WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, September 27, 2012

Hakuna mtu wa kuzuwia mabadiliko



Na Abdallah Vuai,  Zanzibar
Dunia ni uwanja wa fujo, kila mwenye ngoma yake aingie acheze, maneno haya yametamkwa karne nyingi zilizopita, katika safu hii  nimeyatumia maneno hayo kulinganisha na mabadiliko ya mifumo ya kisiasa hapa duniani.

Mwishoni mwa miaka ya tisinini tulishuhudua namna ujamaa ukianguka kwa kasi kubwa na ile kambi ya Mashariki ikilazimika kubadili mwelekeo wa chombo chake.


 Pamoja na mabadiliko hayo, wapo wanasiasa wasiokubali mabadiliko ya jambo katika jamii,mara nyingi huitwa “Muhafidhina” ambao kwa hapa Zanzibar Muhafidhina wapo,lakini sio wengi sana.
Muhafidhina wamekuwa wakijaribu kupotosha ukweli kwa maslahi binafsi ya kisiasa na ya kujaza tumbo, utawasikia wakitamka kwamba Zanzibar itarejea kwa Waarabu!!

Tishio hilo wanadhani kuwa lina nguvu na linaweza kuwatio woga vijana kutopaza sauti zao kutoa maoni kwa mambo muhimu ya nchi kama mabadiliko ya katiba ya Tanzania na mfumo wa Muungano wanaoutaka.

Itakumbukwa kuwa Jamhuri ya watu wa Zanzibar ilianzishwa baada ya Mapinduzi ya 1964 iliyomaliza  Utawala wa Usultani wa Zanzibar ambapo mwezi mmoja baadaye Taifa huru la Jamhuri ya Watu wa Zanzibar likajiunga na Jamhuri ya Tanganyika. Sultan wa mwisho kutawala Zanzibar ni  Jamshid bin Abdullah Al Said ambaye kwa sasa anaishi Portsmouth,Uingereza akiwa na umri wa miaka 82.


Kabla ya Mapinduzi Zanzibar haikuwa Jamhuri, ilikuwa chini ya Sultan,lakini Mapinduzi  ya umma ndio yaliyoifanya Zanzibar kuwa Jamhuri. Umoja wa Mataifa uliyatambua Mapinduzi hayo kuwa ni halali na uliokuwa Umoja wa nchi huru za Afrika(OAU) ulitambua pia Mapinduzi hayo.

 Masharti ya uanachama wa Umoja wa Mataifa yapo wazi na pia mkataba wa Muungano baina ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika upo Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na ni mkataba wa Kimataifa ambao kuvunjika kwake kumeelezwa wazi katika sheria za Kimataifa.

 Sasa ikiwa ombi la vijana na wananchi walio wengi kutaka muundo wa Muungano kama wa EU kila nchi itarejea kukaa kwenye kiti chake sio Sultan maana Ban-Kimoon hamtambui Jamshid anaitambua Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ndio iliyoungana mwaka 1964.

Kwa hivyo, hakuna njia wala upenyo kwa Sultan kurejea kuitawala Zanzibar wala Umoja wa Mataifa kumpa kiti kule New York akikalie,atakaa kwa misingi ipi na kwa hoja gani?
Visiwa vya Zanzibar sio pekee vilivyofanya Mapinduzi, Ufaransa imefanya Mapinduzi, sasa nayo UN watarejesha kiti kwa mfalme Louis XVII?

Mapinduzi ya Ufaransa ni jina linalojumlisha matukio muhimu ya siasa kwa kipindi cha miaka 10, tangu 1789 hadi 1799, yaliyobadilisha uso wa Ufaransa na utamaduni wa Ulaya kwa jumla.

Athari zake zilienea kote duniani kama fikra za haki za binadamu, uhuru na maendeleo ambapo  dhana ya kuwa mamlaka ya dola ni haki ya raia, si ya wafalme wala watawala wengine, ilienea polepole pande zote za dunia na ilipofika Januari 12,1964 Wazalendo wa Zanzibar chini ya Afro Shiraz Party walirejesha heshima na utu kwa wakulima na wakwezi.

Vugu vugu la mabadiliko lilianza baada ya Wafaransa kuchoshwa ugumu wa maisha huku watu wachache wakinufaika kama ilivyo kwa nchi yetu Muhafidhina wanaonekana kuneemeka na migogoro ya kisiasa kwa kuwatumilia vijana kwa kupandikiza chuki na hasama miongoni mwao.

Madeni makubwa yaliyokuwa yakiikabili Ufaransa kwa wakati huo ilisababisha Mwaka 1789 mfalme Louis XVII   kuitisha Bunge  kwa mara ya kwanza baada ya miaka 170. Wananchi walilalamika kwamba matumizi makubwa ya mfalme pamoja na gharama za vita vya uhuru vya Marekani vilivyosaidiwa na Ufaransa dhidi ya Uingereza kumewabebesha mzigo Wafaransa.

Tangu Louis XIV (1643–1715) wafalme waliotawala Ufaransa bila Bunge, lakini kisheria mfalme hakuwa na madaraka ya kuongeza kodi bila idhini ya bunge, na Louis XVII hakuwa tena na nguvu ya kutosha kupuuza utaratibu huo.

Kutokana na vurugu za kisiasa na mfumuko wa bei za chakula, wananchi wa Paris waliasi wakashambulia gereza la Bastille na kuibomoa. Mfalme aliyedhoofika hakutaka kukandamiza uasi huo na Bunge la taifa liliendelea kubadilisha sheria kwa kufuta haki za pekee za waungwana. Mashambani wakulima walianza kuasi na kukataa ulipaji kodi katika mikoa mbalimbali.

Mfalme alipoona kwamba madaraka yake yanapungua zaidi na zaidi alijaribu kuondoka lakini alikamatwa na kurudishwa kama mfungwa mwaka 1791.

Mwelekeo mkali kati ya wabunge ulipata ushindi na 1792 Ufaransa ulitangazwa kuwa jamhuri. Mfalme alishtakiwa kuwa msaliti wa Taifa akapewa hukumu ya kifo na kukatwa kichwa pamoja na mke wake  Januari  21, 1793 .

Vijana wa Zanzibar na pengine Tanzania nzima sasa wanataka mabadiliko, hawatafanya kama wale wa Ufaransa isipokuwa watatumia haki ya kutoa maoni kukataa ukandamizaji wa hoja na maoni sahihi katika mwelekeo wa Muundo wa Muungano wanaoutaka ambao kwa mtazamo wa wengi wanatamani kama ule Umoja wa Ulaya.

Saa ya mabadiliko imefika, vijana wasiokuwa na ajira, uhakika wa chakula, kulala wamefikia pahala wanataka kuona mabadiliko ya kweli yanatokea sio tu katika siasa bali hata katika uchumi na ndio maana wanataka Muungano wa Kiuchumi zaidi kuliko mfumo ulipo wa Serikali mbili tena katika mkataba wa kikatiba.

Ni lazima Muhafidhina wafahamu kuwa ulimwengu wa vijana haukubali tena kuburuzwa na mara nyingi vijana wa kileo waliozaliwa katika Tenknohama wanaunga mkono siasa yenye uchumi na Wanazuoni wanaipima hoja hiyo katika  mizania  miwili mosi  msukumo binafsi wa kijana wa Zanzibar wa uhitaji wa mabadiliko.

Pili ni mhemko wa majira (seasonal emotions/exctitement). Mhemko huu ni kama kilevi  ambapo kama ukweli ulivyo idadi kubwa ya  vijana ndio wanjwaji ambao hawatapenda kunywa kilevi kisichokuwa na stim yoyote kwao kama kile cha Kihafidhina.

Demokrasia ya kisasa inalazimisha kuheshimu maoni ya mwengine hata kama huyataki ndio maana watu makini wanaamini kuwa uvumilivu  mzuri ni ule unaojiepusha na chuki zisizo na msingi (prejudice).

Hata kama anayetoa maoni  au kueleza ni yule msiyeafikiana, au kimaumbile si mzungumzaji mzuri jaribu kuuweka sawa ujumbe huo. Zingatia "alichokizungumza siyo namna alivyozungumza". Mara zote chuki isiyo na msingi huviza mabadiliko.

Ikiwa dhana ya ujana ndio nguvu ya mabadiliko katika jamii, Muhafidhina waliozeeka kifikra na kimwili hawawezi tena kutumia mbinu  chafu tena za kizamani kuwapotosha vijana au kuwatumia kwa kuendeleza chuki.

