mahali pazuri na kutumia usemi usemao ‘yaliyopita si ndwele tugange yajayo’.

Alizungumzia kujenga bomba la kuipeleka gesi Dar es Salaam alisema hakuinyimi mikoa ya Mtwara na Lindi fursa ya kunufaika na gesi hiyo.

Aliahidi kuwa serikali imefanya na ina mipango ya mizuri ya kuwekeza na kuleta maendeleo ya wananchi wa Mtwara na Lindi.

Alitaja baadhi ya  mipango hiyo kuwa ni kuboresha miundombinu, huduma za kijamii ,  kujenga viwanda vikubwa na vidogo Lindi na Mtwara, kuipanua na kuijenga upya bandari ya Mtwara ili ihudumie kufanikisha uchimbaji wa gesi baharini, kuhudumia na kuvifanyia matengenezo vyombo vinavyotumika katika utafiti, uchimbaji na uendelezaji wa gesi.

Aliongeza kuwa mwaka juzi alikubali ombi la makampuni yanayotafuta gesi Mtwara la kuifanya bandari ya Mtwara ihudumie vyombo vyote vinavyofanya shughuli ya utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta katika pwani ya Afrika ya bahari kuu ya Hindi.

“Pia nilikubali Mtwara iwe bandari huru na tayari hekari 110 zimetengwa na kutangazwa rasmi kuwa bandari huru.”

Alisema wawekezaji waliomba wapewe sehemu ya bandari ya sasa kuendeshea shughuli na eneo la kujenga kituo cha mitambo ya kuchakata gesi na kusafirisha nje. 

“Baada ya kuzungumza na makampuni haya na kuelezwa mahitaji yao nilibaini kuwa bandari ya Mtwara inahitaji kupanuliwa na kujengwa upya, viongozi wa Mamlaka ya Bandari walikuwepo na walinihakikishia kuwa watafanya hivyo,” alisema na kuongeza:

“Tayari eneo la bandari limeongezwa kutoka hekta 70.68 hadi 2,693.68, eneo la bandari huru limeshatengwa hivyo hivyo na eneo la kampuni ya Dangote na makampuni ya gesi yaliyopo.  

Aidha, mchakato wa kupanua bandari iliyopo, kujenga gati mpya na kuendelea na ujenzi hadi maeneo ya Msanga Mkuu ipo katika hatua mbalimbali za matayarisho na utekelezaji,”
alisema. 

Alikumbushia kuwa Novemba mwaka jana aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asili kutoka mkoani humo kuja Dar es Salaam eneo la Kinyerezi lakini mwezi uliofuata yalifanyika maandamano Mtwara kupinga ujenzi huo. Maandamano yalitaka gesi hiyo itumike kwa maendeleo ya Mtwara na kwamba yale yanayotakiwa kufanyika Dar es Salaam yafanyike Mtwara.

Pia, alisema serikali ilishutumiwa kuwa imewasahau na haiwajali wananchi wa Kusini na ujenzi wa bomba hilo ni muendelezo wa hayo.

“Kauli hizi za wanasiasa na wanaharakati ni kama vile ziliongeza mafuta kwenye kaa la moto na kuuchochea mpaka kukatokea matukio yaliyotusikitisha na kutushtua sote….,” alisema.

MAENDELEO YA MTWARA
Alisema hivi sasa Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA)  Mtwara inatoa mafunzo kwa kushirikana na kampuni ya PetroBras ya Brazil inaendesha mafunzo ya sekta ya gesi kwa vijana 25 kutoka mkoani Mtwara.

“Nilisisitiza tuwapatie vijana wetu mafunzo yatakayowawezesha kuajiriwa na makampuni ya gesi na yale yatakayokuwa yanatoa huduma kwa makampuni hayo kwa sababu kinyume na hapo  makampuni hayo yataajiri watu kutoka nje,” alisema.

Aliongeza kuwa Wizara ya Nishati na Madini imetoa upendeleo maalum wa kudhamini wanafunzi 50 kutoka Mtwara kusoma masuala ya gesi  na  wamehitimu mafunzo ya msingi ya uunganishaji vyuma viwandani.

Alisema mchakato wa kuwapata wanafunzi 50 kwa ajili ya mafunzo kama hayo kutoka mkoa wa Lindi unaendelea na kwamba hadi sasa wamepatikana 25 na Wizara inawadhamini wanafunzi 10 kupata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Dodoma.

KUHUSU UWEKEZAJI
Alisema mpaka sasa makampuni 51 yameonyesha nia ya kuwekeza Mtwara katika viwanda, hoteli, shughuli za uchukuzi na huduma hasa kwa sekta ya gesi ambapo wanasubiri kutengewa maeneo ya kujenga.

Alisema kukamilika mapema kwa ‘Masterplan’ ya mji wa Mtwara kutasaidia kuongeza kasi ya uwekezaji huu.

“Nimeambiwa kwa mfano, wakati wa ujenzi wa kiwanda cha saruji watu zaidi ya 7,000 wataajiriwa,” alisema. 

Akizungumzia gesi iliyoko baharini, alisema kulikuwa na mipango ya kutumia gesi ya Msimbati (Mnazi Bay) kwa ajili ya kuzalisha umeme, kuzalisha mbolea na kutumika katika kiwanda cha saruji. 

Akizungumzia kuhusu kiwanda cha saruji kitakachojengwa na kampuni ya Dangote Dk. Kikwete alisema  ucheleweshaji ulisababishwa na kampuni hiyo kuomba eneo zaidi ya ililokuwa imeomba na kupewa.

Aidha alisema baada ya mwenye eneo kupinga mahakamani, walishinda lakini kampuni hiyo ilichukua muda kuanza na kwamba hivi sasa timu yake ipo kwenye eneo la mradi tayari kwa kuanza.

“Madai kuwa kiwanda hicho kimehamishiwa Bagamoyo si ya kweli.  Ni uzushi wa makusudi wa watu wenye nia mbaya na serikali.Huwezi kudai kuwa mtetezi wa wananchi wa Mtwara kwa hoja za uongo na kufanya upotoshaji wa makusudi kabisa,”alisema.

“Wengine walisema gesi inapalekwa Bagamoyo ili kuzidisha chumvi na kupandikiza chuki kwa wananchi dhidi ya serikali kwamba Rais anapeleka gesi kwao. Kwanza, Kinyerezi iko Ilala na siyo Bagamoyo,” alisema na kuongeza:

“Ukweli ni kwamba pale Mtwara kuna gesi nyingi ya kutosheleza mahitaji yao ya Lindi na Dar es Salaam na kubaki.  Gesi itakayoletwa Dar es Salaam ni asilimia 16 tu iliyoko Mtwara….hivyo asilimia 84 ya gesi itabaki Mtwara kwa ajili ya kuuzwa nje ya nchi na kupelekwa kwingineko nchini,” alisema. Amewataka wanamtwara kutokuwa na wasiwasi na kuwaeleza kuwa ipo gesi ya kutosha kwa mahitaji ya sasa na ya miaka mingi ijayo.

MNYAA AWASILISHA MAOMBI YA WANAMTWARA
MBUNGE wa  Mkanyageni  (CUF),  Mohamed Mnyaa, amewasilisha kwa Spika Anne Makinda maombi ya wananchi  Mtwara yajadiliwe bungeni.

Akizungumza na wanahabari jana mjini hapa, Mnyaa alisema licha ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwenda mkoani humo kutafuta suluhu ya matatizo  yaliyoibuka Mtwara,  kuna mambo mengine yalisahaulika.

Alitaja suala la kutaka gridi ya taifa ya umeme kupelekwa Mtwara kuwa ni miongoni mwa mambo yaliyowasilishwa na kusema  maelezo ya hoja ya gridi  hayawekwa sawa ama kupatiwa ufumbuzi  na Waziri Mkuu.

Alisema  serikali pekee haiwezi kumaliza mgogoro huo hivyo ameona haja  ya maombi hayo kuwasilishwa, bungeni kujadiliwa na kupatiwa muafaka ni muhimu.

Aliwaambia waandishi kuwa amewasilisha maombi zaidi ya 22,000 ya wana-Mtwara ili yafanyiwe kazi kwani Lindi na Mtwara ni mikoa iliyosahaulika.
Imeandaliwa na Romana Mallya, Dar na Beatrice Shayo, Dodoma
kwamba atakuwa mtu wa mwisho
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment