WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, February 13, 2013

Hakuna siri



MAJUZI nikiwa Dodoma nilipata bahati ya kuzungumza na Maofisa Habari na Mawasiliano wa Serikali na Mawakala wake kutoka Tanzania nzima.
Mada yangu ilihusu Matumizi ya Mitandao ya Kijamii na Changamoto zake. Na ni kwa namna gani maofisa habari hao wangeweza, kwa ufanisi kutumia mitandao hiyo katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku ya kuupasha umma habari.
Changamoto kubwa ambayo niliiweka wazi ni hulka ya kizamani ya kuficha taarifa. Kwamba kuchelewa kufikishwa kwa taarifa sahihi kwa umma kutoka upande wa Serikali, huchangia pia kwenye mikanganyiko katika jamii. Nikatoa mfano wa vurugu za Mtwara, kuwa, kwa kiasi kikubwa zimechangiwa na hali niliyoielezea hapo juu.
Katika hili la kuficha taarifa sahihi, na wakati mwingine kutanguliza propaganda kwa maana ya uongo, nilitoa mfano wa kisa cha Urusi ya zamani.
Kwamba enzi za Ukomunisti kule Urusi ya zamani (Soviet Union) kulikuwa na magazeti mawili makubwa; Pravda na Izvestia, ikiwa na maana ya Ukweli na Habari.
Na Urusi kulikuwa na utani mitaani; kwamba kwenye Pravda hakukuwa na ukweli wowote ulioandikwa, na kwenye Izvestia hakukuwa na habari!
Na kwa kiasi kikubwa watu wa mitaani hawakutania. Huo ndio ulikuwa ukweli wenyewe. Chama cha Kikomunisti kiliendesha zaidi propaganda. Na tafsiri sahihi ya propaganda ni uongo.
Na propaganda maana yake haswa ni uongo unaorudiwa rudiwa sana hadi pale jamii inapoamini kuwa ni ukweli. Kule Soviet Union, kitengo cha propaganda kwenye Chama Cha Kikomunisti kilikuwa na kazi moja kubwa; kusambaza uongo.
Na anayeajiriwa kufanya kazi hapo lazima moja ya sifa zake ziwe ni umahiri wa kusema uongo. Kwamba hata kama kinachoonekana na kila mmoja kuwa ni jiwe, mtu wa propaganda anaweza kusema hilo si jiwe, ni mchanga uliolundikana na kufanya kichuguu.
Na atarudia rudia kusema hilo mpaka pale wengine mtakapoanza kuamini kuwa mnaloliona mbele yenu si jiwe ni ' mchanga uliolundikana'!
Na ukweli una sifa moja kubwa, kuwa hata ukifichwa chini ya uvungu wa kitanda kwa miaka 50 ( nusu karne) , iko siku, utatoka na kutembea hadharani wenyewe. Hautasubiri kuvalishwa viatu.
Ndugu zangu, wanadamu tunahangaika sana kutaka kutunza siri. Niwaambie, katika maisha hakuna siri. Na kama zipo, ni chache sana.
Inasemwa, kuwa siri ni ya mmoja. Lakini tazama, hata mmoja huyo anaweza kuweweseka na siri ya moyoni mwake.
Na mara ile atakapomnong'oneza mwenzake, basi, kuna unafuu atauona. Ukweli ni huu, kuwa hata kwenye maisha haya tunayoishi, siri ni chache sana.
Ndiyo, ni wanadamu wachache sana wenye siri na wakazitunza. Hivyo, wanadamu tunapoteza muda na nguvu zetu nyingi sana katika kujifanya tunatunza siri. Ni kazi bure.
Duniani kuna wenye kusema wasiyomaanisha, na kuna wasiomaanisha wanayosema. Haya ni mawili tofauti. Na wenye kuyatenda wanadhani kuna wanachoficha. Kuwa wana siri. Hapana, wanajidanganya. Hivyo, ni waongo tu.
Mara nyingi nakutana na watu wenye kutamka; " E bwana ee, jambo nililokueleza ni siri, usimwambie mtu!" Na jambo hilo hilo unaweza kuambiwa na mwingine, kwa staili hiyo hiyo, kuwa ni la siri!
Wanachoshindwa wengi kutofautisha ni hiki; muhimu na siri. Lililo la muhimu, na pengine nyeti, si lazima liwe la siri. Nahitimisha
Source Raia Mwema: Maggid Mjengwa

No comments:

Post a Comment