UCHAGUZI wa wajumbe wa
Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) uliofanywa na Halmashauri Kuu (NEC) ya
chama hicho Jumatatu wiki hii mjini Dodoma, ni kama unabadili mwelekeo wa siasa
za ndani za chama hicho kikongwe nchini.
Tangu Rais Jakaya Kikwete aingie madarakani miaka saba iliyopita
na kupewa kofia ya uenyekiti wa CCM, chama hicho kimekuwa kwenye minyukano ya
siasa za visasi kiasi kwamba hakijawahi kuwa na utulivu wa kisiasa kama ilivyo
sasa, miezi michache baada ya kufanyika mabadiliko kadhaa ya kiuongozi.
Uteuzi na baadaye uchaguzi wa wajumbe wa Kamati Kuu umeweka
kando baadhi ya vigogo wa kisiasa hasa waliokuwa wakitajwa katika harakati za
kuusaka urais katika uchaguzi wa 2015 na kuziingiza sura mpya ambazo huenda
baadhi yao wanaweza kuingia katika kinyang’anyiro hicho.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta ni vigogo ambao wamekuwa wakitajwa kupiga mbio hizo,
lakini waliwekwa kando katika Kamati Kuu ya sasa.
Pia majina ya mawaziri na wizara zao kwenye mabano Profesa Mark
Mwandosya (Ofisi ya Rais – Kazi Maalumu), Dk John Magufuli (Ujenzi), Dk
Harrison Mwakyembe (Uchukuzi) pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba na Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela, pia
hayakuwa sehemu ya waliopendekezwa kuingia katika CC ambacho ni chombo cha
kufanya uamuzi mkubwa ndani ya CCM.
Profesa Mwandosya licha ya kuwa na matatizo ya kiafya, amekuwa
akitajwa kuwa mmoja wa watu muhimu katika mustakabali wa siasa za sasa za
Tanzania wakati Dk Magufuli na Dk Mwakyembe wamekuwa wakipigiwa chapuo na umma
kwamba huenda wangefaa kuwania urais kutokana na kasi katika utendaji kwenye
wizara wanazoziongoza.
Badala yake Kamati Kuu inawajumuisha makada ambao siyo wapya,
lakini ambao wanaweza kutumika kubadili sura na mwelekeo wa siasa ndani ya CCM
hasa tunapoelekea 2015, akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Dk Salim Ahmed Salim.
Hatua hiyo inaweza kuwa ni hatua ya kujaribu kujipanga kwa CCM
katika kuzipa sura mpya siasa za ndani ya chama hicho. Dk Salim kama ilivyo kwa
Profesa Mwandosya, alikuwa mpinzani wa Kikwete katika kinyang’anyiro cha urais
wa 2005, ambaye bado anatizamwa kuwa mtu mwenye uwezo licha ya kwamba umri wake
ni mkubwa.
Wengine ambao kuingia kwao katika Kamati Kuu ya CCM kunaweza
kuwa na maana ya kubadili siasa za urais ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein
Mwinyi na mwenzake kutoka Tanzania Visiwani ambaye alipata kuwa Waziri Kiongozi
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Shamsi Vuai Nahodha.
Dk Nchimbi anarejea Kamati Kuu ambako aliingia kwa mara ya
kwanza akiwa na umri mdogo pale alipochaguliwa kuongoza Umoja wa Vijana wa CCM
(UVCCM) na kuongoza jumuiya hiyo kwa miaka kumi mfululizo. Kwa mujibu wa kanuni
za CCM, wenyeviti wa jumuiya za chama huwa ni wajumbe wa CC kwa mujibu wa
nyadhifa zao. Nchimbi amekuwa mjumbe wa CC kwa mi
aka 10.
Hali kadhalika, Dk Mwinyi ni mmoja wa makada wa CCM ambaye
amekuwa ndani ya CC kwa muda mrefu, wakati Nahodha alikuwa akiingia ndani ya
kamati hiyo alipokuwa Waziri Kiongozi wa SMZ (kwa wadhifa wake).
Nahodha, Dk Mwinyi na Dk Nchimbi kwa nyakati tofauti wote
wamepita katika wizara nyeti ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Dk Mwinyi
wakati alipokuwa waziri, naibu wake alikuwa Dk Nchimbi ambaye baadaye
alihamishiwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na sasa Mambo ya
Ndani.
Dk Nchimbi alichukua nafasi ya Nahodha ambaye sasa yupo ulinzi.
Mwingine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Sera na Uratibu), Steven Wassira ambaye katika siku za karibuni ametokea kuwa moja ya nguzo kuu za CCM katika kujibu hoja mbalimbali ndani na nje ya Bunge, kusuluhisha migogoro ya kichama na kupambana na wapinzani wakuu wa chama chake, ambacho ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Mwingine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Sera na Uratibu), Steven Wassira ambaye katika siku za karibuni ametokea kuwa moja ya nguzo kuu za CCM katika kujibu hoja mbalimbali ndani na nje ya Bunge, kusuluhisha migogoro ya kichama na kupambana na wapinzani wakuu wa chama chake, ambacho ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Wassira
aliongoza kwa kupata kura nyingi miongoni mwa makada wa CCM waliochaguliwa kuwa
wajumbe wa NEC kupitia uchaguzi wa kitaifa, lakini amekuwa akitajwa kwamba ni
mmoja wa wanaokusudia kuchukua fomu za urais katika uchaguzi wa 2015.
Katika
mazingira ya kawaida hii ni CC mpya ya mwisho kuundwa na Rais Kikwete akiwa
Mwenyekiti wa CCM kwani ndiyo inayotazamiwa kukivusha chama hicho katika
kinyang’anyiro cha 2015 ambacho yeye hatogombea kwani atakuwa amemaliza muda
wake.
Umekuwa
ni utaratibu wa CCM kwamba ni vigumu kumteua mgombea urais ambaye si mjumbe wa
Kamati Kuu na kitendo cha baadhi ya vigogo wa kisiasa kuwekwa kando kunaweza
kutafsiriwa kwamba ni kuwaweka kando katika kuwania nafasi hiyo na kuwapa fursa
makada wengine ambao wanaonekana kuwa ‘watulivu’.
Licha
ya kwamba Rais Kikwete ni mwenyekiti, lakini uwapo makamu wake, Philip Mangula
na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kunakipa nguvu chama hicho
kuendeleza utulivu uliopo na kupitia kwao, CCM wanaweza kufanya uamuzi mgumu
ambao utawashangaza wengi kwa kumteua mgombea ambaye hafikiriwi na wengi
kupeperusha bendera ya chama hicho.Pia aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa, Asha-Rose Migiro ambaye ameteuliwa hivi karibuni katika sekretarieti mpya,
naye amekuwa akitajwa kwamba huenda akachukua fomu ya kugombea urais katika
chama hicho.
Kwa
upande wa Dk Mohammed Shein naye huenda akachukua fomu ya kugombea urais wa
Muungano baada ya kuweza kufanya kazi na upinzani bila ya mikwaruzo mikubwa
huko Zanzibar. Hata hivyo, CCM kama itatupa karata yake kwa Dk Shein itabidi
kufanya kazi ya ziada kumnadi.
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment