MWENYEKITI wa Taasisi ya Kiislamu ya Imamu
Bukhary, Sheikh Khalifa Khamis ameishauri Serikali kuchukua hatua za
haraka kulinusuru taifa ili lisiingie katika dimbwi la umwagaji damu kwa
misingi ya chuki za kidini.
Hivi karibuni kulitokea matukio ya kuuawa kwa viongozi wa kidini mkoani Geita na visiwani Zanzibar ambapo Padre Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki aliuawa baada ya kupigwa risasi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Sheikh Khamis alisema vitendo vya mauaji ya viongozi wa kidini, uchomaji wa nyumba za ibada na vurugu za maandamano ya kila siku ya Ijumaa vinaashiria kuwepo kwa kikundi cha watu wachache ambao wamechoka kuishi kwa amani.
“Hatuamini kama mauaji hayo yametekelezwa na waislamu kwa sababu Uislamu unahimiza amani na unapinga waziwazi vitendo vya kinyama kama hivyo,” alisema Sheikh Khamis.
Sheikh huyo alisema kuna baadhi ya vikundi ambavyo vimekuwa vikiwatumia vijana wasiojua kitu kwa masilahi yao binafsi na kwamba vikundi hivyo vinaitia fedheha na aibu jamii ya Kiislamu kwa kulitumia vibaya jina la Uislamu.
Alisema vikundi hivyo vimekuwa vikivamia baadhi ya misikiti na kuiteka huku wakiigeuza mingine kuwa vituo vya kujifunzia kareti na kufanyia mikutano na hotuba za kuwahamasisha waislamu kufanya vurugu.
Alisema hakuna mahala ambapo Uislamu unafundisha
kujichukulia sheria mikononi, kupuuza au kutokuheshimu mamlaka ya dola
na vyombo vya sheria.
Alisema kitendo cha baadhi ya waumini wa dini hiyo kujitumbukiza katika maandamano ya kuishinikiza Serikali, mahakama na Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP) ili kumwachia kwa dhamana Sheikh Ponda na wenzake ni kinyume na taratibu za kisheria zilizowekwa katika kumpatia mtuhumiwa dhamana.
Mwenyekiti huyo aliwaasa waislamu wote Tanzania kuendelea kuilinda amani na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kufanikiwa kuwakamata wauaji na wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Pia aliishauri Serikali iache kufumbia macho matendo maovu na ya kuvunja sheria badala yake itumie uwezo na dhamira yake ili kudumisha amani iliyoko nchini.
source Mwananchi
No comments:
Post a Comment