BAO lililofungwa na mshambuliaji Mbwana Samatta jana liliiwezesha timu ya Taifa, Taifa Stars kuichapa Cameroon bao 1-0 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa ya soka iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Samatta alifunga bao hilo kiulaini dakika ya 88 baada ya kuunganisha wavuni krosi iliyopigwa na Frank Domayo kutoka pembeni ya uwanja.
Bao hilo liliwanyong'onyesha wachezaji na viongozi wa Cameroon, ambao baadhi yao waliinamisha vichwa vyao chini kwa majonzi na wengine kurusha mikono hewani kwa hasira.
Ushindi huo haukuwa wa kubahatisha kwa Taifa Stars kwani ilionyesha kiwango cha juu cha soka na kuwapa raha mamia ya mashabiki waliofurika kwenye uwanja huo.
Mabeki wa kati, Aggrey Morris na Kevin Yondan walikuwa kisiki kwa washambuliaji wa Cameroon huku viungo Salum Abubakar, Domayo na Amri Kiemba wakicheza kwa uelewano mkubwa.
Katika kipindi cha kwanza, Cameroon ilidhibiti zaidi eneo lake la ulinzi na kiungo na kufanya mashambulizi machache ya kushtukiza.Katika kipindi hicho, Taifa Stars haikufanya shambulizi lolote la maana.
Taifa Stars ilifanikiwa kupata adhabu ya penalti dakika ya 27 baada ya beki, Ngoula wa Cameroon kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari. Hata hivyo, shuti la beki Erasto Nyoni wa Taifa Stars liliokolewa na kipa Effala Komguep.
Pierre Wome nusura aifungie bao Cameroon dakika ya 29 alipofumua shuti kali la mbali, lakini liligonga mwamba wa juu wa goli na kuokolewa na beki, Kevin Yondan.
Kuingia kwa Thomas Ulimwengu katika kipindi cha pili, aliyechukua nafasi ya Mwinyi Kazimoto, kuliongeza uhai kwenye safu ya ushambuliaji ya Taifa Stars na hivyo kuongeza mashambulizi kwenye lango la Cameroon.
Ulimwengu aliweza kuwachosha mabeki wa Cameroon kutokana na kuruka nao hewani, kutumia nguvu kugombea mipira na kuwakimbiza kwa kasi, tofauti na ilivyokuwa kwa Samatta na Mrisho Ngasa.
Taifa Stars ilipata nafasi mbili nzuri za kufunga mabao dakika ya 84 na 86, lakini zilipotezwa na Ulimwengu na Samatta kutokana na kukosa umakini.
Hii ni mara ya tatu kwa Taifa Stars kukutana na Cameroon. Zilikutana kwa mara ya kwanza mwaka 2009 wakati wa michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika za 2010, ambapo katika mchezo wa kwanza uliochezwa Dar es Salaam, zilitoka suluhu na ziliporudiana mjini Yaounde, Cameroon ilishinda mabao 2-1.
Taifa Stars iliutumia mchezo huo kwa ajili ya kujiandaa kwa pambano lake la michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014 dhidi ya Morocco.
Taifa Stars iliwakilishwa na Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Kelvin Yondan, Aggrey Morris, Salum Abubakar, Mrisho Ngasa, Frank Domayo, Mbwana Samatta, Mwinyi Kazimoto/Thomas Ulimwengu na Amri Kiemba
source Liwazo Zito blog
No comments:
Post a Comment