SIKU zinazidi kusogea huku tambo za kisiasa zikizidi
kuhusu nafasi ya vyama vya siasa katika uchaguzi mkuu wa 2015. Tambo hizo hasa
ni kwa vyama vikubwa – CCM na Chadema.
Chadema kimeanza kuandaa mashambulizi ya kuchukua madaraka ya
nchi kutoka mikononi mwa CCM, lakini hiyo haitakuwa kazi rahisi kwa kuwa CCM
nayo inaelekeza mashambulizi kwa Chadema kama chama, na wanachama binafsi, hasa
Dk Willibrod Slaa ambaye jina lake limeendelea kusimama kama alama ya chama
hicho.
Chama hicho kimetokea kuwa ni mwiba mkali kwa CCM, na kuwa
kivutio kwa idadi kubwa ya vijana kutokana na ushawishi unaojidhihirisha kutoka
kwa wabunge na makamanda wa chama hicho.
Mbali na ushawishi huo, pia chama hicho kimekuwa kikijivunia
mipango yake mahususi, kama operesheni za ujenzi wa chama, kurudisha madaraka
kwa wanachama kupitia Sera yake ya majimbo na shughuli zingine.
Januari 27 na 28, mwaka huu chama hicho kimefanya vikao vyake
vya juu – Kamati Kuu na Baraza Kuu – na kujadili ajenda mbalimbali ikiwa ni
sehemu ya mkakati wa kuhakikisha kinashinda Uchaguzi Mkuu 2015.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho,
John Mnyika hatua iliyopo ni kuzingatia uamuzi ya kuwapata viongozi na kuweka
mpango kazi wa kuongeza nguvu ya umma.
“Tunaanza ujenzi wa chama ili kujiimarisha zaidi katika harakati
za kushinda uchaguzi mkuu ujao, lakini pia tunajiweka sawa kwa namna
tutakavyosimamia ahadi zetu za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kwa kuishinikiza
Serikali kutekeleza,” anasema Mnyika. Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama
hicho, Freeman Mbowe ametangaza vita ya kisiasa, akisisitiza kuwa “Mwaka 2013
ni mwaka wa nguvu ya umma.”
Anasema chama hicho kimeweka mikakati ya kujijenga kuanzia
matawi hadi taifa na kutawashughulikia wanachama wanaodaiwa kutumiwa na CCM
kuanzisha migogoro ndani ya chama.
Kauli hiyo ya mwenyekiti, ni kinaashiria kuwa ndani ya chama
hicho kuna migogoro ambayo isipoangaliwa na kutatuliwa katika kipindi hiki,
wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema inaweza kuwa kikwazo kwa harakati na
mipango yake ya kushika dola.
Uamuzi kufuata Katiba
Profesa Chris Maina wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema
Chadema inapaswa kuhakikisha inafanya uamuzi na kutekeleza mipango yake kwa
kufuata Katiba, ili kuhakikisha inaendelea kuimarika zaidi mpaka kufikia
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Anasema endapo migogoro inayodaiwa kuwamo itaendelea ndani ya
chama hicho, na chenyewe kikafanya uamuzi bila kufuata katiba yake, basi
hakutakuwa na mafanikio ndani ya chama hicho.
“Ninachoamini
mimi wanatakiwa kutekeleza mipango yao kwa kufuata katiba, ndio inayoweza
kuwaongoza wakasimamia misingi yao, hata migogoro na mivutano haitaweza
kujitokeza, mhimili wa chama ni makubaliano ya kufuata misingi na kanuni ya
katiba,” anasema Profesa Maina.
Uteuzi
usio wa haki
Jambo
lingine ambalo anasisitiza Profesa Maina linalotakiwa kuepukwa ni makosa katika
uteuzi wa wagombea katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika, ili kujenga dhana ya
uaminifu kwa Watanzania wanaotakiwa kutenda haki katika uchaguzi huo.
Profesa
Maina anasema endapo chama hicho kinahitaji kufanikiwa katika uchaguzi mkuu
ujao, kinapaswa kumchagua kwa umakini kiongozi wanayeamini kuwa atastahili
kusimama katika uchaguzi mkuu.
“Waangalie
mfano wa Kenya na vyama vingine, utakuta mgombea mwingine hakubaliki kwa
wananchi lakini anakubalika ndani ya chama, na mwingine hakubaliki kwenye chama
chake lakini ndio anayeonekana kipenzi cha wananchi, anasema Profesa Maina bila
kutaja majina.
Mbinu
za CCM
Mkazi
na mfanyabiashara wa Dar es Salaam, Alfani Mohamed anasema chama hicho
kinapaswa kuwa makini na mbinu mbalimbali zinazotoka upande Chama Cha Mapinduzi
(CCM), kwani kumbukumbu zinaonyesha kuwepo kwa vyama vilivyowahi kuwa na nguvu
na baadaye kudhoofishwa.
“Kuna
vyama viliundiwa njama mpaka leo vimeshakosa nguvu tena, kulikuwa na NCCR-
Mageuzi baadaye kikafuata CUF, lakini viko wapi kwa sasa, kuna utekelezwaji wa
mbinu kabambe za kuvidhoofisha kwa hali na namna yoyote,” anasema Mohamed.
Mfumo
wa uchaguzi
Moja
ya vikwazo vinavyoweza kukwamisha ndoto za Chadema ni kutokuwapo uhuru kwa Tume
ya uchaguzi iliyopo sasa, ambayo mwenyekiti, watendaji na makamishna wake
wanateuliwa na Rais ambaye ni mwenyekiti wa chama shindani.
Kiongozi
wa kituo cha madereva wa taksi, Tabata, Kanaluza Abdi anasema mfumo huo ni
tatizo linaloweza kuondoa imani ya wapigakura kwa kuona haki haiwezi kutendeka.
“Kama
mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi amechaguliwa na Rais ambaye pia ni mhusika
katika uchaguzi, sio rahisi kupata matokeo mazuri, labda Katiba ibadilishe
suala hilo kabla ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu wa 2015, vinginevyo Chadema
haitaweza kuchukua nchi,” anasema Abdi.
Muundo
wa chama
Mfanyabiashara
na mkazi wa Buguruni, Dar es Salaam, Mohamed Salim (27) anasema kuna uwezekano
mkubwa wa Chadema kushindwa kwenda Ikulu kutokana na muundo wake kwa sasa.
Anasema
chama hicho bado hakijashuka hadi chini kwa wananchi, kipo mijini tofauti na
CCM ambacho kimejikita zaidi katika mashina ya vijijini.
“CCM
bado wana mashina mengi vijijini ukienda mpaka leo kuna watu wanaamini na
kusema CCM ikiondolewa madarakani kuna vita itatokea, dhana hiyo ni kwa sababu
ya kukosa elimu, unadhani mpaka kizazi hicho kitoweke ni lini,”anahoji Abdi.
Idadi
ya wapiga kura
Kwa
mujibu wa Alfani Mohamed, asilimia kubwa ya wapigakura wanaoiunga mkono Chadema
wengi ni vijana, wakiwamo walio na sifa na wasio na sifa ya kupiga kura.
Anasema
kumbukumbu zinaonyesha kuwa wanawake na wazee ndio hujitokeza katika kipindi
cha uchaguzi kupiga kura, tofauti na vijana ambao huonekana mstari wa mbele
katika mikutano ya kampeni.
“Uchaguzi
uliopita kulikuwa na watu karibu milioni 19 waliojiandikisha, lakini kwenye
matokeo ikabainika ni asilimia 42 tu kati hao ndio walijitokeza, sasa ukiuliza
unaambiwa vijana ndio wengi hapa nchini, sasa sijui huwa wanakwenda wapi wakati
wa kupiga kura,”anahoji Mohamed.
“Endapo
vijana watahamasika kupiga kura, Chadema wakasimika matawi vijiji vyote nchi
nzima na elimu ikatolewa juu ya umuhimu wa kura ya Mtanzania, katika uchaguzi
huo wa 2015, Chadema itachukua nchi, ila naona muda uliobakia si haba,” anasema
Abdi.
Ahadi
zisizotekelezeka
Hata
hivyo, kada mmoja wa CCM, Paul Makonda anasema chama hicho kina tatizo la
kutangaza ahadi zenye matumaini hafifu ya kutekelezeka na kuwafanya watu
wajenge hofu katika utekelezaji wake.
Makonda
anasema ahadi hizo zinajenga tafasili ya Chadema kuonyesha shauku ya kutamanani
kuingia madarakani badala ya kuangalia njia mbalimbali za kuisaidia jamii kabla
ya kuingia madarakani ili kujijengea uaminifu zaidi. “Angalia mfano, utaona mara nyingi wao wanatumia mianya ya changamoto
kama daraja la kujijengea umaarufu, utakumbuka, migomo ya walimu, madaktari na
sasa hivi wamehamia Mtwara, haijawahi kutokea Chadema wakahamisha wananchi
kutii sheria za nchi au kuandaa makundi ya kuelimisha kwa mambo mbalimbali,”
anasema Makonda.
SOURCE: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment