UTAFITI wa Taasisi ya
Utafiti kuhusu Kuondoa Umaskini (Repoa), kuhusu mabadiliko ya katiba, muungano
na madaraka umeonyesha kuwa asilimia 40 ya Watanzania wanataka Bunge lisimamie
mchakato mzima wa mabadiliko ya kupatikana Katiba Mpya.
Pia, utafiti huo umebainisha kuwa asilimia 88 ya Watanzania hawataki muungano
uvunjwe huku asilimia 23 wakitaka muungano huo uvunjwe.
Mtafiti Mshauri wa Repoa, Costantine Manda alibainisha hayo jana wakati wa
uzinduzi wa utafiti huo uliofanyika kati ya Mei 27 hadi Juni 30 mwaka jana.
“Utafiti wetu umetokana na maswali waliyoulizwa watu wa kada tofauti wapatao
2,400 ambapo mbali na asilimia 40 kutaka Bunge lisimamie kupatikana Katiba,
asilimia 25 wanataka Rais ndiye asimamie huku asilimia 18 ikitaka vyama vya
kiraia, asilimia 9 ikitaka mahakama na asilimia 6 ikitaka vyama vya siasa
vifanye hivyo,”alisema Manda.Alisema mbali na kuangalia upande huo pia wananchi
asilimia 54 wametaka mawaziri wote wasitokane na wabunge,hivyo uwekwe utaratibu
katika Katiba Mpya ya jinsi ya kuwapata mawaziri hao.
Manda alisema pia waliangalia watu kama wana maoni juu ya Rais kuongoza kwa
awamu mbili au la na kati ya wananchi hao waliohojiwa asilimia 87 walieleza
kuwa aongoze kwa awamu mbili huku asilimia 12 wakitaka asiwe na ukomo wa
kuongoza.
“Wengi wanaonyesha kuwa wanataka Rais aongoze kwa awamu mbili ila kuna wengine
ambao wanapinga hilo kama mnavyoona kwenye utafiti wetu,”alisema Manda.
Hata hivyo alisema wananchi asilima 85 wanakubali kufanyika kwa mabadiliko ya
katiba iliyopo na kati yao asilimia 71 wanasema ni muhimu iwe hivyo kwa kuwa
nchi inakoelekea hivi sasa ni kubaya.
“Lakini kuna wengine asilimia 19 wanaridhishwa na jinsi nchi inavyoongozwa hivi
sasa na demokrasia iliyopo,”alisema Manda.
source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment