MENGINE tuandikayo tulishayaandika zamani. Tunayarudia maana yanayotokea sasa ishara zake tulishaziona, isipokuwa, tu mahodari sana wa kupuuzia.
Nimepata kuandika ( Raia Mwema) juu ya nilichokiona Jumapili moja nilipokuwa nikipita mitaa ya Kariakoo. Pale kona ya Mtaa wa Nyamwezi na Narung’ombe nikamkuta kijana na mkokoteni wake. Alikuwa akiuza filamu na CD za kidini.
Kijana yule alikuwa akionyesha pia mkanda wa video. Mzungumzaji kwenye mkanda huo alikuwa akihubiri chuki. Ni kuanzia nilipoanza kumsikiliza hadi nilipoondoka mahali hapo.
Na watu, hususan vijana, waliuzunguka mkokoteni ule kusikiliza chuki ile ya kidini iliyokuwa ikipandikizwa. Ndipo tulipofikia. Kwamba mijini si tu kuna wanaouza sumu za panya na mende. Bali siku hizi kuna wanaosambaza bure, ’sumu za kijamii.’
Vyombo vinavyohusika vimebaki vikiwaangalia wenye kupandikiza mbegu hizi za chuki.Kosa kubwa tulifanyalo, ni kudhani yanayotokea Kariakoo au Unguja hayatuhusu wa Kinondoni, Iringa au Mwanza.
Nimepata kusimulia kisa cha mtego wa panya uliosababisha madhara hata kwa wasio panya.
Panya kwenye nyumba aliubaini mtego wa panya uliowekwa na mwenye nyumba uvunguni mwa kitanda. Panya yule akamwendea jogoo wa mwenye nyumba. Akamwambia: “Ewe jogoo, kuna mtego umewekwa uvunguni mwa kitanda. Tusaidiane namna ya kuutegua kabla haujatudhuru wote."
Jogoo akajibu: "Ondoka zako, mie mtego wa panya unanihusu nini wakati sina kawaida ya kufika uvunguni mwa kitanda?" Panya yule akaenda hadi kwa mbuzi wa mwenye nyumba. Akamwambia: "Ewe mbuzi mwema, unajua kuna mtego wa panya uvunguni mwa kitanda cha mwenye nyumba. Tusaidiane mawazo ya kuutegua kabla haujatudhuru sote."
Mbuzi akajibu: "Hivi tangu lini ukaniona nikiingia chumbani kwa mwenye nyumba? Mtego huo wa panya haunihusu mie mbuzi." Panya akaenda hadi kwa ng'ombe wa mwenye nyumba. Akamwambia: "Ewe ng'ombe wa Bwana, kuna mtego wa panya umewekwa uvunguni mwa kitanda. Tusaidiane mawazo namna ya kuutegua kabla haujatuletea madhara."
Ng'ombe akajibu akionyesha mshangao! "Sijapata kusikia jambo la ajabu kama hilo. Yaani, mie ng'ombe nidhurike na mtego wa panya ulio uvunguni mwa kitanda! Hilo halinihusu."
Basi, ikatokea siku moja, nyoka akaingia chumbani kwa mwenye nyumba. Katika kutambaa kwake uvunguni mwa kitanda, mkia wa nyoka ukanasa mtegoni. Kishindo kilisikika. Mwenye nyumba alikwenda kwa furaha akiamini hatimaye panya aliyekuwa akimsumbua sasa amenaswa. Hapana, ni nyoka aliyenaswa mkia. Na ni mwenye hasira pia. Akamng'ata mguu. Sumu kali akamwachia. Mwenye nyumba akafa.
Jirani wakafika msibani. Siku ya kwanza watu walikuwa wachache. Wakahitaji kitoweo. Akakamatwa jogoo wa mwenye nyumba. Jogoo akachinjwa. Siku ya pili watu wakaongezeka. Kilihitajika kitoweo pia. Akakamatwa mbuzi wa mwenye nyumba. Mbuzi akachinjwa. Na siku ya maziko watu wakawa wengi zaidi. Akakamatwa ng'ombe wa mwenye nyumba. Naye akachinjwa!
Ni jogoo, mbuzi na ng'ombe wa mwenye nyumba walioamini kuwa madhara ya mtego ule wa panya yasingewahusu wao. Walikosea. Panya alikuwa sahihi, na wala mtego haukumdhuru panya! Kuna cha kujifunza kutoka kwenye kisa hiki. Nahitimisha.
No comments:
Post a Comment