DEMOKRASIA
imefafanuliwa kuwa ni Serikali ya watu inayoendeshwa na kusimamiwa na watu kwa
ajili ya watu wenyewe.
Lakini
kwa Wanasosholojia, wao huiangalia jamii kwa mtazamo wa kiuhusiano zaidi ambapo
umoja wa kijamii ni kielelezo madhubuti cha uhusiano mzuri na ustaarabu wa
jamii husika. Kwa mtazamo huo, demokrasia ni uhusiano kati ya watu, jinsi
wanavyochukuliana na kutatua au kumaliza tofauti zao; na pia kati ya watu na
serikali.
Demokrasia ya kweli
inampa kila raia mtu mzima, mwenye akili timamu, haki ya kushiriki katika
utawala na katika uamuzi wa serikali yake. Lakini kwa kuwa si rahisi
kuitisha kikao chenye kushirikisha watu wote kwa shughuli hii (kama ilivyokuwa
enzi za mababu wa demokrasia – Wayunani), jamii imebuni mfumo wa demokrasia ya
uwakilishi (“representative“ au “elective democracy“) ambapo watu huchagua
wachache miongoni mwao wanaofikiri ni wazuri sana(aristoi) kuliko
wengine katika kusimamia mambo kwa niaba ya hao wengi.
Kwa
jinsi hii, demokrasia ni aina fulani ya utawala unaojumuisha haki ya
kuwakilishwa na haki ya kusemewa katika masuala yanayowagusa
wanaowakilishwa. Uwakilishi huo huongozwa na Katiba ya nchi ambayo ni
“msahafu“ au mkataba unaotungwa na wananchi kufafanua namna serikali yao
inavyopaswa kuongoza.
Kuibuka
kwa vyama vya upinzani kama njia moja ya mabadiliko ya Kikatiba ni tukio muhimu
la kisiasa nchini mwetu na barani Afrika, ambapo tangu enzi za uhuru mfumo wa
demokrasia ya Chama kimoja ulitawala. Lengo kuu la mabadiliko haya ni
“uwajibikaji“ kwa watawala ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa, unaosimamia
uhuru wa mawazo na fikra tofauti bila ya kugombana.
Lakini,
pamoja na hilo, mabadiliko hayo hayajaondoa ukweli kwamba, demokrasia kwa raia
hivi sasa imefungwa kwenye rumande ya vyama vya siasa kiasi kwamba raia
amewekewa masharti yanayomnyima haki ya kuchaguliwa au kushiriki katika utawala
wa nchi, isipokuwa kupitia vyama vya siasa (Katiba ya nchi – Ibara 39 (c) na 67
b ).
Lengo
hapa ni kuzuia demokrasia ya uwakilishi nje ya vyama vya siasa, kana kwamba mtu
hana uwezo wa kufikiri isipokuwa kwa nguvu ya vyama vya siasa; hivi kwamba
utawala sasa maana yake ni vyama vya siasa. Lakini kwenye vyama vya siasa huko
ndiko demokrasia inakouawa.
Baada
ya demokrasia ya uwakilishi kuhodhiwa na kudhibitiwa na vyama vya siasa (kwa
kupiga marufuku wagombea binafsi), kile kinachoitwa “vikao vya chama“ vimegeuka
machinjio ya demokrasia kupitia vikundi vya kidikteta vyenye uwezo kamili
kuzima matarajio ya watu katika uongozi.
Hii ni
pamoja na dhana mpya ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kwa mawaziri wa
serikali kuwajibika kwa Halmashauri Kuu (|NEC) ya CCM katika utendaji kazi wao,
badala ya kuwajibika kwa Rais wa nchi, kana kwamba serikali ni ya chama
kimoja!. Mawaziri wanawajibika kwa wananchi (Bunge) kupitia Katiba ya nchi, na
si kwa Chama cha siasa. Iweje Katiba ya Chama ichukue nafasi ya Katiba ya
nchi?
Vyama
kinzani vinaweza kuingia malumbano kwa “kujibu mapigo“, kama Mwenyekiti wa CCM
Taifa, Jakaya Kikwete, alivyowaelekeza makada wa CCM hivi karibuni. Lakini
isiwe “kujibu mapigo“ tu hata penye ukweli;huko ni kukwaza maendeleo, kwani
“ukweli“ hauna Chama wala itikadi.
Ni
Mwalimu Julius Nyerere aliyetuonya katika kitabu chake “TUJISAHIHISHE“, kwamba,
“Ukweli una tabia moja nzuri juu yake; kwa wakubwa na wadogo, kwa marafiki na
maadui, “UKWELI“ ni ule ule kwa wote. Na tabia moja ya ukweli ni kwamba,
ukiubeza, siku zote utaujutia. UKWELI haupendi kubezwa wala kupuuzwa“.
Kwa
misingi ya demokrasia makini, ubora wa serikali ya nchi haupimwi kwa kigezo cha
kuwekwa madarakani na wengi (kwa ushindi wa kishindo), bali kwa kigezo cha
uhuru na uvumilivu inaotoa kwa wachache wanaotokea kutokukubaliana nayo, na
ambao vinginevyo, ni wazalendo wema tu wenye kuzingatia sheria za nchi.
Kwa hiyo, kigezo cha demokrasia makini sio ushindi wa kishindo, wala ushindi
huo si leseni ya kukiuka misingi ya utawala bora na utawala wa sheria.
Tunayo
mifano mingi; mmoja ni ule kwamba, Adolf Hitler wa Ujerumani, aliingia
madarakani kwa ushindi wa kimbunga kwa Chama chake cha NAZI, na nchi hiyo ikiwa
na Katiba nzuri kuliko zote barani Ulaya enzi hizo; lakini bado Hitler alitokea
kuwa dikteta mbaya mno ulimwengu huu umepata kuona. Hii ni kwa sababu
Wajerumani walibweteka na kuamini kwa makosa kwamba, demokrasia hupimwa kwa
kigezo cha vyama vya siasa. Hapo, udikteta wa serikali hugeuka kuwa udikteta wa
Chama, ukiwakilishwa na kikundi kidogo cha wahafidhina wa kichama.
Inachefua
leo chini ya dhana ya demokrasia ya vyama vingi, kusikia Viongozi wa Chama
fulani kutishia kuwafukuza kazi wakuu wa mikoa na wilaya (wanaoteuliwa kwa
mujibu wa Katiba ya nchi), watakaoshindwa kutii maagizo ya Chama, kana kwamba
Katiba ya Chama cha siasa ni sehemu ya Katiba ya nchi. Huo ni ubabe butu kutoka
kaburini, wa mzimu wa uliokuwa mfumo (mfu) wa chama kimoja. Kama wakuu hao wa
Kikatiba wanakubali hilo, heri wajiondoe wakahubiri vyama, badala ya kusimamia
kikatiba, maendeleo ya wananchi yasiyofungamana na itikadi za kivikundi za
vyama.
Uzalendo
ndio msingi pekee ambao demokrasia ya kweli, au mfumo wowote wa serikali
unaweza kufanya kazi. Uzalendo unajumuisha utii wa mtu kwa Katiba ya nchi
ambayo iko juu ya vyama vya siasa. Chama cha siasa kinapaswa
kufanya kazi ndani ya Katiba ya nchi. Vyombo vya dola si mali ya Chama cha
siasa, bali ni vya wananchi wote, wanachama na wasio wanachama wa vyama. Hivyo,
havipashwi kutumika kwa manufaa ya kisiasa.
Ukandamizaji
ni adui wa uzalendo; Chama hakiwezi kudai hatimiliki au kuhodhi uzalendo kuliko
Chama kingine. Huo utakuwa udikteta wa vikundi, kama si kulewa madaraka.
Wahenga walisema, madaraka yote hulevya; lakini madaraka makubwa zaidi hulevya
zaidi na kuhatarisha demokrasia.
Kwa
nchi zenye demokrasia komavu, uzalendo unaonyeshwa na vyama vyote vya siasa kwa
kupeperusha bendera ya taifa katika mikutano yake, sambamba na za vyama, na
kumalizia shughuli kwa wimbo wa taifa ambao hauna Chama.
Kikwazo
kwa demokrasia ya kweli hapa nchini ni kule kuichukulia siasa kama njia rahisi
ya kujipatia utajiri na nguvu za kiuchumi.Kwa watu hawa kuachia madaraka ni
suala la kufa na kupona, hata kama ni kwa gharama ya demokrasia, kwa sababu
kufanya hivyo ni sawa na kuachia utajiri. Hawa ndio wamehalalisha rushwa na
sheria tata ya uchaguzi kujijengea ngome. Uchaguzi siku hizi ni fedha, bila
hivyo, kwa masikini, haki ya kuchaguliwa haipo. Rushwa au “dau”
wanavyoita, maana yake ni pesa kwanza nchi baadaye; hapa ni kupata bora
viongozi badala ya viongozi bora.
Chaguzi
za kidemokrasia hufanya serikali iwajibike kwa watu. Sheria za uchaguzi
zinapashwa kuwa huru na za haki, badala ya kuweka mazingira yanayokaribisha
fujo na rushwa na kuua misingi ya uadilifu, uwazi na utawala bora.
Demokrasia
itashamiri vipi kama ilivyoshamiri kwa nchi zilizoendelea, wakati watu wetu
wanateseka kwa njaa, wanatembea peku kwa ufukara, ili mradi wengine wachache
wamiliki magari na majumba ya kifahari, wakila na kusaza?
Ili
serikali ipate uhalali wa kutawala (legitimacy), inapaswa kutekeleza mambo
yafuatayo: kupanua maendeleo ya kiuchumi; kujenga umoja wa kitaifa na kuongeza
uwezo wa serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya kijamii.
Uhalali
huu utayoyoma kama tutaruhusu demokrasia ife msalabani kwa jina la siasa za
vyama, uhasama wa vyama, ubinafsi, kulindana na kubinafsishwa kwa serikali na
kikundi kidogo chenye nguvu ya fedha.
Uhalali
huu utapotea pia kama tutaruhusu fedha inunue siasa na siasa inunue fedha,
kufanya uongozi na uchumi kuwa mikononi mwa kikundi cha matajiri. Kumetokea
nini leo, kwamba nafasi za chama tawala, ni jambo la kufa na kupona kwa wakuu
wa wilaya na mikoa, wafanyabiashara, mawaziri na vigogo wengine? Ni uchu
wa madaraka ya kisiasa. Lengo ni kununua utajiri na si kutumikia; maadili na
malengo ya taifa yanapotea haraka.
Kukosekana
tabia ya kukosoa na kukosolewa huzaa kiburi, maringo, majivuno, kunata,
uongozi kwa mkono wa chuma na uhaba wa uvumilivu; na hapo ndipo, ngoma hulia
sana ambapo mwisho wake ni kupasuka, kwani wale wanaojiona hawawezi kukosolewa
sasa hujihesabu kama miungu watu; maisha hugeuka ya kuabudu mashujaa wa bandia
ambao hupenda kuitwa “Waheshimiwa“ badala ya kuitwa “Ndugu“; wenye kutaka
kutumikiwa badala ya kutumikia. Ni kuthibitisha ukweli wa Karl Marx kwamba, “Chama
si chochote bali ni taasisi ya kitabaka kwa lengo la kunufaisha kikundi cha
kitabaka kiuchumi“.
Katika “TUJISAHIHISHE“,
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere anabainisha kuwa, tunapojadili masuala
yanayoigusa jamii nzima, ni vyema kujifunza kusikiliza hoja zinazotolewa na
wenzetu na kuzijibu kwa kuzikubali au kuzikataa, bila kujali zimeletwa na
marafiki au watu wasio marafiki zetu. Inapokuwa hivyo hapana sababu ya
“kujibu mapigo“ penye ukweli.
Kuna
sababu gani, kwa mfano, kukana au kukataa mchana kweupe, tuhuma za ufisadi
nchini zilizo wazi, kwa sababu tu zimetolewa na wapinzani? Tujue kwamba,
uzalendo hauna Chama wala itikadi; lazima tukubali yote yaliyo ya msingi kwa
taifa, bila kujali yanatoka kambi gani. Wanasiasa wasitangulize maslahi yao binafsi
na ya vyama vyao; muhimu ni maslahi ya taifa kwanza na watu wake, vyama
vya siasa baadaye. Tunaongozwa na Katiba ya nchi ambayo iko juu ya Katiba za
vyama na juu ya sheria zingine zote za nchi.
Wanasiasa,
tofauti na wanasosholojia na waandishi wa habari, ni watu waliopungukiwa
milango ya hisia na fahamu kuweza kunusa, kusikia au kuonja, kujua
kinachoendelea katika jamii; hawawezi kusoma alama za nyakati na maandishi
ukutani. Kuna misemo miwili ya Kihaya kuthibitisha hatima yao kwamba:
“ugonjwa unaomuua Mbwa haraka ni ule unaoziba pua,” kwa maana atakosa
hisia na kula sumu na kufa. Au kwamba, “Kumbikumbi akikaribia kufa, huota mbawa
na kuruka”. Lakini pamoja na hayo, je, haikusemwa kwamba “ngoma ikilia sana
hupasuka”? Ni lini wanasiasa watajenga utamaduni wa kujikosoa na kukubali
kukosolewa kwa uvumilivu ili wasishikwe ugonjwa wa kuziba pua?
Kwa
sasa tabaka hili haliwezi kuendelea kuishi au kuokolewa kwa njia ya utawala wa
serikali yenye kutenda haki; njia pekee kwake sasa liweze kuishi, ni kujihami kwa
kuhubiri injili ya ufisadi ili chama na serikali viache maadili ya kitaifa na
kuabudu kwenye madhabahu ya ufisadi, kama utamaduni mpya!
Source: Raia Mwema: Joseph Mihangwa
No comments:
Post a Comment