- Kwenda Bunge la Katiba Novemba
TUME ya
Mabadiliko ya Katiba, inatarajia kukabidhi rasmi Ripoti yake na Rasimu ya
Katiba kwa Marais Jakaya Kikwete wa Jamhuri ya Muungano na Dk. Ali Mohamed
Shein wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Oktoba, mwaka huu, imefahamika.
Sambamba na hilo, Tume
hiyo itawasilisha rasmi Rasimu ya Katiba hiyo katika kikao cha Bunge Maalumu la
Katiba, Novemba 11, mwaka huu, kabla ya Bunge hilo kujadili Rasimu hiyo kuanzia
tarehe hiyo hadi Januari 19, mwaka ujao wa 2014 na kuiridhia kuwa Katiba rasmi
ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Mpango
kazi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba,
unaoonyeshwa katika kalenda ya mwaka huu ya Tume hiyo, kukabidhiwa kwa Ripoti
na Rasimu ya Katiba Mpya kwa marais, na baadaye Rasimu hiyo kuwasilishwa mbele
ya Bunge Maalumu la Katiba, itakuwa ndiyo mwanzo wa upatikanaji wa Katiba Mpya,
ambayo uzinduzi wake unatarajiwa kufanyika rasmi katika kilele cha maadhimisho
ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, hapo Aprili 26, 2014.
Akizungumza
na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari katika ofisi za Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, jijini Dar es Salaam, juzi Jumatatu, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji
Warioba, alisema Tume yake ilikamilisha mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi
mmoja mmoja kupitia mikutano ya wazi Desemba 19, mwaka jana, kabla ya Januari 7
hadi Januari 28 mwaka huu kukusanya maoni ya makundi maalumu ya kijamii
wakiwamo viongozi wa sasa, wastaafu na watu mashuhuri.
Aliyataja
makundi maalumu hayo kuwa ni pamoja na vyama vya siasa, ambapo Tume ilikutana
na vyama 19 vya siasa kati ya 20 vyenye usajili wa kudumu, taasisi 22 za
kidini, tasisi 72 za kiraia, taasisi 71 za kiserikali na viongozi na watu
mashuhuri takriban 43 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Katika
mkutano huo na waandishi wa habari, ambao Tume hiyo iliuitisha kwa lengo la
kuelezea utaratibu wa uundwaji wa Mabaraza ya Katiba, Jaji Warioba alisema
kabla ya Rasimu ya Katiba Mpya kukabidhiwa kwa marais Kikwete na Dk. Shein na
baadaye Bunge Maalumu la Katiba kwa hatua ya mwisho, Rasimu hiyo itajadiliwa
kwanza na wananchi kupitia mabaraza yao watakayoyaunda wenyewe kuanzia kwenye
ngazi ya Kata kwa Tanzania Bara na Shehia kwa Tanzania Visiwani.
Aidha,
alisema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, inataka wananchi wapate
kwanza fursa ya kuisoma Rasimu hiyo, ikiwa ni pamoja na kuchapishwa katika
magazeti mbalimbali kama sehemu ya kutoa elimu kwa umma, kabla ya kuwasilishwa
rasmi katika Mabaraza hayo ya Katiba yatakayoitishwa na kuratibiwa na Tume
hiyo.
Wachambuzi
kadhaa wa mambo kuhusu mwenendo wa mchakato wa utoaji wa maoni kuhusu Katiba
hiyo, wanasema wazi kwamba huenda ukatokea mvutano mkali baina ya vyama vikuu
viwili vyenye ushawishi na ufuasi mkubwa kwa Tanzania Bara, Chama cha Mapinduzi
(CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika upatikanaji wa
wajumbe wa Mabaraza hayo, kila chama kikitaka kiwe na uwakilishi mkubwa kwa
lengo kulinda na kutetea matakwa na maslahi ya vyama hivyo.
Katika
uundaji huo wa Mabaraza ya Katiba, mikoa yote ya Tanzania Bara, isipokuwa Dar
es Salaam, kila Kata itatakiwa kuwa na uwakilishi wa wajumbe wanne. Kwa upande
wa mkoa wa Dar es Salaam wenye idadi kubwa ya watu ikilinganishwa na mikoa
mingine nchini, kila Kata itawakilishwa na wajumbe wanane, wakati kwa upande wa
Tanzania Visiwani, kila Shehia itatakiwa kuwa na wajumbe watatu. Diwani wa kila
Kata na kila Shehia ataingia moja kwa moja kuwa mjumbe na kufanya idadi hiyo ya
wajumbe wanaotakiwa.
Wakati
wa mchakato wa awali kabisa wa kuandikwa kwa sheria ya mabadiliko ya Katiba
kulitokea mvutano mkali baina ya makada wa CCM na CHADEMA, kila upande
ukisimama kidete kuhakikisha kwamba baadhi ya matakwa ya vyama vyao yanaingizwa
ndani ya sheria hiyo, kiasi cha baadhi ya wabunge wa CHADEMA kususia
upitishwaji wa sheria hiyo kwa kutoka nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.
Hali
kama hiyo ndiyo inayotazamiwa na wachambuzi hao wa mambo kujitokeza katika
mchakato huu unaofuata wa uundaji wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, yenye jukumu
la kupitia na kutolea maoni Rasimu ya Katiba hiyo, kwa kila chama kati ya vyama
vikuu hivyo viwili mahasimu kwa Tanzania Bara, lakini pia kwa CUF dhidi ya CCM
kwa upande wa Zanzibar, kwa kila kimoja kujaribu kuhakikisha kwamba wajumbe
walio wengi wanatokana na vyama hivyo kwa lengo la kutaka kupenyeza matakwa ya
kila chama katika Rasimu hiyo kabla ya kuandikwa rasmi.
Kwa
mujibu wa ratiba ya mpango kazi huo katika kalenda ya Tume hiyo ya mwaka 2013,
kuanzia Jumpili iliyopita ya Februari 3 hadi Machi 4, mwaka huu, Tume ya
Mabadiliko ya Katiba itakuwa na kazi muhimu ya uchambuzi wa maoni mbalimbali yaliyotolewa
na wananchi mmoja mmoja, makundi ya kijamii na ya viongozi na watu mashuhuri.
Aidha,
kuanzia Machi 5 hadi Aprili 3, Tume itakuwa na kazi ya kuandika Rasimu ya
Ripoti ya ukusanyaji wa maoni hayo, wakati kazi ya kuandika Rasimu ya Katiba
itaanza Aprili 4 hadi Mei 2, mwaka huu. Kazi hiyo itafuatiwa na uchapwaji wa
Rasimu hiyo utakayofanywa kati ya Mei 3 na 8, kabla ya kuingia kwenye hatua ya
kutoa elimu kwa wananchi kuhusu Rasimu ya Katiba hiyo, kazi itakayofanyika
kuanzia Mei 9 hadi Juni 7, mwaka huu.
Kati ya
Juni 10 hadi Agosti 7, mwaka huu, mpango kazi huo unaonyesha kwamba Tume ya Mabadiliko
ya Katiba itakuwa na kibarua kingine kigumu cha kuratibu na kusimamia mikutano
ya Mabaraza ya Katiba ya kila wilaya nchini, mabaraza ambayo yatakuwa na jukumu
la kupitia, kujadili na kutolea maoni Rasimu hiyo ya Katiba.
Kalenda
hiyo ya kazi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba, inaonyesha zaidi kwamba kati ya
Agosti 12 na Septemba 10, kutakuwa na kazi ya kuchambua maoni yatakayotokana na
Mabaraza ya Katiba, kabla ya Ripoti na Rasimu ya Katiba hiyo kuingizwa
mitamboni tena kwa ajili ya kuchapwa, kazi itakayofanyika kuanzia Septemba 11
hadi Septemba 30.
Jumanne
ya Oktoba Mosi, mwaka huu, Tume ya Mabaduiliko ya Katiba itakabidhi Ripoti na
Rasimu ya Katiba Mpya kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Kikwete, na
siku ya Alhamisi ya Oktoba 3, mwaka huu, Tume hiyo itakabidhi Ripoti na Rasimu
ya Katiba kwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Habari
zinasema baada ya marais hao kukabidhiwa Ripoti na Rasimu ya Katiba,
watalazimika sasa kukutana na kuunda Bunge Maalum la Katiba kwa mujibu wa
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kabla ya Bunge hilo nalo kupokea Rasimu hiyo ya
Katiba na kuanza kuijadili katika kikao chake cha kwanza kitakachoanza Novemba
11, mwaka huu hadi Januari 19, 2014.
Akitangaza
mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya mapema mwaka jana, Rais Kikwete aliiagiza
Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuhakikisha inakamilisha kazi hiyo mapema
iwezekanavyo ili Katiba Mpya iweze kuzinduliwa rasmi katika kilele cha
maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ulioasisiwa
rasmi na waasisi wa Taifa hili, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh
Abeid Amani Karume, Aprili 26, 1964.
Source:
Raia Mwema
No comments:
Post a Comment