Kwa kutambua dhana hiyo, Chama cha Mapinduzi kiliwahi kuelezea siku za nyuma dhamira yake ya mabadiliko katika Idara zake na Maofisa huku viongozi wake wakijitayarisha kukikabidhi Chama hicho kwa umma wa Vijana kuongoza na wao kubaki kama washauri.

Katika operesheni hiyo, CCM imetenga bilioni 7 kuwaondoa watumishi wasiokuwa na uwezo wasiofundishika na viongozi mzigo, bila shaka fagio la chuma litafagia uozo uliosheheni CCM na katika hili Muhafidhina siku zao zinahesabika.

Tumeshuhudia vyama vya Upinzani viongozi wao vijana, CUF yupo Ismail Jussa, CHADEMA Zitto Kabwe, CCM Bara yupo Januari Makamba na Nape Nnauye ambao utawapata kwa anuani za barua pepe,kwenye mitandao ya kijamii.

Iwapo maoni ya vijana yatapuuzwa au kunyamazishwa kwa aina yoyote ile, CCM itambue kuwa inapaswa kujiandaa kuishi maisha mapya ya kambi ya upinzani mwaka 2015 na Vuai ndio atakuwa Naibu Katibu Mkuu wa kwanza akiwa Chama pinzani.

Kama nilivyoeleza awali kwamba mara nyingi  sifa kuu ya ujana kama rika ni kuwa na mapenzi katika mabadiliko. Kufanya mambo au kuwa na vitu tofauti na mazoea. Huo ndio ujana daima ambapo Muhafidhina wamekuwa wakitaka kuendeleza mwenendo wao kwa mazoea.

Hali ilivyo hivi sasa ni ya upepo mkali wa mabadiliko ya kisiasa ambapo tumeshuhudia Mataifa kadhaa ya Afrika yakishindwa kuhimili vishindo vya mabadiliko hususan kwa wanasiasa ving'ang'anizi hivyo  anayedhani kuwa , amesimama ajitazame asianguke kama alivyoanguka Hosni Mubarak,Gadaff na wengineo.

Kwa kuthibitisha hilo, tumeona namna kura ya maoni iliyofanyika mwezi Julai mwaka 2010  iliamua kuzika kabisa siasa za chuki Zanzibar huku Wahafidhina wakibaki vinywa wazi wengine ukiwatazama hata kwenda mbio hawawezi pale panapotokezea balaa! Mungu aepushe mbali nchi yetu iendelee kubaki na amani na utulivu daima.


Bado tunakumbuka namna Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye kwa wakati huo akiwa Rais wa Zanzibar alipata ukinzani mkali uliosababishwa na kukolezwa chumvi na Wahafidhina, vipeperushi vya kumkejeli  vilimwaga.

Viongozi wengine waliokuwa wakiunga mkono umoja na mapatano walihesabiwa kuwa ni vibaraka wa Hizbu huku wengine wakiambiwa walikuwa Hizbu tangu zamani,lakini jambo la kushangaza Wahafidhina hao hao ndio waliokwenda kuomba vyeo kwa chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Pamoja na Wahafidhina wa siasa za chuki kuanza kuhaha kila kona, Karume hakutishwa wala kukatishwa tamaa na hali hiyo na hatimaye  kaburi la siasa za chuki, uhasama wa kulipiza kisasi Zanzibar likachimbwa na marehemu siasa za mti kwa macho kuzikwa humo na hivi sasa hakuna hata anayemuombea dua.

Matokeo ya kura ya maoni iliyoamua mfumo wa muundo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yanathibitisha kuchoshwa kwa wananchi na siasa za chuki kwani waliosema ndio walikuwa 175,476  sawa na asilimia 66.0 na waliosema hapana ni 90,588 sawa na asilimia 34.0 .

Vijana wengi walipiga kura ya ndio kutaka mabadiliko huku Muhafidhina wakipinga bila mafanikio na ndivyo utabiri wangu kuhusu anguko lao katika mabadiliko mapya ya muundo wa Muungano kuwa kama ule wa Umoja wa Ulaya.

Takwimu za Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba idadi ya watu zaidi ya bilioni 6, kati ya hao asilimia 80 ikiwa ni vijana. Kwa kigezo cha wingi pekee hatuwezi kupuuza kuwa vijana hawawezi kuwa nguvu ya mabadiliko. Mathalani Afrika Mashariki tu ina jumla ya watu wapatao 126 milioni, kati ya hao asilimia 70 ni vijana.

No comments:

Post a Comment