WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, October 9, 2014

NINI HASARA YA DEMOKRASIA MATAYARISHO YA KATIBA MPYA JAMUHURI YA MUUNGANO TANZANIA?


Demokrasia imefafanuliwa katika namna mbalimbali; wengi wa wanazuoni wameeleza  kuwa “Demokrasia ni mfumo wa utawala ambao watu huwachagua  viongozi wa serikali yao wenyewe na kuainisha jinsi inavyopaswa kufanya kazi”. Wakaendelea kukufafanua kuwa “ Demokrasia hukuza ustawi wa watu wote kwani Kila raia ana haki ya kushiriki katika uendeshaji wa shughuli za umma na katika mambo yote yanayoathiri maisha yake”.wengi wa wanazuoni wanakubalia kuwa Demokrasia inauwezo mkubwa wa kushugulikia  uwajibishaji serikali kupitia kura za maoni  na maamuzi yanayofanywa na wawakilishi wao katika vyombo mbalimbali vya maamuzi”.Kwa maneno mengine Demokrasia ni  mkataba wa kijamii kati ya wananchi na watawala(serikali); mkataba huu ni wa pande mbili raia wana wajibu wa kutekeleza sehemu yao na serikali pia inawajibu wa kuwatendea raia matakwa yao. Kwa maneno mengine ni mkataba wa kijamii unadhihirisha uaminifu na matumaini ambayo raia  wanakuwa nayo kwa wawakilishi wao ili watende kwa niaba yao.na pale wanaposhindwa kufanya majukumu ambayo jamii iliyowachagua imewapa wananchi wanayo nafasi ya kuwachagua wawakilishi wengine.


Swali la msingi chimbuko la demokrasia ni nini?

Tunafahamu kuwa lengo kubwa la demokrasia ni kuleta mabadiliko kwa wananchi wake, ili kuwaletea maisha mazuri, kuwatoa  kwenye dimwi la umasikini na kuwaletea maisha bora kwa jamii nzima na sio kikundi kidogo cha watu; kwa msingi huu ukifuatwa vizuri na kutekeleza kwa ufanisi ni ukweli usiopingika kwamba mfumo wa utawala wa kidemokrasia una umuhimu wake katika  maendeleo ya jamii nzima.

Je demokrasia inatumika wakati wote?

Hili ni swali lenye changamoto kubwa; lakini ni lazima ieleweke na tujiulize kuwa  ni wakati gani demokrasia inapaswa kutumika na wakati gani siyo muhimu kuitumia; Nasema hivyo kwa sababu siyo wakati wote ni muhimu ama lazima kutumia mfumo wa demokrasia umaohusisha maamuzi ya wengi, ndani ya  uendeshaji wa serikali na maamuzi yake; mfano mzuri ni uamuzi ambao uliwahi tolewa Mheshimiwa Raisi Kikwete baada ya kukutana na wawakilishi wa vyama vya siasa na kukubaliana kuwa mchakato wa kupata katiba mpya utakao husisha maoni ya wananchi utaendelea baada ya uchaguzi ujao.  Uamuzi huu umekuwa tofauti na uamuzi wa awali kuwa Katiba mpya itapatikana kabla ya uchaguzi 2015.

Je msingi wa demokrasia ni nini?

Msingi wa demokrasia inawapendelea sana walio wengi kwa kukubali mawazo ya wengi. Usahihi wa hoja mara nyingi sio jambo muhimu kuliko wingi wa ufuasi. Walio wengi katika kufikia muafaka wa jambo kulingana na demokrasia ndio washindi wa demokrasia hata kama hawana hoja

Je hasara ya demokrasia ni nini?
Demokrasia inaangalia uwingi wa wawakilishi na sio lazima hoja zinazotolewa, hata kama hoja hazina mantiki lakini zina ungwa mkono na wengi zinafanyiwa maamuzi na hatimaye yanaonekana kuwa sahihi.

Hasara hii ya demokrasia tunaweza kulinganisha na mwenendo wa upatikanaji wa katiba mpya ambao umekamilika huko Dodoma hivi karibuni.
kinachoangaliwa katika kufikia upatikaji wa katiba mpya umekuwa ni wa wawakilishi ndani ya bunge la Katiba, kwa mfano katika nchi yetu ya Tanzania “Chama cha Mapinduzi (CCM) kina wajumbe wengi katika Bunge la Katiba kwa hiyo  Msingi wa wingi wao ni ushindi walioupata katika uchaguzi halali wa kisheria na kidemokrasia”

 
Kutokana na mazingira haya, mjadala wa upande mmoja uliokuwa unaendelea bungeni ulikuwa halali, hata kama UKAWA waliamua vikao vya bunge hilo. Walichofanya UKAWA ni mbembwe za siasa za kususia ili pengine kupata huruma ya wananchi lakini kimsingi walitakiwa kuendelee kujenga hoja ili kuwafanya walio wengi wabadilishe mawazo yao na wananchi weelewe msingi wao wa hapana ni nini.

Naamini kuwa UKAWA walikuwa na hoja walitakiwa kufa kiume katika ushindani wa hoja Bungeni;  kwa maneno menginehii ndio demokrasia ya ushindani iliyoletwa kwetu na warumi na tukaikubali na kuona ni chombo sahihi cha maamuzi. Ndio hasara ya demokrasia lakini kwa kuwaachia wenzao uwanja wamewanyima wananchi ushindani wa hoja za pande mbili.

Hata kama UKAWA watafanya mikutano ya kupinga katiba nje ya vikao halali vya Bunge inakuwa ni hadithi, ni simulizi ya upande mmoja ambao hauna usindani.

Ushindani wa hoja kati ya wanasiasa na kati ya vyama vya siasa inatakiwa ieleweke kama ustawi wa jamii husika. Kwa kuwa tofauti ya hoja haitakiwi ilete  utengano na hatimaye migongano, bali iwe ni sehemu ya kuleta maendeleo ndani ya jamii husika; kwani demokrasia ya ushindani itakayo ishia katika kuleta vurugu na ugomvi ndani ya jamii itaathiri maendeleo ya jamii na kuongeza maisha magumu kwa jamii husika hivyo kubadilisha mfumo huu na kuingia katika mfumo wa kikatili

 

Utawala wa demokrasia unatakiwa utufundishe namna ya kupanua fikra za wawakilishi wetu. Demokrasia inatakiwa iwe mkombozi wa fikra na kuwapa wananchi uhuru wa kufikiri, uhuru wa kutenda na hata wa kwenda kinyume na fikra za kikale. Ili jamii iweze kuendelea na iwe na demokrasia iliyopevuka ni muhimu wananchi wawe na uhuru wa kuweza kuasi kisiasa na kuwa na fikra zisizofuata mkondo wa fikra za kawaida za wanajamii.

 

Tofauti za hoja baina ya wafuasi wa vyama tofauti  ndani ya mfumo wa demokrasia huzaa chuki ambayo inajengwa kati ya watawala na wapinzani dhidi ya wananchi kila upende ukijaribu kushinda  hisia za wananchi ambao ndio wenye nchi. Ni wajibu wa wananchi kuamka  na kuwa  imara na kukataa mbwebwe za wanasiasa.

 Tunatakiwa kuanza kuhoji mambo ambayo tunaona kuwa sio ya kweli. Inafurahisha kwa sasa ndani ya Tanzania  kuwa mwamko wa wananchi wetu kwa sasa umebadilika na wananchi wameanza kuonyesha dalili ya kuelewa Zaidi nini wanataka hasa kuhusiana na maendeleo yao.
 

Tukiweza kuepukana na itikadi za matukio  na polojo za matukio na udaku: Lazima tukubali kuwa kila chama cha siasa Tanzania tupende au tusipende kina uzuri wake na ubaya wake, lakini la msingi katika mantiki ya demokrasi lazima tukubali kuwa chama ambacho kimefanikiwa kuingia mkataba wa hiari na wananchi wa kuongoza nchi ndicho kimefanikiwa kupata ridhaa ya kuongoza ndipo tunapona hasara ya demokraisa pengine matendo yao hayakubaliki na wachache ambao wanafikiri kuwa nao wana mwelekeo tofauti na wenye tija kwa jamii. Kwa msingi huo ni kuwa  tofauti za siasa na wanasiasa katika jamii haziwezi kuepukika na wakati mwingine unyama wao unaotokana na tofauti zao za kutamani kuhodhi madaraka unapelekea kuiangamiza  jamii ambayo haina kosa kutokana tu na uelewa wao mdogo;


Napenda katika hitimisho la Makala yangu nimshukuru sana Mheshimiwa Raisi Kikwete na Mheshimiwa Ally Mohamed Shein wamekuwa wasikivu, wavumilivu  na walezi wa demokrasia ya kweli kwa  kuendelea kuvishirikisha vyama na asisi zote ambazo zimefika mahala na kukinzana na serikali zetu zote mbili ili kufikia muafaka kwa kusikiliza mawazo ya wachache bila  kinyongo na hata wakati mwingine kubadilisha  msimamo wa wengi na kufuata mawazo ya wachache.
 

Hapa tunaona  Sifa mojawapo ya demokrasia ya kweli ni kwamba: inawapatia wachache VILEVILE nafasi ya kisheria ya kuwashawishi wengi waone ubora wa maoni yao hata kama hawakubaliani nayo. Demokrasia ya namna hii ndiyo njia pekee ya kuleta mawazo mapya katika jamii kwa njia ya amani na utulivu. Hii ndio sifu kubwa ya viongozi wa serikali zetu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Dr. Mohamed Ally Shein

Lazima tukubali kuwa demokrasia in faida na hasara yake na kamwe sio kila mtu ataridhika na maamuzi ambayo yataendelea kutolewa katika uwajibikaji wa pamoja.

 

Mungu Ibariki Tanzania

No comments:

Post a Comment