Ndugu zangu,
Maneno hayo juu yalipatwa kutamkwa na Martin Luther King ( Jr) alipokuwa gerezani.
Mwanadamu unapokuwa kwenye matatizo unawahitaji zaidi wanadamu wenzako, na hususan marafiki.
Moja ya hotuba bora kabisa kupatwa kutolewa na Julius Nyerere ni ile ya mwezi Oktoba mwaka 1978. Ni pale alipotangaza vita dhidi ya mvamizi Idi Amin wa Uganda.
Nilikuwa na miaka 12 tu. Nakumbuka niliisikiliza hotuba ile kutoka mwanzo hadi mwisho; neno kwa neno. Nikiri, kuwa Julius Nyerere alikuwa hodari sana kwenye rhetoric- sanaa ya kuzungumza.
Kwa mtawala, kuamrisha vikosi vya nchi yako kwenda vitani ni moja ya maamuzi magumu sana. Na wakati mwingine, hotuba ya kuamrisha vita yaweza kuamua hatma ya vita.
Kwenye hotuba ile, Julius Nyerere aliweka vema msingi wa hoja, ya kwanini, sisi , kama taifa, tulilazimika kwenda vitani.
Na akatamka yafuatayo yaliyosisimua na kuhamasisha vikosi na taifa kwa ujumla. Kwamba;
- Uwezo wa kumpiga Amin tunao...
- Sababu ya kumpiga Amin tunayo..
- Na nia ya kumpiga Amin tunayo...
Kisha akatoka nje ya mipaka yetu akitamka;
" Tunataka dunia ituelewe hivyo". Akaonyesha pia kuwa taifa lina marafiki kwa kutamka;
" Marafiki zetu kwanza tuacheni, tumwonyeshe mshenzi huyu!"
Naam, katika maisha, mwanadamu kuna wakati unalazimika kuingia vitani. Unalazimika kupambana kudai haki yako na kulinda hadhi yako. Hayo ni mapambano ya haki. Na vita ya kudai haki ni vita ya lazima kupiganwa.
Hapo mwanadamu anakuwa kwenye matatizo. Katika hali hiyo, anachohitaji mwanadamu ni kuungwa mkono na marafiki zake.
Katika hilo, kama alivyotamka Martini Luther King Jr, kwamba ukimya wa marafiki unaumiza zaidi kuliko kelele za maadui.
Na hilo ni Neno la Leo
Maggid Mjengwa,
Iringa.
No comments:
Post a Comment