WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, October 20, 2014

Yanga yabadilika mara tatu


Beki wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (aliyelala chini) akimzuia mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi wakati wa mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Timu hizo zilitoka 0-0. Picha na Emmanuel Herman 
Dar es Salaam. Licha ya kocha mkuu wa Yanga, Marcio Maximo kubadilisha fomesheni mara tatu katika mechi dhidi ya Simba, bado malengo yake hayakutosha kuisaidia timu hiyo kuondoka na pointi tatu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam juzi.
Mechi hiyo ya Ligi Kuu ya Bara ilimalizika kwa suluhu.
Katika mechi hiyo, Maximo alianza na fomesheni ya 4-2-3-1, akimtumia Jaja kama mshambuliaji pekee akisaidiwa na Haruna Niyonzima, Mrisho Ngassa na Andrey Coutinho, kabla ya kubadilisha na kutumia 4-4-2 iliyomuhusisha Ngassa na Jaja kama washambuliaji wawili na kisha kutumia 4-3-3 baada ya kuwaingiza Simon Msuva na Hamisi Kiiza kusaidiana na Ngassa katika mashambulizi.
Maximo alisema alilazimika kubadilisha fomesheni aliyoanza nayo kutokana na aina ya uchezaji wa wapinzani wao.
“Simba walitumia mabeki wanne na kiungo mkabaji mmoja juu ya mabeki hao, ikawa ngumu kwa wachezaji wangu kushambulia. Nikabadili fomesheni na kutumia 4-4-2 ambayo pia haikunisaidia kupata bao,” alisema Maximo.
Anasema fomesheni ya mwisho aliyotumia ni ile ya 4-3-3 ili kuongeza nguvu ya mashambulizi na kukaba katikati ya uwanja.
“Vijana wangu walitaka kufunga ila fomesheni waliyoitumia Simba, walikuwa na wachezaji wengi katikati na katika safu ya ulinzi, halafu walikuwa wakipiga pasi fupi na ndefu,” alisema Maximo.
Alisema: “Mabeki wa Simba walikaba wawili wawili, hawakumuacha mshambuliaji wa Yanga na beki mmoja, ila ni mara tatu tu ndiyo beki ya Simba ilitoa nafasi kwa washambuliaji wa Yanga, lakini nafasi hizo tulishindwa kuzitumia, Coutinho alipata nafasi mbili, Jaja alipata nafasi moja.”
Kocha wa Simba, Patrick Phiri alisema alitumia fomesheni ya 3-5-2 japo nafasi ya kiungo ilipwaya baada ya Jonas Mkude kuumia na kuingia Pierre Kwizera.
“Mkude alipotoka timu ilibadilika, ilipwaya katikati. Mkude ana uwezo wa kuchukua mipira na kuchezesha timu, pia anakaba, kuumia kwake ilikuwa pengo hata hivyo, timu ilicheza vizuri, lakini bado sijafurahia kiwango chake kwa kuwa hii ni sare ya nne,”alisema Phiri.
Wakati huo huo, JKT Ruvu imeichapa Tanzania Prisons 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya. Pia katika Ligi daraja la kwanza JKT Oljoro imetoka sare 1-1 na Mwadui kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha. Hata hivyo zilitokea vurugu mashabiki wakipinga mpira wa faulo ulioipatia Mwadui bao la kusawazisha.
(Imeandaliwa na Imani Makongoro, Bertha Ismail na Godfrey Kahango).
source: mwananchi

No comments:

Post a Comment