Ndugu zangu,
Delirium ni hali ya mwanadamu kuwa katika mkanganyiko ( kuchanganyikiwa). Ni maradhi.
Tunayoyashuhudia sasa ni dalili za kuwa tumo kwenye hali ya Mkanganyiko- Delirium.
Maana, ukiona wanafunzi wa Form Four wanaambulia sifuri kwa malaki ni Mkanganyiko. Ukimwona Waziri Mkuu wa Nchi anaacha majukumu mengine na anahangakia kusuluhisha mgogoro wa nyama ni Mkanganyiko .
Ukimwona Babu wa Loliondo anawafanya Watanzania kwa mamilioni kuacha mambo ya msingi na kujadili kikombe chake cha kitapeli ni Mkanganyiko.
Ukiwaona Watanzania kwa mamilioni wanaacha mambo ya msingi na kujikita kwenye ujinga wa kuamini kuna Freemasons na utajiri wa njia za mkato ni Mkannganyiko. Mlolongo ni mrefu, wa dalili za mikanganyiko ya kitaifa.
Ndio, ni heri ya giza la Tanesco kuliko giza hili la elimu ambalo Taifa limegubikwa nalo. Ni giza la mchana na usiku. Ni lenye madhara ya muda mrefu. Tuna lazima ya kuchukua hatua za haraka.
Kiwango hiki cha kutisha cha vijana wetu kufeli vibaya mitihani ya Form Four ni sawa na ajali nne za MV. Bukoba kwa mwaka mmoja.
Na tunachokiona ni kichuguu cha janga, hatujaufikia mlima.
Enzi zile tulikuwa tukimsoma mwandishi mahiri Elvis Musiba. Wengi wa kizazi changu hatukukosa hata kitabu kimoja cha Elvis Musiba; ni kuanzia ' Kikosi Cha Kisasi', ' Njama' hadi ' Hujuma'.
Elvis Musiba kupitia Willy Gamba, alichangia sana kutujengea uwezo wa kufahamu masuala mazito ya kitaifa na kimataifa. Alichangia pia kutujengea mioyo ya uzalendo.
Swali ni hili; " Hivi vijana wetu wa leo Willy Gamba wao ni nani?
Nahofia, kuwa vijana wetu wamezama tu kwenye maandiko mepesi ya kwenye majarida ya udaku. Hayawasaidii hata kufikiri mambo ya msingi. Wanaishia kwenye porojo za Freemasons na matamasha ya Bongo Fleva. Na baadhi ya walimu ni zao hilo hilo. Kwa nini basi tunazishangaa sifuri hizi tunazozifuna kwa magunia ya kujaza mabohari?
Na kwa akili zetu nyepesi. Kuna hata wanasiasa watakaokimbilia kuvuna ponti za kisiasa hata kwa kutamka hadharani; kuwa haya matokeo mabaya ya Form Four ni ' Njama' za mabeberu wa nje ya mipaka yetu wanaowatumikia mamluki wa ndani ya nchi!
Nimemkumbuka mwandishi Elvis Musiba. Na kama angekuwa hai, huenda angemleta tena Willy Gamba kwenye kitabu cha ' Mkanganyiko'. Willy Gamba angetusaidia kufanya upepelezi wa kizalendo ili kuja na ' Siri ya Sifuri!'- Nacho kingeweza kuwa kitabu kingine.
Angetusaidia kupata majibu ya kwanini, ile Tanzania iliyosifika kwa kujaa raia wazalendo, majasiri na wenye ufahamu mkubwa wa mambo leo inazalisha vijana wenye kuambulia malaki ya sifuri kwenye mitihani yao.
Tungepata majibu ya walikopotelea viongozi- makamanda wa mapinduzi ya ukombozi wa kifikra. Kwanini hawazaliwi wapya? Badala yake, tuna lundo la viongozi- makomamanga- si makamanda.
Ndio hawa wanaoilisha jamii fikra za kikomamanga; ni fikra hizi za udini, ukabila na ubaguzi hata wa rangi. Na matokeo ya Form Four ni matokeo ya kuachana na mambo ya msingi ya kulijenga taifa letu kwa pamoja na kukimbilia kwenye siasa za rejaraja-siasa za kikomamanga.
Ndio msingi pia wa Mkanganyiko huu wa Kitaifa- Delirium.
Na hilo ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam.
0788 111 765
http://mjengwablog.co.tz/
No comments:
Post a Comment