WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, February 4, 2013

Lema wawaa, Zitto asepa



Mbunge Lema akirejea Bungeni
WAKATI Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema akivuma katika safari yake ya kwanza kurejea bungeni Dodoma jana, Mbunge Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, ametimkia jimboni kwake katika hatua inayoashiria kuiva kwa mizengwe ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Taarifa zilizotufikia wakati tukienda mitamboni zilieleza kwamba Lema alikuwa anatarajiwa kuhutubia mkutano mkubwa mjini Dodoma baada ya kupokewa kwa maandamano yaliyotarajiwa kuanzia kijiji cha Ihumwa, umbali wa kiasi cha kilometa  14 kutoka Dodoma Mjini.
Lema alivuliwa ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Aprili 5, mwaka jana kabla ya kurejeshewa nafasi hiyo na jopo la majaji baada ya kuridhishwa na sababu za rufaa yake.
Hayo yakiendelea, taarifa za watu wa karibu na Zitto zinabainisha kuwa anatarajiwa kufanya kile kilichoelezwa kuwa ni “uamuzi mgumu” baada kushambuliwa sana katika mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), bila kupewa nafasi ya kujitetea na kwamba, mpango huo ulisukwa mahsusi ili kumchafua.
Kwa muda mrefu sasa Zitto anatajwa kuwa na mivutano na baadhi ya viongozi wa CHADEMA, wakiwamo waliomo katika sekretariati ya chama, akionekana kama mwanasiasa msaliti ndani ya chama hicho, na mivutano hiyo ilianza tangu alipokusudia kutaka kuwania uenyekiti wa CHADEMA dhidi ya Freeman Mbowe, ambaye ndiye Mwenyekiti wa sasa.
Taarifa kutoka vyanzo tofauti vya habari ndani ya mkutano wa Baraza Kuu la CHADEMA zinasema baada ya mashambulizi dhidi ya Zitto, sehemu ya wajumbe wa Baraza hilo walipiga kelele kutaka apewe nafasi ya kujieleza, lakini wito wao huo ulipuuzwa.
Kwa mujibu wa taarifa hizo za ndani ya kikao hicho, mashambulizi dhidi ya Zitto yalichomekwa katika ajenda ya mengineyo, na watu tisa walimjadili miongoni mwao wakishusha tuhuma kadhaa na wengine wakimtetea.
Hoja za mashambulizi
Kati ya hoja zilizoelekezwa kwake ni pamoja na madai ya kwamba ameshiriki kuanzisha chama cha siasa kinachoitwa Chaumma na kwamba vijana waliofukuzwa kutoka Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) ni sehemu ya kambi yake iliyolenga kuchafua baadhi ya viongozi wa kitaifa akiwamo Katibu Mkuu, Dk. Wilbroad Slaa.
“Zitto huyu ndiye aliyeanzisha Chaumma, sioni sababu ni kwa nini aachwe kuendelea kuwamo CHADEMA,” chanzo chetu cha habari kinamnukuu mmoja wa vijana (jina linahifadhiwa) aliyekuwa katikati ya mgogoro wa BAVICHA dhidi ya Makamu Mwenyekiti, Juliana Shonza. Katika mgogoro huo kijana huyo anadaiwa kuwa upande wa kambi inayoongozwa na baadhi ya viongozi wa juu wa CHADEMA, ambayo imekuwa ikikabiliana na Zitto ambaye hata hivyo, naye anatajwa kuwa na kambi yenye vijana wengi wasomi CHADEMA.
Lakini kiongozi mwingine kutoka Mkoa wa Njombe (jina linahifadhiwa) anadaiwa kusimama na anakaririwa akisema; “Kuna vijana wamefukuzwa BAVICHA kwa madai ya kuwachafua baadhi ya viongozi wa kitaifa, lakini kuna kijana anaitwa Ben Sanane, huyu ametoa kauli kadhaa za kumchafua Zitto ....kwa nini naye haadhibiwi, nani anamlinda huyu? Hivi tunajuaje kwa kumchafua Zitto huyu Sanane hafanyi kazi ya CCM?”
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, takriban watu tisa walipewa nafasi ya kuzungumza kuhusu Zitto. viongozi hao ni pamoja na mmoja kutoka Wilaya ya Ilala-Dar es Salaam, mwingine kutoka Karatu, mkoani Arusha pamoja na kutoka Kilimanjaro. Yupo pia kutoka Longido, mkoani Manyara na Njombe.
Hata hivyo, katika mashambulizi hao, kiongozi mmoja (jina linahifadhiwa) kutoka Longido alikaririwa akimtetea Zitto kwa kusema; “Ninyi mnatumiwa na CCM kuhakikisha Zitto anagombanishwa na viongozi wenzake. CCM wanapenda Zitto aporomoke kisiasa.”
Katika hatua nyingine, baada ya kuona mashambulizi yanazidi bila kupatiwa majibu, inadaiwa Zitto aliomba nafasi ya kutaka ajieleze lakini mwongoza kikao alikataa kumpa fursa hiyo.
Kutokana na kutopewa nafasi, baadhi ya wajumbe walipiga kelele wakitaka apewe nafasi ya kujieleza bila mafanikio.
“Baada ya kuona kama vile kuna mchezo mchafu dhidi yake, Zitto hakukaa kwenye kikao hadi mwisho, aliondoka wakati Mwenyekiti Mbowe (Freeman) akitoa hotuba yake. Alikasirika na baada ya muda akaondoka,” kinaeleza chanzo chetu cha habari.
Mbunge Zitto Kabwe akiwa jimboni kwake akihutubia
Katika hatua nyingine, taarifa zaidi kutoka kwa watu wa karibu na Zitto zinaeleza ya kuwa, mbunge huyo amekwenda jimboni kwake Kigoma Kaskazini, licha ya kwanza Bunge kwa sasa linaendelea na mkutano wake mjini Dodoma.

“Anakwenda kufanya uamuzi mgumu jimboni kwake,” alieleza mmoja wa watu waliokaribu na mbunge huyo ambaye hata hivyo, hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Jitihada za kumpata Zitto mwenyewe kuzungumzia hali halisi ya mambo yalivyokuwa katika mkutano huo na nini hasa kinampeleka kwao hazikuweza kufanikiwa.
Mbali na Zitto, Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda naye alishushiwa mvua ya mashambulizi akitajwa kukihujumu chama hicho. Mashambulizi hayo dhidi ya Shibuda yamefanyika huku kukiwa na taarifa kwamba baadhi ya viongozi wa chama hicho kuhakikisha mbunge huyo kutoka Kanda ya Ziwa anavuliwa uanachama.
Shibuda aliingia CHADEMA akitokea CCM kipindi kifupi kabla ya kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, wakati Zitto ameanza maisha ya siasa akiwa katika CHADEMA na hakuwahi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa.
source: Raia Mwema

No comments:

Post a Comment