NA WAANDISHI WETU
Rais Jakaya Kikwete ameongoza maelfu ya Watanzania kuomboleza aliyekuwa Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Thomas Laizer, aliyefariki juzi katika hospitali ya Selian mjini Arusha.
Rais Kikwete, amemtumia salaam za rambirambi Askofu Mkuu wa Kanisa hilo nchini, Dk Alex Malasusa, kufuatia kifo hicho na kueleza kuwa, enzi za uhai wake ametoa mchango katika uongozi wa kiroho kwa Watanzania.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi jijini Dar es Salaam na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, marehemu Askofu Laizer, atakumbukwa kwa utumishi wake kwa kanisa na taifa.
“Alitumia vipaji vyake kuwatumikia waumini waliokuwa chini yake, kufuatia msiba huu nakutumia salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kukupa pole ya msiba huu,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
MALASUSA: ALIPIGA VITA UMASIKINI
Askofu Mkuu wa Kanisa hilo nchini, Dk Alex Malasusa, alisema mazishi ya Askofu Laizer, yanatarajia kufanyika Ijumaa ijayo Mjini Kati, Arusha.
Dk. Malasusa alisema Alhamis ijayo, waumini na wananchi wengine watatoa heshima za mwisho na siku itakayofuata atazikwa katika eneo la kanisa la Mjini Kati.
Alisema enzi za uhai wake, marehemu Askofu Laizer alianzisha miradi ya maendeleo iliyowawezesha waumini wake kuondokana na umasikini.
Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, alisema miongoni mwa mambo yaliyoasisiwa na kuendelezwa na marehemu Askofu Laizer ujenzi wa hospitali ya kisasa ya Selian, hoteli ya Corridor Springs na shule mbalimbali.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alisema Askofu Laizer alikuwa ni kiongozi jasiri ambaye enzi za uhai wake alitoa misaada mingi kwa jamii, dayosisi ya mkoa na serikali kwa ujumla.
Alikumbusha moja ya mambo aliyokemea kwa ujasiri ni kuhusu kitendo cha vijana kupelekwa porini na kukaa huko muda mrefu kwa ajili ya kutahiriwa na kusababisha kukosa elimu.
Alisema kufanya hivyo kulihitaji ujasiri wa pekee kwa jamii yake ya kabila la Wamasai.
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alisema kifo cha Askofu Laizer, kimemgusa kwa sababu mara nyingi (Lema) alikuwa akimfuata ofisi kwake kuomba ushauri katika masuala ya kisiasa.
Alisema atamkumbuka hasa aliposimama kidete kama kiongozi wa dini kupinga uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha.
“Kama kiongozi wa dini na Mtumishi wa Mungu, alikuwa na haki ya kukemea, kukaripia, kuonya, kurekebisha na kushauri,” ALISEMA.
MKE WA LAIZER AFUNGUKA
Mke wa marehemu, Maria Thomas Laizer, alisema alianza kuhisi mwili wake una tatizo, muda mrefu baada ya kutokewa na tezi la upande wa kushoto.
Alisema alifanyika uchunguzi hospitali mbalimbali na majibu yalionyesha hana tatizo Jingine zaidi ya tezi.
“Ilipita miaka 10 kutoka tatizo hilo ligundulike, mwaka 2010 alizidiwa na kupelekwa hospitali ya Selian ambapo huko iligundulika tezi lina tatizo ambalo alishauriwa aende Nairobi, nchini Kenya kwa matibabu zaidi,” alisema.
Maria alisema baada ya kufika Nairobi majibu ya daktari yalionyesha tatizo lililopo ni kubwa hivyo anatakiwa kupelekwa nchini India.
Alisema kutokana na gharama za matibabu kuwa kubwa, waumini walichangia na mwezi Septemba mwaka jana, walienda nchini humo kwa matibabu.
Alisema uchunguzi ulionyesha tezi hilo limesababisha ugonjwa wa saratani hivyo kupelekea tumbo kujaa maji na baadaye
kushindwa kuhema.
“Tulirudi nchini aliendelea na matibabu na kulazwa hospitali ya Selian na kukumbwa na umauti, kabla ya kifo chake alidhoofu sana, alishindwa kabisa hata kuhema, nashukuru viongozi wa serikali, wanasiasa na wa dini walitufariji,” alisema.
“Askofu Laizer aliongea neno la mwisho kabla ya kukata roho na
kushukuru wote waliomwombea kwa sala na angetamani sana kanisa lidumu kwa kutekeleza yale yote aliyoacha wakati wa uhai wake,” alisema.
MTOTO WA MAREHEMU AOMBA
Mtoto wa marehemu Ezra Laizer, amewaomba waumini wa kanisa hilo kumsamehe baba yao kwa mabaya aliyofanya na kuyachukua mazuri aliyotenda katika uhai wake
“Tunaamini kifo ni kifo na hasa unapoondokewa na mzazi, lakini kikubwa baba alikuwa kiongozi wa watu hivyo kama binadamu alitenda mambo mengi mazuri, lakini jambo moja baya lisichukuliwe na kuwa ndilo alilotenda…” alisema hayo bila kufafanua zaidi.
Naye, mkazi wa Elerai jijini hapa, Samuel Mollel, alisema atamkumbuka askofu huyo kupitia mahubiri yake na jinsi alivyokuwa akikemea ufisadi na dhuluma zingine katika jamii.
HISTORIA FUPI
Alizaliwa Machi 10, mwaka 1945 katika kijiji cha Ketumbeine wilayani Arumeru mkoani Arusha. Alisoma Shule ya Msingi Long’ido na kuhitimu darasa la nane mwaka 1965, ambapo alijiunga na Shule ya Sekondari Arusha na kuhitimu 1965.
Baada ya hapo alijiunga na masomo ya Theolojia (BD), katika chuo cha Makumira na kuhitimu 1972, ambapo aliendelea na masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Wartburg cha nchini Marekani na kuhitimu 1984.
Alianza kazi rasmi katika Sharika mbalimbali kama Mkuu wa Jimbo, Sinodi na hatimaye akafanikiwa kuwa Rais wa Sinodi katika vipindi tofauti.
Januari 4, mwaka 1987 alisimikwa rasmi kuwa askofu wa Dayosisi ya mkoani Arusha na baadaye ya Kaskazini na Kati.
Marehemu ameacha mke na alikuwa na watoto watano ambapo mmoja kati yao alifariki.
Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, Amen.
Habari hii imeandikwa na Romana Mallya, Efracia Massawe Dar, John Ngunge, Cynthia Mwilolezi, Arusha
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment