VURUGU BUNGENI
- Ni Peter Msigwa wa Iringa Mjini-CHADEMA
- Siri zafichuka, Tundu Lissu achafuliwa
- Mnyika, Nassari kuhojiwa Kamati ya Maadili
WAKATI
Spika wa Bunge, Anne Makinda akiahirisha hoja binafsi za wabunge kutokana na
vurugu za bungeni Jumatatu wiki hii, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter
Msigwa, amesema upendeleo wa Spika ukizidi, kuna siku watavunja viti vya Ukumbi
wa Bunge.
Msigwa
alitoa onyo hilo alipozungumza na mwandishi wetu aliyeko Dodoma kwa ajili ya
vikao vya Bunge, akionekana kukerwa na kile wanachokiita; “Upendeleo wa Spika
kwa wabunge wa CCM.”
“Tumekwishakata
rufaa nyingi hata dhidi ya Spika mwenyewe hakuna hatua zinazochukuliwa. Hoja
zetu zinatupwa bungeni...kuna upendeleo wa wazi, achana na vurugu zile, mimi
nasema ipo siku kama hali hii itaendelea tutavunja viti bungeni,” alisema
Msigwa.
Kutokana
na uzito wa kauli hiyo, mwandishi wetu alimuuliza; “..nikunukuu kuhusu kauli
hii gazetini? Naye akajibu; “Nukuu, wala usiwe na wasiwasi ndiyo hali halisi,
uonevu ukizidi watu hujitetea kwa taratibu zao. Hatupendi kufika huko,
wajirekebishe. Wasitusukume kwenda huko.”
Maelezo ya Spika
Jumanne
wiki hii, Spika Makinda alitoa maelezo bungeni kuhusu vurugu hizo za Jumatatu
wiki hii, wakati Naibu Spika Job Ndugai, alipoongoza mjadala wa hoja binafsi
kuhusu maji safi na maji taka ya Mbunge wa Ubungo- Dar es Salaam, John Mnyika.
Katika
kikao hicho, wabunge wa upinzani walisimama na baadhi kuanza kuzomea hovyo,
wakiashiria kutokukubaliana na uamuzi wa kumruhusu Waziri wa Maji, Profesa
Jumanne Maghembe, kutoa hoja ya kuondoa hoja ya awali ya Mnyika, kwa maelezo
kuwa, Dar es Salaam imepewa bajeti kubwa na fedha nyingi za maji kuliko mikoa
mingine na zaidi ya hapo, miradi mingi ya maji inafanyika kwa hiyo hoja iwe ni
tatizo la maji nchi nzima.
Kwa
mujibu wa maelezo yake kuhusu vurugu hizo, Spika Makinda alisema Kamati ya
Uongozi ya Bunge imekemea utovu wa nidhamu wa wabunge waliozomea, lakini pia
imeahirisha hoja binafsi zilizopangwa kujadiliwa katika mkutano wa sasa wa
Bunge, unaokwisha mwishoni mwa wiki hii.
Mbali
na hayo, Spika alisema waliohusika katika fujo hizo watafikishwa katika Kamati
ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge kwa hatua zaidi. Kwa kadiri ya picha za
televisheni zilioonyeshwa moja kwa moja na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)
wakati wa fujo hizo, wabunge John Mnyika, Tundu Lissu, Peter Msigwa, Moses
Machali na wengine wengi wa kambi ya upinzani walionekana wakziomea na
mwandishi wetu aliyeko Dodoma alishuhudia hali hiyo moja kwa moja bungeni.
Lakini
katika kambi hiyo ya upinzani, wapo wabunge ambao walisimama kuungana na wenzao
bila kupiga kelele ambao ni pamoja na Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, James
Mbatia, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, wabunge wa CUF wengi
hawakusimama wala kuzomea.
Kwa
hiyo, kwa maelezo ya Spika, wabunge Mnyika, Lissu, Machali ni kati ya
watakaofikishwa Kamati ya Maadili kwa ajili ya mahojiano. Baadhi ya wabunge
ambao hawakufanya fujo nao pia wataitwa kama sehemu ya ushahidi.
Siri za mtikisiko
Siri za
mtikisiko huo bungeni wenye taswira ya upendeleo kwa wabunge wa CCM dhidi ya
wabunge wa upinzani msingi wake unatajwa ni kanuni kuu ya kidemokrasia;
“wachache wasikilizwe, wengi waamue.
Ndani
ya siri hizo inaelezwa kwamba kukwama kwa hoja binafsi za wabunge wa upinzani
msingi wake ni kushindwa kufanya ushawishi (lobbying) kabla ya hoja hizo
hazijawasilishwa bungeni, lakini pia ushindani wa kutumia Bunge kama jukwaa la
kukuza siasa za vyama ni tatizo jingine.
Katika
mabunge mengi duniani, na hasa yanayofuata mfumo wa Mabunge ya Jumuiya ya
Madola, wabunge wenye idadi ndogo bungeni wamekuwa wakifanya ushawishi kwa
wenzao walio wengi nje ya Bunge, ili hoja zao zenye maslahi mapana kwa sekta au
nchi kwa ujumla zifanikiwe.
Mjumbe
mmoja wa Kamati ya Uongozi ya Bunge inayoundwa na wenyeviti wa kamati za kudumu
za Bunge, pamoja na Spika, Naibu wake na Waziri Mkuu, amesema; “Siri ya hiki
kinachoonekana upendeleo ni kambi ya upinzani kushindwa kutumia mbinu za
mabunge ya Jumuiya ya Madola. Kanuni kuu ya kufanya uamuzi bungeni ni kuhoji
pande mbili zinazogongana katika hoja husika.”
“Kwa
mfano, Mnyika (John Mnyika- Mbunge wa Ubungo Dar es Salaam) ameleta hoja kuhusu
kuboreshwa kwa huduma ya maji safi na maji taka Dar es Salaam, Waziri wa Maji
Profesa Jumanne Maghembe ameleta hoja ya kutaka hoja hiyo iondolewa kwa sababu
kwanza Dar es Salaam imepewa bajeti kubwa ya kutatua tatizo hilo kuliko mikoa
mingine nchini.
“Sasa
ilibidi hizi hoja mbili zijadiliwe na wabunge na kisha uamuzi ufanyike, lakini
mwenendo wa mjadala inategemea nani alifanya vizuri kazi ya kushawishi wabunge
kabla ya kikao na hata wakati anapowasilisha hoja yake,” alieleza mjumbe huyo.
Wakati
mjumbe huyo wa kamati ya uongozi akisema hayo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika
kwa upande wake bado anaamini ameonewa na anakusudia kukata rufaa kupinga hoja
yake kutupwa bungeni.
Hatua
hiyo ya Mnyika inaungwa mkono na wabunge wengi wa Kambi ya Upinzani, ambao ni
pamoja na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na Mbunge wa Singida
Mashariki, Tundu Lissu ambaye ndiye aliyeongoza wabunge kusimama bungeni na
kuzomea kwa lengo la kuonyesha kupinga uendeshaji wa kikao cha Bunge uliofanywa
na Naibu Spika, Ndugai.
Lakini
kuhusu ushawishi Msigwa ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Maliasili na
Utalii, anasema; “Hoja za wapinzani zipo wazi kabisa, kwa nini ufanye lobbying?
Mimi nitawasilisha hoja binafsi kuhusu meno ya tembo kama kuna mbunge anahitaji
kushawishiwa ili aone umuhimu wa hoja hii wakati tembo wanauawa basi huyo ana
matatizo na hastahili kuwa mbunge.”
Msigwa
anaongeza: “Kwanza lobbying ni sawa na compromise, hivi mimi nijishushe na
kujipendekeza kwa Waziri Mkuu, au mawaziri wengine ili iweje? Si wao walioniingiza
bungeni na wala si wao watakaonirudisha bungeni. Ni bora nionekane kama
nilivyo, uhalisia wangu ujioneshe na si vinginevyo.”
Wakati
hayo yakiendelea, Naibu Spika Ndugai, ambaye ndiye aliyeahirisha Bunge juzi
Jumatatu kutokana na zomeazomea iliyofanywa na baadhi ya wabunge wa upinzani,
amemweleza mwandishi wetu akisema; “Kilichotokea ni kwamba, Mnyika alifuata
taratibu zote za kuwasilisha hoja binafsi, hoja hiyo ikapitishwa kwa taratibu
za Bunge na wabunge wote kupewa nakala ya hoja hiyo.
“Lakini
kabla hoja hiyo haijajadiliwa bungeni, Mnyika akawasilisha nyongeza ya
marekebisho, akitaka hoja yake ihusu tatizo la maji kwa upana zaidi na si Dar
es Salaam pekee. Marekebisho yake ni sawa na kuandika hoja nyingine mpya, kwa
hiyo kiutaratibu alitakiwa ama kuendelea na hoja yake ya zamani au kuleta hoja
mpya kwa kufuata taratibu za awali, yeye akaamua kwenda na hoja ya awali na
Waziri akaleta hoja yake kuhusu suala la maji nchi nzima akisema Dar es Salaam
imepewa bajeti kubwa kuliko mikoa mingine na miradi inaendelea kwa hiyo hoja ya
Mnyika iondolewe,” anasema Ndugai.
Alipoulizwa
ni kwa nini alimruhusu Waziri Maghembe kuchangia hoja ya Mnyika kwa zaidi ya
dakika 15 walizopewa wabunge wengine, Ndugai alisema; “Waziri alikuwa
akiwasilisha hoja yake kutaka hoja ya Mnyika iondolewe, kwa hiyo kwa utaratibu
alikuwa na nusu saa ya kufanya hivyo.”
Ndugai
alionyesha kusikitishwa na kitendo cha wabunge kuzomea bungeni, akisema ni
“uhuni usiokuwa na mafunzo yoyote kwa vijana wenye kiu ya kujifunza kuwa
viongozi bora wanaoshindana kwa hoja na si vihoja.”
Kwa
upande wake, Mbunge wa NCCR-Mageuzi, Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila
alisema anaunga mkono kitendo cha wabunge wa upinzani kusimama wote bungeni ili
kupinga uendeshaji wa kikao cha Bunge lakini haungi mkono tabia ya kuzomea na
kupiga kelele hovyo iliyofanywa na baadhi ya wabunge hao wa upinzani.
“Bunge
linaangaliwa na watu wengi wastaarabu na hata wapenda fujo, kuna viongozi wa
dini, maaskofu na mashekhe, wasomi na wasio wasomi, wanachotaka kuona ni
mvutano wa uzito wa hoja na si kelele za kuzomea, nadhani baadhi yetu tumevuka
kiwango,” alisema Kafulila.
Katika
hatua nyingine, taarifa zaidi zinaeleza kwamba kikao cha dharura cha Kamati ya
Uongozi ya Bunge kimemshambulia Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kwa
kudai kila anapokasimishwa madaraka na Freeman Mbowe kuongoza Kambi ya Upinzani
Bungeni, amekuwa akivuruga mwenendo wa mijadala.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka kamati hiyo ya uongozi, baadhi ya wajumbe wa kamati
hiyo wameshangazwa na wabunge wengine wa Kambi ya Upinzani kuburuzwa na Lissu
katika kila jambo bila kuchuja mambo hayo kwa kuzingatia uelewa wao binafsi na
si uelewa wa mtu waliyemwita mvurugaji wa mijadala bungeni.
Ni
kutokana na hali hiyo, inaelezwa kuwa baadhi ya wajumbe wanaamini mwenendo wa
Lissu kila anapoachwa kuongoza Kambi ya Upinzani Bunge si mzuri, akidaiwa
kutumia muda mwingi kukatisha wazungumzaji hata wale wa upinzani.
Vurugu za mabunge duniani
Vurugu
si tu za kuzomea bali hata za kupigana na kuharibu vifaa vya ukumbi wa Bunge
hutokea katika mabunge kadhaa duniani.
Kwa
mfano, Novemba mwaka 2008, vurugu zilizuka katika Bunge la Ukraine wakati
baadhi ya wabunge walipotaka kushinikiza kupigwa kura ya kumwondoa Spika wa
Bunge hilo, Arseniy Yatsenyuk.
Bunge
la Mexico pia liliingia katika rekodi ya vurugu, Desemba mwaka 2006, vurugu
hizo zilikuwa zikionyeshwa moja kwa moja (live) na kituo cha televisheni nchini
humo huku wabunge wakitwangana ngumi.
Juni,
2010 nchini Nigeria, ngumi zilipigwa baada ya baadhi ya wabunge kusimamishwa
ubunge kutokana na shutuma walizopata kuzitoa kwamba Spika wao alikula rushwa.
Bunge
la Korea Kusini ndiyo mara kadhaa limepata kuwa uwanja wa mpambano wa ngumi.
Machi, mwaka 1998, wakati wa upigaji kura za kumuidhinisha Waziri Mkuu Kim
Jong-pil, baadhi ya wabunge walirejesha karatasi tupu za kura zikiwa
hazikuandikwa chochote, na hapo ngumi zilianza baada ya baadhi ya wabunge
kutaka kura hizo zitambuliwe zimeharibika, na wengine wakibisha.
Zimewahi
pia kuzuka vurugu wakati wa jaribio la kutaka kumng’oa madarakani, Machi 2004,
Rais wa nchi hiyo, Roh Moo-hyun, wabunge wafuasi wa Rais wakitwangana na
wabunge wa upinzani.
Lakini
Julai, mwaka 2009, ngumi zilipigwa bungeni Korea Kusini baada ya kutokea
mvutano kuhusu Muswada wa Mabadiliko katika sekta ya vyombo vya habari.
Katika
mvutano huo, wabunge wa upinzani walitanda na kuzuia njia ya Spika kuingia
bungeni, na wabunge waliokuwa wakipinga kitendo hicho waliinuka na kuanza
mpambano, lakini hatimaye muswada huo ulipitishwa.
Huko
Taiwan, sehemu inayokusudia kujitenga na China ili iwe nchi rasmi
inayotambulika duniani, vurugu ziliwahi kutokea katika Bunge lao.
Huko,
mwaka 1995 iliwahi kuelezwa kwamba pengine baadhi ya wabunge wangepewa nishani
ya Nobel kwa kuwa mstari wa mbele kupambana kwa ngumi bungeni badala ya
kuchambua mambo kwa ajili ya kukabiliana na mataifa mengine katika masuala
mbalimbali, yakiwamo ya maendeleo.
Machi,
2004, vurugu ziliibuka kati ya wabunge wa upinzani na chama tawala, baada ya
kuwapo mvutano wa kutaka kura zilizopigwa wakati wa uchaguzi wa rais zirudiwe.
Lakini
Mei, mwaka 2004, wabunge Chu Hsing-yu na Lai Ching-teh, walitwangana ngumi
baada ya ubishi kuhusu taratibu za Bunge, huku vituo ya televisheni vikionyesha
Mbunge Chu, akimkwida mwenzake, Lai, huku akijaribu kumpiga ngwara.
Katika
Bunge la Uingereza imewahi kutokea wabunge wa upinzani na wale wa upande wa
utawala kuchorewa mstari wa kuwatenganisha bungeni kwenye zuria.
Mstari
huo mwekundu ulichorwa mbele ya mabenchi ya pande hizo mbili, mbunge wa upande
mmoja hakuwa akiruhusiwa kuvuka kwenda upande mwingine, ikihofiwa anaweza
kuvuka kwenda kumshambulia mbunge wa upande mwingine, na kwa wakati huo wabunge
walikuwa wakiruhusiwa kuingia na silaha bungeni.
Vurugu
nyingine zimewahi kutokea mwaka 1972 katika Bunge la Uingereza na mwaka 1976.
Marekani,
Februari mwaka 1798, kuliwahi kuzuka vurugu, msingi wake ukiwa ni katuni ya
kisiasa na hatimaye kuzua ugomvi kati ya wabunge Roger Griswold kutoka
Connecticut na Matthew Lyon.
Wakati
huo huo, mwandishi wetu Hafidh Kido anaripoti kwamba Katibu Mkuu wa CHADEMA,
Dk. Willbrod Slaa amewataka wabunge wa chama hicho kususia kikao cha Tume ya
Haki na Madaraka ya Bunge, ikiwa wataitwa kujieleza kutokana na mambo
yaliyotokea bungeni jana na juzi, hadi hapo Spika wa Bunge, Anne Makinda
atakapotoa hadharani matokeo ya rufaa kumi walizoweka tangu Makinda kushika
kiti hicho.
Akizungumzia
msimamo wa CHADEMA mbele ya waandishi wa habari katika Makao Makuu ya chama
hicho jana, Dk Slaa alitamka kulaani kiti cha Spika na wale wote wanaoendesha
majukumu yao katika Bunge la Tanzania kwa kufuata matakwa ya vyama vyao.
“CHADEMA
tunalaani kiti cha Spika na wale wote walioonyesha ubaguzi wa wazi katika
kuondoa hoja tatu za wabunge John Mnyika (CHADEMA), James Mbatia (NCCR-Mageuzi)
na Dk Hamis Kigwangala (CCM) kinyume na kanuzi ya Nane ya Bunge inayotamka
Spika hatakiwi kuwa na upande,” alisema Dk Slaa na kuongeza:
“Ninachotaka
kuwaeleza wabunge wangu wa CHADEMA, ikiwa wataitwa katika Tume ya Haki na
Madaraka ya Bunge wasiende. Wamweleze Anne Makinda wapi zilipo zile rufani 10
zilizokatwa na CHADEMA tangu aingie madarakani. Kwanza watoe majibu ya rufani
hizo tulizokata, tena mbele ya ukumbi wa Bunge baada ya hapo wabunge wangu
watakuwa tayari kusimamishwa mbele ya tume hiyo.
“Kinachotokea
sasa bungeni mjini Dodoma ni kuendesha vikao vya Bunge kwa chuki, uongo na
kutofuata haki. Bunge ndiyo sehemu ya kupatikana haki na kutungwa sheria lakini
pamegeuka kichaka cha udhalilishaji, uovu, chuki na ubaguzi wa kichama.
“Enzi
za uspika wa Samwel Sitta kulikuwa na ubabe kidogo lakini namsifia Sitta kwani
hakupenda kupindisha haki na kanuni za bunge ni bora Sitta angeendelea kuwa
Spika ni mtu makini sana. Bunge haliwezi kuwa na haki wacha nikuchekeshe kamati
ya uongozi wa wabunge wa CCM ina wajumbe 18 ambao ni viongozi wa kamati kuu ya
chama chao. Katika kamati hiyo hata maspika wanaingia hoja zote zinazotakiwa
kujadiliwa katika kikao cha bunge lazima zijadiliwe na kamati hiyo ya wabunge
18 wa CCM unadhani lini haki itapatikana, lazima tuzichukue hoja zetu na
tuzipeleke kwa wananchi na tukifanya hivyo wasituite wachochezi.”
Source: Raia Mwema
No comments:
Post a Comment