HALALI
mtoto kufanya mambo ya kitoto, marufuku kwa mtu mzima.
Tofauti
kati ya udogo na ukubwa haielezeki kwa umbile wala ‘saizi.’ Wapo watu wadogo wa
mwili ambao ni wakubwa na pia wapo watu wenye miili mikubwa ambao bado ni
wadogo, kwa umri, tabia na jinsi wanavyotenda mambo yao.
Tunapokuwa
wadogo tunakuwa na haki ya kutenda mambo madogo, mambo ya kitoto, na wazazi na
wakubwa zetu wanatuvumilia huku wakituelekeza kwa sababu wanajua kwamba bado tu
wadogo, bado tunakua na tutaachana na tabia hizo tutakapokuwa tumefikia utu
uzima.
Dalili
za kusogea mbele na kukua, kutoka hali ya utoto na kuelekea utu uzima, pia
huonekana. Mtoto hufikia umri wa kutumwa dukani, kuchunga mbuzi, kwenda shule
ya karibu, kwenda shule ya mbali, na hatimaye kuondoka nyumbani kwa wazazi wake
kabisa.
Utoto
una raha zake, na hizi hazipatikani kwingineko isipokuwa utotoni. Tulifundishwa
tukiwa wadogo kwamba “Watoto hucheza ni sentenso” kwa maana kwamba
inajitosheleza kwa nomino na kitendo lakini pia kwa sababu ina mantiki kwamba
ada ya watoto ni kucheza. Mtoto asiyecheza ni chanzo cha shauku kubwa kwa
wazazi wake ( anaweza kuwa anaumwa) na mtu mzima asiyeisha kucheza anawafanya
wanaomuangalia wajiulize kama akili yake iko sawa.
Katika
utoto, hata matendo yanayojithibitisha kwamba si ya haki yanaelezeka kwa sababu
ni ya utotoni na utotoni watoto hutenda kama watoto watendavyo utotoni. Kwa
mfano, ipo tabia ya kunyang’anyana wakati wa mlo, mara nyingi ukiwa ni mlo wa
pamoja, watoto wakilizunguka sinia la wali au ugali, huku macho yote yakiiangalia
minofu michache ya nyama iliyopo.
Kwa
sababu nyama inakuwa ni tunu katika mazingira yetu halisi, kila mtoto anaweka
‘akiba’ yake ya nyama ili aile pale wali au ugali utakapokuwa umeisha na aweze
kuwaringia wenzake waliomaliza kitoweo chao mapema. Zahma inayompata mtoto
‘mjanja’ kama huyo ni kwamba mlo unapokaribia mwisho hutokea binamu mkubwa
miongoni mwa watoto wale, akalikumba sinia, pamoja na wali au ugali uliosalia,
na nyama zote zilizowekwa ‘akiba’ kisha akakimbia na kwenda kula peke yake.
Zogo
linalotokea pale huishia pale pale, na hakuna mtu mzima atakayeshughulishwa mno
na tukio hili, kwa sababu ni mambo ya kitoto, na watoto wakikua wataachana na
michezo hiyo.
Watoto
hucheza michezo ya “baba na mama,” wakiigiza ndoa na harusi, mara nyingi wakiwa
faragha, kwa maana kwamba hakuna mtu mzima anayewaona. Mchezo kama huo hauna
madhara kwa sababu watoto wanafikiria ni nini baba na mama huwa wanafanya
wanapokuwa faragha. Wakigundulika wanachapwa, lakini wasipogundulika ni raha
tupu.
Na
michezo hii nayo ina ukomo wake. Ni marufuku kwa kijana aliyebalehe kucheza
mchezo huu, kwa sababu umri wake haumruhusu kucheza michezo ya kitoto, na sasa
anatakiwa ajiandae kucheza michezo ya kikweli ya “baba na mama.” Kadhalika,
michezo ya kutega ndege, kurusha tiara (kishada) na “mchezo wa kalinge
kanyama”. Ni michezo wafanyayo watoto wakati wanakua kuelekea utu uzima.
Utoto
pia hujumuisha adha mbali mbali ambazo ukubwani hutoweka. Watoto wengi hukumbwa
na tatizo la kukojoa kitandani, na huchapwa na wazazi wao kwa sababu ni tabia
inayoudhi na inayosababishwa na uvivu wa kuamka inapobidi kwenda haja ndogo.
Tatizo hili nalo hutoweka mtoto anapokuwa kijana, na ni zahma kubwa iwapo mtoto
ataendelea kulowesha matandiko baada ya kuwa amebalehe.
Hata
kuangukaanguka ni sehemu ya utoto. Mtoto anahitaji muda wa kuyajua mazingira
yake, tokea ndani ya nyumba ya wazazi wake hadi viwanja anakokwenda kucheza.
Uwezo wa kutambua mazingira hatarishi, kama vile utelezi, bado ni mdogo.
Inabidi aanguke mara nyingi kabla hajatambua ni wapi kuna utelezi, ili afanye
hadhari kila anapokanyaga sehemu hiyo.
Baada
ya muda tatizo hili pia huisha, na mtu mzima anayeonekana akidondoka hovyo
anajulikana kama aliyelewa au mgonjwa. Binafsi nakumbuka kwamba kwenye umri
fulani nilisema kimoyomoyo, " Lo, siku hizi sianguki tena !" Ilikuwa
ni ishara ya kukua.
Si
watoto wote hunyonya kidole, lakini wale wanaofanya hivyo huwapa shauku kubwa
wazazi wao, ambao hufanya jitihada za kila aina kuwafanya waache tabia hiyo. Ni
tabia ya utoto ambayo ikionekana kwa mtu mzima itakuwa ni kioja, ni balaa.
Matamanio
ya watoto nayo pia huendana na hali ya utoto. Utamu wa peremende, soda, keki,
andazi, kitumbua na ‘shikilimu’ ni utamu wa utotoni. Nilipokuwa mtoto niliweka
nadhiri kwamba nikikua na nikapata fedha ningenunua peremende, mandazi, keki na
vitumbua, nile hadi nivimbiwe. Hamu hii ilinitoka kabla hata sijapata mshahara
wangu wa kwanza. Utu uzima ulileta matamanio mapya, tofauti kabisa.
Kupenda
kubembea pia ni tamanio la utotoni. Tunapokuwa wadogo mama zetu hutubelembeza
kwa kuturusharusha. Siku hizi bembea zinatengenezwa China na zinapata soko
kubwa kwetu, kwa sababu mtoto anaona raha kubwa anapobembea. Akiisha kuwa
mkubwa atakutukana ukimwambia apande kwenye bembea, jambo la kitoto. Mtu mzima
anayependa kubembea anasumbuliwa na taahira ya akili.
Yapo
mambo mengi ambayo yanajulikana kwamba yanahusiana na utoto, na watoto wengi
huyapitia bila kupata lawama kubwa, kwa sababu yanatambulika kama sehemu ya
awamu mahsusi ya makuzi. Kadri mtoto anavyobadilika na kuwa kijana, na kisha kijana
akawa mtu mzima ndivyo tabia hizi zinavyotakiwa kupungua, kufifia na mwisho
kutoweka kabisa, ili mtu mzima atende mambo ya utu uzima. Hili lisipotokea,
jamii itajua kwamba mtu huyo, pamoja na utu uzima wake, amevia. Vivyo hivyo kwa
taifa pia.
SOURCE:
RAIA MWEMA: Jenerali Ulimwengu
No comments:
Post a Comment