Ndugu zangu,
Wanazuoni wa Kiislamu ni wenye kufahamu zaidi juu ya kisa kifuatacho nilichokipokea miaka mingi iliyopita. Hivyo, wanaweza kukiboresha zaidi.
Inasimuliwa, kuwa katika wakati wake, Mtume Muhammad (S. A. W) alipata kupokea makusanyo ya zakka kutoka kwa mjumbe wake.
Mjumbe yule katika kupita kwake na kukusanya zakka, huko alipewa pia zawadi mbali mbali. Basi, alipofika kwa Mtume na kukabidhi zakka, akaweka kando zile zawadi alizopewa na waja wa Mwenyezi Mungu. Akakabidhi tu kile alichoambiwa akusanye kama zakka.
Mtume akamwambia; kuwa na zile zawadi alizopewa nazo anapaswa kuzikabidhi kwenye mamlaka ili ziingizwe kwenye hazina kuu.
Maana, mjumbe yule asingeweza kupewa zawadi zile kama asingetumwa na mamlaka kwenda kukusanya zakka.
Inahusu maadili ya kiuongozi.
Mjumbe yule alitanguliza ubinafsi. Kuna cha kujifunza kutoka kwenye simulizi hii.
Ndugu zangu,
Kwenye gazeti la Mwananchi la hii leo nimeandika juu katuni ya HakiElimu na kisa cha Mkurugenzi aliyerudisha fedha hazina.
Ndio, kwenye moja ya machapisho ya Shirika la Haki Elimu kuna katuni inayoonyesha walichokiita kitendo cha ajabu pale Halmashauri ya Wilaya ya Urambo kwa bajeti ya mwaka 2009/2010 ilipobakisha kiasi cha shilingi milioni 68 kati ya shilingi milioni 188 zilizotengwa kwa ajili ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi wakati shule hazina walimu, madarasa, madawati, vitabu, nyumba za walimu, vyoo na maabara.
Katuni ile haiwezi kupita bila kujadiliwa, maana, yaweza pia kuwa ni yenye kupotosha pale inapoonyesha ajabu ya ‘ Mkurugenzi’ anayerudisha fedha hizo hazina huku akitamka; “ Katika zile mlizonipa kwa ajili ya Maendeleo ya Elimu ya hao... hizi zimebaki!” Katuni ikaonyesha pia kuwa anachofikiri ni; “ Najua nitapandishwa cheo!”
Kwa haraka mtu anaweza kufikiri kuwa ‘ Mkurugenzi’ hakuwa ni mtu anayejali wananchi wake, na kuwa kitendo chake cha kurudisha fedha iliyobaki hazina kinaonyesha kuwa ni mtu asiyefaa.
Lakini, tunaweza pia kutafsiri kitendo cha Mkurugenzi na kiwango cha juu cha uadilifu, pale, fedha ambazo zilitengewa jambo fulani zimebaki zinapaswa kurudishwa hazina kwanza kabla ya Halmashauri kuamua kuzitumia kwa mambo ambayo hayakuwekewa bajeti.
Maana, hilo pia ni moja ya mapungufu ya watendaji wetu, kufanya matumizi kwa mambo ambayo hayapo kwenye bajeti . Hutokea pia, fedha zinapobaki, watendaji huamua kuzitumbua hata kwa kufanyia sherehe ilimradi zisirudi hazina.
Cha hazina kinapobaki kinapaswa kurudishwa hazina, ndipo kitolewe tena kutoka hazina, kwa utaratibu. Ndio mifumo ya Kiserikali na kitawala inavyotaka. Na npyo uadilifu wa kiungozi unavyotaka.
Na hilo ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
No comments:
Post a Comment